Habari

KUMBUKUMBU: Maalim Seif/CUF dhidi ya adui CCM na viongozi wake

Picha: Maalim Seif Sharif Hamad ambaye tarehe 22 Oktoba 2016 alitimiza umri wa miaka 73, alizaliwa tarehe hiyo, mwaka 1943. Maalim Seif ni kipenzi cha Wazanzibari kwa asalimia 79.5 wanoishi ndani na asilimia 91.03 wanaoishi nje ya Zanzibar.

Habari iliyopo chini, Julius Mtatiro anaeleza ni kwa kiasi gani Maalim Seif na CUF kwa ujumla wanavyokumbana na changamoto nyingi za uadui zinazotengenezwa na kuratibiwa na Serikali za CCM ya Zanzibar na ya Muungano kupitia viongozi wa awamu zote za serikali hizo.

Changamoto hizo bado zinaendelea na kwa dalili zote zimeanza kuonesha kuwa awamu hii ya tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli, imefurutu ada na mipaka dhidi ya Maalim Seif na CUF.

Ushahidi wa hilo, tafuta hotuba za Dk Magufuli, alizozitoa miezi mitatu iliyopita kwenye uwanja wa Kibandamaiti, Unguja na ile ya uwanja wa Gombani, Pemba.

Dk Magufuli ni Rais wa Tanzania, aliyeshindwa kuficha ubaya na chuki zake za moyoni dhidi ya Maalim Seif. Ni dhahiri yanayotokea sasa, kupitia msajili wa vyama vya siasa, kupitia vitendo vya polisi na kadhalika ni maagizo ya Dk magufuli.

Wahenga wana msemo kwamba: “Nyota njema huonekana asubuhi” Maalim Seif ni nyota njema iliyoonekana tangu asubuhi. Kwa hivyo, Dk Magufuli na wenzake wote wataendelea kufanya ubaya dhidi ya Maalim Seif na CUF, wakichoka wataangusha manyanga chini.

Kwa ufupi ni kwamba, DUNIA itafika mwisho au niseme KIAMA kitawadia lakini CCM kwa Unguja na Pemba haiwezi kuja juu tena, kinachofanyika ni mabavu ya dola.

Tangu uchaguzi wa mwaka 1995 mpaka uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana 2015 CCM Pemba, imepoteza uwakilishi kutoka kwa wananchi. Hali hiyo inabainisha kuwa, kwa Zanzibar, CCM imebakia ghaito kukata roho.

Huo ulikuwa utangulizi wangu, lakini njama, ubaya na uadui vinavyofanywa na serikali za CCM, dhidi ya Maalim Seif na CUF soma KUMBUKUMBU iliyowekwa hapo chini na Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa CUF Kamati ya Uongozi Taifa.

Na Julius S. Mtatiro
Ijumaa, Novemba 25, 2016

….NIWAKUMBUSHE wasomaji mwanamama mmoja aliyejulikana kwa jina la Anjelina Levarasi a.k.a ‘Anjelina Mrema. Alivuma sana nchini.

Huyu alidaiwa kuzaa na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augsutine Mrema. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilijua fika jambo hilo, lakini ni baada tu ya Mrema kujiengua kwao.

Anjelina alitoka na kutangaza hilo hadharani na CCM ikamdaka kuendeleza kampeni chafu hiyo kwa kumtumia ili kumvunjia staha Mrema; wakati huo akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Mwanamama huyo alikwenda nyumbani kwa Mrema kudai hili na lile. Alifikia hatua ya kuvua nguo zote na kubaki uchi. CCM wakachekelea.

Hata hivyo, Anjelina alifika mwisho bila kupata cha maana kutoka CCM waliomtumia. Mwishowe alikuja kufa kifo cha kusikitisha akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni (guest house) bila ya msaada wowote. Waliokuwa wakimtumia hawakumsitiri.

Michael Nyaruba aliyekuwa kiongozi mwandamizi Chama cha Wananchi (CUF), ni mfano mwingine. Hakuwa mali kitu kwa CCM hadi pale alipokosana na viongozi wa CUF.

Alihamia CCM ambako alionekana lulu. Akatumiwa kuvuruga CUF. Alijinasibu kujua siri za aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF wakati huo, Seif Sharif Hamad, ambaye sasa ni katibu mkuu wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Siri alizodai kuzijua zikihusisha viongozi wa CUF zikatumika kutengeneza “kesi ya uhaini” Zanzibar. Nyaruba alikuwa anakwenda Zanzibar kama mfalme.

Akikodishiwa hadi ndege na kuandaliwa mikutano ya hadhara uwanja wa Malindi, kwa ufadhili wa iliyokuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Rais aliyejipachika jina la Komandoo, Dk. Salmin Amour.

Siyo tu alihudumiwa usafiri na matumizi kwa safari za kwenda na kurudi Zanzibar kuandaa ushahidi dhidi ya Maalim Seif ili ashitakiwe mahakamani, bali pia alipewa ulinzi mzito.

Hakufika mbali. Aliishia tu mtu wa kutumwa na kazi yake ilipoonekana haina tena tija, akatelekezwa na CCM. Kwa kuwa angali hai, mwenyewe anaweza kueleza haya vizuri zaidi.

Mtu mwingine wa mfano huo ni Salum Msabaha Mbarouk, kijana aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, jimbo la zamani la Mkunazini, kupitia CUF.

Wapinzani wa CUF walipofanikiwa kumlaghai, alidai ametekwa katika tukio ambalo halijawahi kuelezwa bayana mpaka leo.

Alidai amefichwa kusikojulikana na mara moja akamtaja aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Idi Pandu Hassan akidai kuwa alihusika.

Wakati huo alishatangaza kujiuzulu uwakilishi. Hapo CCM ikaona imepata. Ilimtumia Msabaha ili kuidhoofisha CUF. Hatimaye alijiunga na CCM ili maisha yaendelee kwa kuwa jamii ilianza kumchukulia ni msaliti.

Watatu hao wanatosha kuonyesha kuwa CCM ina jadi ya kutafuta watu wa kudhoofisha nguvu za upinzani, lakini baadaye hukwama huku wakikosa walichokitarajia.”

Mwandishi wa Makala nzima ni Mbasha Asenga, ilichapwa kwenye Gazeti la Mwanahalisi, Tarehe 30 Mei 2012. Mimi nimenyofoa kipande tu, kwa hisani ya Ali Baraka Kh.

JSM..

Tagsslider
Share: