Habari

Kifo cha ZANTEL Chakaribia

Zanzibar Telecommunication Company kama inavyojulikana Zantel ni kampuni iliyoanzishwa Zanzibar, huku Serikali Ya Zanzibar ikiwa na shear yake. Hii ni kusema fedha za wananchi walipa kodi ndizo zilizotumika kuanzisha shirika hili.

Ingawa sehemu kubwa ya shear hizo ni za kampuni binafsi, zilizopambiwa kwa mapambo ya serikali kiasi kuonekana kama vile kampuni hii ya Wazanzibar. Huku ikibeba jina “Zanzibar” wananchi wengi wamekuwa watiifu (loyally) kwa kampuni hii.

Pamoja na udhaifu mwengi ulioko katika utendaji, huduma, utaratibu mbovu, nk Huna nyimbo ya kumwambia Mzanzibar abadili matumizi ya simu yake, kabisa hakubali kubadili na kujiunga na kampuni nyengine za simu.

Udhaifu mkubwa uliofanywa na Zantel ni pale ilipoamua kuhamisha makao yake makuu kutoka Zanzibar na kuyapeleka Tanganyika. Hii ilikuwa aidha kwa kukusudia au njama zilizojificha, huku watendaji wa Zanztel wa wakati ule kushindwa kuimaizi siri nzito. Naam baada ya kufika Tanganyika, shirika lilianza kuingiza kwa wingi watendaji kutoka huko.

Hadi hivi sasa shirika hili linayumba kiutendaji, kihuduma, hata uhusiano wake na wateja umekuwa ukiporomoka siku hadi siku.

Sasa hivi jenenza la Zantel linatayarishwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanzisha mfumo mmoja wa kulipia gharama (tarrif) za matumizi ya simu kwa wateja wa kampuni zote. Hili litawaathiri Zantel kwa vile wanawateja kidogo kuliko makampuni mengine ya Tanganyika. Halkadhalika itapelekea gharama za bei ya simu kupanda, hivyo kutokana na udhaifu na kutokuwa na huduma bora ukilinganisha na makampuni mengine wateja wengi watahama Zantel.

Bado uongozi wa Zantel uko kwenye usingizi, hawajuwi nini kinaendelea wala hawajajiweka tayari lakini ninachokiona mimi kifo cha Zantel kinakaribia.

Share: