Habari

Kilio kodi ya ushuru chapatiwa dawa

JUNE 22, 2017 BY ZANZIBARIYETU
Kilio kodi ya ushuru chapatiwa dawa

Aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha muswaada wa sheria ya ushuru wa stempu itakayochukua nafasi ya sheria ya ushuru wa stempu namba 6 ya mwaka 1996 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Alisema, muswada huo utasaidia wafanyabiashara wadogo kulipa kodi kwenye taasisi moja tu yaani ZRB ambapo viwango watakavyolipia vimepunguzwa ikilinganishwa na kiwango cha jumla wanacholipa sasa TRA na ZRB.

Aidha, alisema kimsingi wafanyabiashara wadogo hulipa kodi maalum ya wafanyabishara wadogo chini ya sheria ya kodi ya mapato inayosimamiwa na TRA na kulipa ushuru wa stempu unaosimamiwa na ZRB.

Alisema, chini ya utaratibu huo wafanyabiashara wamekuwa wakilamikia gharama za ulipaji kwa kutakiwa kulipa kodi katika taasisi mbili tofauti kwa bidhaa moja na kusababisha kupata hasara.

Alisema kwa upande mwengine ushuru wa stempu hukusanywa katika mauzo yasiyostahiki kulipiwa kodi ya ongezeko la thamani ama kwa kusamehewa kutokana na kufikia kiwango cha kusajiliwa chini ya VAT.

Alisema madhumuni na sababu ya muswaada huo ni kupatikana sheria mpya ya utozaji kodi ya ushuru wa stempu itakayoleta ufanisi katika kukusanya kodi, kuimarika kwa usimamizi wa ukusanyaji kodi na kuongezeka mapato ya serikali.

Alitaja madhumuni mengine ni kuingizwa hati na nyaraka zilizokua hazikuainishwa katika sheria ya ushuru wa stempu iliyopo pamoja na kuainishwa kwa hati na nyaraka zinazopaswa kutozwa ushuru wa stempu na mtu anaestahili kulipa ushuru huo.

Alisema, faida nyengine zitakazopatikana ni kuwepo utaratibu bora zaidi na viwango maalum vya kutozea kodi kwa wafanyabiashara wadogo wa bidhaa na huduma na kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa ukusanyaji kodi kwa wafanyabishara waliokua hawakusajiliwa katika kiwango cha VAT.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi kuhusu muswaada huo, Mjumbe wa Kamati hiyo, Simai Mohammed Said, alisema muswaada huo utaleta ufanisi zaidi katika ukusanyaji mapato yatakayosaidia katika shughuli mbali mbali za kuwafikishia wananchi huduma za msingi.

Hata hivyo, alisema ili kujenga mazingira rafiki baina ya serikali na walipa kodi na kuepusha ukandamizaji kwa wafanyabiashara kamati inashauri kupewa uwezo Kamishna wa Bodi ya Mapato kufanya tathmini ya mauzo ya mlipa kodi na kumbadilishia kiwango anachopaswa kulipia ikitokezea mauzo yake yameshuka.

Wakati huo huo, Wawakilishi waliupitisha muswaada wa sheria ya kuweka vifungu vya uanzishaji wa kodi itakayojulikana kama ushuru wa bidhaa na huduma zinazoingizwa na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Chanzo: Zanzibar Leo

Share: