Habari

Kuelekea Zanzibar ya viwanda

March 10, 2018

Dk. Shein aonesha dira
Aitaka UNIDO kuongeza nguvu

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), kuiunga mkono katika dhamira ya Zanzibar kuwa na viwanda vidogo na vya kati.

Rais Dk. Shein alieleza hayo jana alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Li Yong aliyefika Ikulu mjini Zanzibar.

Alimueleza Mkurugenzi huyo mikakati iliyowekwa na serikali ya Mapinduzi katika kuhakikisha sekta ya viwanda inaimarika.

Alisema tayari serikali imeandaa mipango na kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya viwanda kwa kutambua umuhimu wake katika kuchangia uchumi na kutoa fursa ya ajira hasa kwa vijana.

Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano wa muda mrefu kati yake na UNIDO na kuahidi kuuendeleza.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 imezielekeza serikali kuelekea katika uchumi wa viwanda, ili iwe ukombozi wa kuwapatia fursa zaidi za ajira vijana na kuimarisha uchumi.

Alisema kuwa hatua za UNIDO kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya viwanda ina umuhimu mkubwa na itasaidia katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Alisema kuwa miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa ni kuimarisha kilimo cha mwani ambacho kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi, lakini zipo changamoto zinazokikabili kilimo hicho, hivyo kuna haja kwa UNIDO kutoa ushirikiano wake katika eneo hilo.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imezungukwa na bahari na pia, ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA), lakini bado haijazitumia vyema rasilimali zinazotokana na bahari kwa kutokuwa na viwanda vinavyotegemea mali ghafi na rasilimali za bahari.

Hata hivyo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo hatua na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Zanzibar inaanzisha Kampuni yake ya Uvuvi na kueleza haja kwa UNIDO kuunga mkono jitihada hizo.

Dk. Shein alimueleza Mkururugenzi Yong kuwa Zanzibar inawakaribishwa wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta ya viwanda, vikiwemo viwanda vya samaki na rasilimali za bahari.

Zanzibarleo

Share: