Kitaifa

Bodi yafungia Hospitali tatu, nyengine yafutiwa leseni.

Na Fatma Kassim, Maelezo

BODI ya Ushauri wa Hospitali Binafsi imezifungia hospitali tatu, na kuifutia usajili hospitali moja kwa  kushindwa kutekeleza maagizo waliyopewa na Bodi hiyo ya kuondosha pamoja na kuondosha kasoro mbali mbali.

Hospitali zilizofungiwa ni pamoja Latifah Cliniki iliyopo maeneo ya Kwalinato, Kitope Roman Catholic iliyopo maeneo ya Kitope pamoja Changongo iliyopo maeneo ya Kwaboko.

Msaidizi Mrajis wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi Dk Shaaban Seif Mohammed ameitaja Hospitali ya Neema Clinic iliyopo maeneo ya Tomondo kuwa imefutiwa usajili kutokana na kupinga taratibu za Bodi hiyo.

Alisema kuwa Hospitali ya Latifah, imefungiwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wenye sifa na Daktari dhamana wa Hospitali hiyo kutohudhuria jambo linaweza kuhatarisha afya za wanaofika kupata matibabu Hospitalini hapo na hospitali Changongo ambayo inajishughulisha kwa tiba ya meno imefungiwa kutokana uchanfu.

Aidha Dk Shaaban amefahamisha kuwa kwa Hospitali ya Kitope Roman Catholic hawana wafanyakazi wenye taaluma ya fani ya afya ambapo tayari huko nyuma wameshapewa taarifa ya kutafuta wafanyakazi wenye taaluma lakini hawajatekeleza agizo hilo  na bodi hiyo imeamua kuifungia mpaka watakapotekeza.

Alifahamisha kuwa Bodi pia inatoa tahadhari kwa Hospitali ambazo mpaka sasa hazikakata kibali cha kuendesha huduma hizo kukata kibali  haraka iwezekanavyo ili waweze kutoa huduma kama inavyotakiwa.

Alisema iwapo wamiliki hao hawatokata kibali cha kuendeshea huduma hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa na pamoja na kuzifungia kabisa hospitali zao hizo zisiweze kutoa huduma kwani zinaweza kuhatarisha afya za wananchi.

Alisema Vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Hospitali Binafsi si vizuri na vinaenda kinyume na maadili ya utoji wa huduma za Afya hali inayoweza kurudisha nyuma maendeleo ya serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii.

Alisema Serikali imekuwa inachukua juhudi kadhaa katika kuhakikisha Hospitali Binafsi zinatoa huduma zenye ubora kwa wananchi kwani zinasaidia sana katika kupunguza misongamano kwenye hospitali za Serikali.

Ametoa tahadhari  kwa wananchi kuwa waangalifu wanapokwenda   hospitali hizo kuwa na kuacha mara moja kutotumia Hospitali ambazo zina kasoro za utoaji huduma za afya

Amefahamisha Bodi itaendelea kufanya   ukaguzi wa mara kwa mara hospitali hizo ili kuhakikisha zinafanya marekebisho ya kasoro walizonazo.na iwapo watakaidi bodi haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuzifungia moja kwa moja na kuwapelekeka katika vyombo vya sheria.

Share: