Habari

KUMBUKUMBU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR 2

Enzi za Washirazi
Hizi ndio enzi za mwanzoni zinazokumbukwa vyema na wanahistoria. Wanahistoria wengi wanathibitisha madai ya wazee wa kale kwamba watu wa mwanzo kuhamia mwambaoni na katika visiwa vya Zanzibar ni washirazi. Inadaiwa kwamba bwana mmja aitwae Hassan Bin Ali, “nguo nyingi” aliondoka shiraz Iran na ukoo wake kwa kutumia majahazi saba ambayo yalichukuiwa na upepo na kuchomoza katika sehemu mbali mbali za pwani ya Afrika ya Mashariki ambapo moja ya mjahazi hayo liliwasili Zanzibar. Watu hawa ndio walianzisha kizazi cha kishirazi katika mwambao. Profesa Abdulsherif, mwanahistoria na msomi maarufu wa Zanzibar anaetegemewa na ulimwengu kwa tafiti za bahari yote ya Hindi anahoji kuweo kwa ushirazi wa watu hawa na anakubaliana na hoja kwamba hawa walikuwa ni washirazi kwa kufikia kwao Shiraz Iran wakitokea bara Arab, hususan Oman. Majina ya mkabia yao, maumbile yao, majina yao na staili ya ujenzi wa nyumba zao walizozijenga, mambo yote haya yanaakisi uarabu zaidi kuliko ushirazi. Majina ya makabila ya mamwinyi wa washirazi ni kama vile Al-alawi, Al-bajuni, Al-addibawy, Al-bahasany, Al-ahdali, Al-attasi n.k, ambayo bila shaka ni makabila ya waarabu na sio waajemi (Issa 1999).

Kama tulivyokwisha kueleza huko nyuma kuwa Mwinyi Mkuu alitokana na washirazi hawa waliohamia sio Zanzibar tu lakini katika mwambao wote wa Afrika ya Mashariki maema mno kabla ya kuingia kwa wageni wengine kutoka ndani ya bara la Afrika na Asia. Washirazi walimtambua mtawala wao kama mwinyi mkuu. Wahadimu, wapemba (wadiba) na watumbatu ndio hasa historia inaowaita washirazi wa Unguja na Pemba. Wahadimu walikuwepo katika maeneo ya Kaskazini ya kisiwa cha Unguja na walikuwa wakiishi kwa wingi katika maeneo ya Nungwi, Kijini, Muyuni, Pwani mchangani, Chwaka, Bwejuu, Makunduchi, Kizimkazi na Uzi. Mji mkuu, au mji muhimu wa wahadimu ulikuwa ni Dunga. Watumbatu walikuwa wakiishi katika maeneo ya kisiwa cha Tumbatu. Pia watumbatu walionekana kuishi maeneo kama vile Donge, Bumbwini na Mwanda (Ingrams 1962).

Ukoloni wa Mreno
Wareno ni katika wakorofi walioweza kujimilikisha sehemu nyingi sana za ulimwengu. Vasco Da Gama, Mchunguzi wa kiren alifika katika pwani ya Afrika ya Mashariki na kutia nanga katika sehemu zote za mwambao ikiwemo Unguja na Pemba. Vasco Dagama alizikuta tawala za mwinyi mkuu zikiwa dhaifu na hivyo kueleka taarifa Ureno ziizopelekea wareno kuja kuutawala mwambao. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 16 wareno walizipiga vita tawala zile za kienyeji za washirazi na washwahili za miji ya pwani ya Afrika mashariki na kuziweka chini ya himaya yao. Matokeo ya utawala wa wareno ni kuzorota kwa bidhaa za dhahabu na biashara nyengine. Ustawi wa miji ya pwani halkadhalika ulididimia kabisa. Kuanzia mwaka 1506 hadi mwaka wa 1698, kipindi cha miaka mia na tisini na mbili (192) au takriban karne mbili, miji ya mwambao, ikiwemo kisiwa cha Pemba pamoja na mwenzake, Unguja, vilivamiwa na kuwekwa chini ya ukoloni wa wareno. Washirazi walijaribu sana kupambana na wareno ikiwemo mapambano ya Mombasa yaliyopelekea wareno kuichoma moto mombasa yote. Hata hivyo jamii iliyooonekana kuambana zaidi na wareno ni wapemba. Wakati wa ukoloni wa kireno wapemba walikuwa wakifanya ubishi mara kwa mara katika suala la kulipa kodi kwa mkoloni huyo na mwishoni waligoma kabisa kulipa (Gray 1962: 171-2). Huu ndio ule unaoitwa ukaidi wa wapemba. Bila ya ukaidi wa namna hii, na misimamo ya namna hii katika kupambana na maonevu mbali mbali ya ukoloni, Zanzibar pengine isingeliweza kujikomboa katika miaka ya 1960. Kibaraka wa wareno huko Pemba aliuliwa na wapemba wote walihama kisiwa na kukimbilia Mombasa Kenya (Ingrams 1962).

Wareno waliyafanya mengi ya uonevu na ukandamizaji kwa watu wa visiwa hivi kama vile kuzisafirisha rasilimali na kuwalipisha raia kodi zisizo na masilahi kwao. Wareno nao wameacha athari kaika ustaarabu na utamaduni wa wazanzibari kama vile mchezo wa ng’ombe ulio maarufu sana huko Pemba. Katika Afrika mashariki nzima iliyotawaliwa na mreno ni wapemba peke yao waliorithi utamaduni huo.

Utawala wa kisultani
Zipo hadithi kuwa waomani waliijiingiza wenyewe Zanzibar kwa kutumia mafungamano ya kibiashara na pole pole kuanzisha utawala wao. Katika hadithi hii waomani wanadaiwa kumlazimisha aliyekuwa Mwinyi Mkuu wa wakati huo, Hassan bin Ahmed mkataba uliotambuwa utawala wa Omani kwa Zanzibar. Kutokea hapo Mwinyi Mkuu alibakia na kazi ya kukusanya kodi tu na kuwasilisha kodi hizo kwa Sultani. Kwa kuwa mafakhari wawili hawakai zizi moja, uhasama ulizuka baina ya Mwinyi mkuu na Sultani. Uhasama huo ulipelekea Sultani kutokuwa na imani tena na Mwinyi Mkuu na hivyo kusimamisha kabisa utawala huo wa kimwinyi. Zipo hadithi zinazosema kwamba Sultani alimwita Mwinyi Mkuu nyumbani kwake Maruhubi kwa kisingizio kwamba yeye Sultani alikuwa mgonjwa. Mwinyi mkuu akiambatana na askari wake walifika Maruhubi kuitikia mwito wa Sultani lakini hatima yake Sultani alimuuwa Mwinyi Mkuu na askari wake na huo ukawa mwisho wa Mwinyi Mkuu. Hata hivyo ushahidi wa uhakika juu ya hadithi hii haujathibitishwa.

Hapa kwanza hapana budi ifahamike kwamba mreno pia aliitawala Oman. Katika mwaka wa 1650 waomani walifanikiwa mapambano ya kumng’oa mreno huko Oman. Kuna simulizi za zamani zinazodai kuwa wenyeji wale wa Zanzibar walioishi chini ya mamwinyi wakuu na watu Oman walikuwa na udugu- wa damu, yaani wote walikuwa wamenasibika na uarabu. Hivyo waliwaomba ndugu zao wa Oman waje wawasaidie ili na wao wamtoe mreno Zanzibar. Haya ni madai ya wale wanahistoria wanaosisitiza kwamba wenyeji wale walioitwa washirazi (wahadimu, watumbatu na wapemba) na bado wangali wanaitwa washirazi ambao waliotawaliwa na mreno bila shaka walikuwa ni waarabu, ndio wakawa ni rahisi kwao kuomba msaada kwa waarabu wenzao (Amrit Wilson 1986). Katika simulizi hizo panadaiwa kwamba ilikuwa ni mababu zao waliofanya safari wakenda Oman kutafuta msaada wa Sultani katika mapambano yao ya kuutoa ukoloni wa kireno Zanzibar. Waomani waliitikia wito wa ndugu zao wa Zanzibar na walifika kutoa msaada wa mapambano ya kumng’a mreno. Baada ya mapambano ya waomani na mreno, wareno wakatolewa Zanzibar mwishoni mwa karne ya 17. Aliyeongoza mapambano yale ni Imam Sultan bin Seif, Al-yarubi. Baada tu ya kumuondoa mreno, utawala rasmi wa kifalme wa kiarabu, chini ya mfalme, Sultan bin Seif ukawekwa. Baada ya hapo Mwinyi Mkuu alifanyanya makubaliano ya hiari na Sultani kuendelea kutawala ijapokuwa yapo madai kwamba makubaliano hayo yalikuwa ni kwa kipindi maalum. (reference).

Utawala huo ulidumu kuanzia 1698 mpaka 1744. Baada ya hapo kulizuka mapambano ya muda mrefu ya waarabu wenyewe kwa wenyewe huko Oman baina ya kabila la Al-yarubi na Al-Busaidi. Mwisho wa mapambano waarabu wa kabila la Al-busaidi wakafanikiwa kuwashinda Al-yarubi na Seyyid Ahmed bin Said Al-busaidi akaweka ufalme wake rasmi wa Oman na Zanzibar kuanzia mwaka 1744 mpaka 1783. Seyyid Ahmed bin Said aliitawala Afrika ya mashariki yote kwa ufalme wake kwa kutumia mfumo wa maliwali (governors). Sehemu za Afrika ya mashariki alizotawala Seyyid Ahmed bin Said ni Zanzibar, Pemba, Lamu na Kilwa kwa mfumo wa maliwali wa kibusaidi waliokuwa na utiifu kwake. Kabila moja tu la Mazrui ndilo lililokuwa likitawala Mombasa kama maliwali wenye utiifu kwa Seyyid Ahmed bin Said Al-busaid.

Katika mwaka wa 1746, kabila la Mazrui waliidai Mombasa iwe huru chini ya himaya yao ikitokana na utawala wa kiomani wa kabila la Al-busaidi. Wamazrui hao waliwapiga vita mabusaidi na wakafanikiwa kuikamata Mombasa na kuiweka chini ya mamlaka yao. Kipindi hicho hicho, Wamazrui wakapigana vita vikali na mabusaidi na wakafanikiwa pia kuwang’oa mabusaidi katika kisiwa cha Pemba. Pemba nayo ikawa chini ya utawala huo wa mmazrui ikiwa makao makuu ya utawala ni Mombasa. Kutokana na umuhimu wa Pemba wakati huo, Wamazrui waliita Pemba “granary of Mombasa” yaani shehena ya chakula cha kulishia utawala wote wa Mombasa wa Mmazrui ilikuwa ikitoka Pemba. Inasemekana kabila hili la Mazrui ni miongoni mwa makabila ya kiarabu yenye ukali wa kivita na ushujaa wa kupigana. Kuanzia hapo Pemba ikawa katika Utawala wa pamoja na Mombasa ya Kenya. Hii ndio sababu mpaka leo waarabu wa kabila la Mazrui wanaonekana kwa wingi kisiwani Pemba na Mombasa Kenya. Katika mwaka wa 1753, Mazrui hawa walijaribu kutaka kuivamia na kuipora Zanzibar (sasa Unguja) kutoka kwa mabusaidi wa Oman na kuidhibiti wao kama vile walivyofanya kwa Mombasa na Pemba lakini liwali wa Kibusaid wa Zanzibar (sasa Unguja) alifanikiwa kuushinda uvamizi huo wa kimazrui, na wamazrui kushindwa kutekeleza azma yao.

Baada ya kufariki Seyyid Ahmed bin Said, ufalme mpya wa Seyyid Sultani bin Ahmed katika mwaka 1792 ukaanza. Kutokana na tishio la Ufaransa kuiteka Muscat, Seyyid Sultan bin Ahmed alianzisha urafiki na waengereza kwa ajili ya ulinzi. Ili kupata ulinzi huo waengereza walimtaka Seyyid Sultan bin Ahmed kutiliana saini mkataba wa kuiruhusu Uengerza kufanya biashara na kupitisha misafara ya meli zake katika eneo la Ghuba. Mkataba ulisainiwa katika mwaka 1798. Pamoja na mkataba huo uliofungwa, Uengereza iliutumia urafiki huo ili kumshurutisha Seyyid Sultan bin Ahmed kuifunga biashara ya utumwa Zanzibar. Seyyid Sultan bin Ahmed inasadikiwa aliuliwa kwa mashirikiano kati ya watoto wake wawili Salim bin Sultan na Said bin Sultan.

Baada ya kufariki Seyyid Sultan bin Ahmed, utawala mpya wa mtoto wake Seyyid Said bin Sultan ukawekwa. Utawala huu ulianza mwaka 1804 na kumalizika mwaka 1856. Huyu ndiye Sultani ambaye wanahistoria wengi humzingatia kama sultani wa mwanzo wa Zanzibar. Seyyid Said bin Sultan alipendelea kuuendeleza na kuutia nguvu zaidi uhusiano wa urafiki kati yake na Uengereza ulioanzishwa na baba yake. Alifanya hivi kwa kutarajia kwamba Uengereza ingempa kila aina ya msaada wa kumg’oa mmazrui Mombasa. Alipochukuwa ufalme tu, Seyyid Said akawapa onyo wale maliwali wote waliojinyakulia madaraka wenyewe katika zile nchi walizopewa kuzilinda wakati wa utawala wa babu yake, Seyyid Ahmed bin Said. Katika mwaka wa 1822 Seyyid Said akafanikiwa kuiweka Pemba katika utawala wake kutoka katika mikono ya wamazrui wa Mombasa. Katika mwaka wa 1823 Seyyid Said aliwaomba waengereza hifadhi ili aweze kumng’oa mmazrui kutoka Mombasa. Kutokana na kushindikana kwa makubaliano kati ya Seyyid Said na waengereza Seyyid Said alinyimwa hifadhi hiyo na badala yake waengereza walitoa hifadhi hiyo kwa wamazrui wa Mombasa dhidi ya Seyyid Said. Hivyo Mombasa ilitangazwa rasmi kama mahmia ya Uengereza katika mwezi wa Julai 1826.

Seyyid Said alianzisha mahusiano ya kidilmasia, kirafiki na kibiashara kati yake na Marekani. Seyyid Said aliutumia urafiki huu na hivyo kupelekea kufungwa kwa mkataba wa ulinzi na biashara kati yake na Marekani. Kwa kutumia msaada mkubwa wa Mmarekani Seyyid Said alifanikiwa kuwafurusha wamazrui na kuiteka na Mombasa katika mwaka wa 1837. Seyyid Said bin Sultan, aliweka utawala wake rasmi wa Oman na Dalwat Zinjibar. Dalwat Zinjibar ni Zanzibar iliyokuwa ikijulikana hapo mwanzo, yaani Afrika mashariki yote pamoja kuanzia kaskazini (Somalia) mpaka kusini (Ruvuma) vikiwemo ndani yake visiwa, tawala na miji yote kama Mogadishu, Merka, Barawa, Kismayu, Pate, Lamu, Malindi, Mombasa (Mvita), Tanga, Bagamoyo, Zanzibar (sasa Unguja), Pemba, Tumbatu, Kilwa, Mafia, Sofala na sehemu nyengine nyingi za mrima na mwambao wote mpaka Congo.

Kwa muda wote huo Zanzibar na Oman zilikuwa na uzalendo wa pamoja ulio rasmi, yaani nchi moja. Uzalendo wa pamoja kama nchi moja baina ya Oman na Zanzibar ulikatika enzi ya utawala wa Seyyid Majid bin Said alipompinga kaka yake mkubwa, Seyyid Thuwein bin Said na kutaka lazima atawale yeye Zanzibar baada ya kifo cha baba yao, Seyyid Said bin Sultan. Suala la Seyyid Majid bin Said kutawala Zanzibar, lilipangwa kupita chokochoko za wajerumani na waingereza pale walipomuahidi Seyyid Majid kuwa atakuwa mfalme wa Zanzibar badala ya kaaka yake endapo atakubali kuzitoa baadhi ya sehemu za Dalwat Zinjibar na kuzikabidhi kwa wakoloni hao. Azma hiyo ilitimia na Seyyid Majid akatawala Zanzibar na utawala wake ukaanza rasmi tarehe 19 Oktoba mwaka 1856. Seyyid Thuwein akazuiwa kuchukua ufalme kwa nguvu za waengereza na wajerumani na kwa usaliti wa ndugu yake na hivyo kulazimishwa kubaki mfalme wa Oman pekee.

Seyyid Thuwein alichukua ufalme wa Oman mwaka huo huo wa 1856 hadi alipofariki katika mwaka 1866. Kuanzia hapa ndipo Oman na Zanzibar zikawa dola mbili tofauti, yaani Zanzibar na ufalme wake na Oman na ufalme wake. Seyyid Thuwein alirithiwa na mwanawe Seyyid Salim katika mwaka 1866 ambae nae alirithiwa na mwanawe Seyyid Turki katika mwaka wa 1871. Seyyid Turki alifariki katika mwaka wa 1888 na hivyo ufalme kurithiwa na mwanawe Seyyid Feisal. Baada ya kifo cha Seyyid Feisal, Seyyid Taimur alirithi kiti cha ufalme katika mwaka wa 1913. Ufalme wa Seyyid Taimur ulidumu hadi mwaka wa 1932 ambapo alifariki na kurithiwa na Seyyid Said. Inasemekana kufuatia dhiki kubwa huko Oman wakati wa utawala wa Seyyid Said, mtoto wake Seyyid Qaboos aliamua kumpindua na kuchukua kiti cha ufalme katika mwaka wa 1970.

Kwa upande wa Zanzibar, wakoloni waliendeleza ubabe wao dhidi ya dola hiyo ya Zinj na hivyo kuendelea kuimegua kidogo kidogo huku wakigawana kwa kuweka mipaka mipya huku na kule. Katika mwaka wa 1886, wajerumani na waingereza wakatiliana saini rasmi mkataba wa kuitambua Zanzibar kuwa ni visiwa vya Unguja, Pemba, Lamu, Mafia, na sehemu ile ya mwambao wa pwani kutoka mto mninjani mpaka kipini, kwa kuingia ndani masafa ya meli kumi (10) tu. Mwisho wa safari ya kumegwa kwa dola ya Zanzibar ilimalizikia na visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Utawala wa kifalme wa kurithishana wa kabila la kiarabu la Al-busaidi ukaendelea kwa Seyyid Barghash Bin Said kuchukua ufalme tarehe 7 Oktoba mwaka 1870 baada ya kifo cha Seyyid Majid. Baada ya kifo cha Seyyid Barghash Bin Said, Seyyid Khalifa Bin Said akarithi ufalme tarehe 26 Machi mwaka 1888. Tarehe 13 Februari mwaka 1893, Seyyid Ali Bin Said akarithi kiti cha ufalme kutoka kwa kaka yake Seyyid Khalifa. Baada ya kifo cha Seyyid Ali, Seyyid Hemed Bin Thuwein akarithi ufalme tarehe 5 Machi 1893. Baada ya kifo cha Seyyid Hemed, Seyyid Khalid akatithi ufalme kwa lazima bila ya ruhusa ya waengereza tarehe 25 Agosti mwaka 1896 jambo lililopelekea vita vya Alhamisi kati yake na waengerza baada ya siku mbili kutolewa katika kiti cha ufalme na kuwekwa Seyyid Hamoud Bin Muhammed siku ya tarehe 27 Agosti 1896. Vita vya Alhamisi na matokeo yake vitazungumzwa zaidi baadae katika kitabu hichi. Baada ya kifo cha Seyyid Hamoud, Seyyid Ali Bin Hamoud akarithi kiti cha ufalme tarehe 18 Julai 1902. Baada ya kifo cha Seyyid Ali Bin hamoud, Seyyid Khalifa Bin Haruob akarithi ufalme tarehe 9 Disemba 1911. Huyu ndie mfalme aliyesifiwa sana kwa utwala mzuri Zanzibar ambapo takriban wazanzibari wote waliridhika na utawala wake na hivyo kupendwa sana na raia zake. Baada ya kifo cha Seyyid Khalifa, Seyyid Abdalla Bin khalifa akarithi kiti cha ufalme tarehe 17 Oktoba mwaka 1960. Baada ya kifo cha Seyyid Abdalla Bin khalifa, Seyyid Jamshid Bin Abdalla akarithi kiti cha ufalme mwaka 1963. Huyu hakuufaidi ufalme kwani baada ya kipindi kisichotimia mwaka mmoja wa utawala wake alitolewa Zanzibar na Mapinduzi ya 1964 ambayo yatazungumzwa hapo baadae.

Wafalme hao waliotawala Zanzibar na walio na asili zao kutokea Oman waliifanya Zanzibar kuwa ni kwao na sio koloni lao. Waliipenda Zanzibar na waliwapenda raia zao. Waliwaoa wenyeji wao, yaani watu weusi na kuzaa watoto machotara. Kila karne zilivyokuwa zikipita ndipo hata ule uarabu wa asili ulivyokua ukipotea ndani ya aila hiyo ya kifalme hadi kufikia na wao kutokua na tofauti yoyote na aila nyengine za kizanzibari. Hata ngozi zao zilikuwa nyeusi kama walivyo washirazi na waafrika. Suala la kwamba waomani waliwavamia wenyeji wale wa Zanzibar na kuwatawala halina nguvu ya hoja. Hii inatokana na kwamba hakuna mapigano yoyote yaliyoelezwa na historia ambayo yaliwahi kutokea baina ya Mwinyi Mkuu na waomani hao kuonyesha kwamba Mwinyi Mkuu hakuukubali utawala huo wa waomani. Halkadhalika mafungamano ya maisha ya watu, uhusiano kati ya waomani na Mwinyi Mkuu na watu wake na hata kudumu kwa utawala wa kifalme kwa miaka mingi bila upinzani wowote kutoka kwa wenyeji ni ushahidi wa wazi kwamba Mwinyi Mkuu na watu wake waliupokea utawala wa waomani kwa hiari.

Wafalme waliwapenda raia zao na waliwalinda na kuwahudumikia kwa mapenzi makubwa. Wafalme wa Zanzibar walifanya kila wawezalo kuwaletea maendeleo raia zao ijapokuwa baadhi ya wakati walionyesha kuwapendelea zaidi waarabu wenzao. Raia pia waliheshimiwa na haki zao kuthaminiwa. Wafalme hawakuwa wakiwatesa wala wakiwauwa raia zao. Utumiaji wa madaraka ulidhibitiwa. Ipo hadithi maarufu kuhusiana na udhibiti wa mamlaka ya wafalme ulivyokuwa. Hadithi hii inamsimulia mjukuu wa kifalme aliewacha kufanya kazi ya nyumbani aliyopewa na mwalimu wake. Mawalimu aliwaadhibu kwa bakora wanafunzi wote walioshindwa kufanya kazi hiyo ya nyumbani aliyowapa. Baadhi ya wanafamilia ya kifalme walikasirika na kuamua kumchukulia hatua mwalimu kwa kumdhalilisha motto wa kifalme. Mfalme mwenyewe ambae ni babu wa mototo alizikia habari hizo na ndipo aliotanguliza barua yake katika skuli husika na kuandika hivi “motto huyu kweli ni mwana wa kifalme “prince” lakini atakua hivyo akiwa ndani ya kasri a baba yake, nakuagiza rasmi kwamba mshughulikie motto huyu kama wenzake anapokua skuli”. Watoto na wajukuu wa wafalme wakiadhibiwa wanapofanya makosa hata kama walikuwa wazee wao walikuwa na vyeo na utukufu mkubwa. Wafalme waliishi bila kuwa ya hofu na raia zao. Hawakuwa na majeshi wala mabodigadi kwa kuwa hawakuona umuhimu wake. Sayyid Khalifa bin Haroub kwa mfano alipanda gari lake akiwa hana askari wala bodigadi, alikuwa yeye na dereva wake pamoja na bawabu wake tu. Wafalme waliacha maendeleo makubwa ya kijamii na kiuchumi ambayo yalikuja yakafisidiwa baadae.

Wakati wa uhai wake, Sheikh Thabit Kombo aliwahi kutamka kwamba “laiti kama Seyyid Khalifa bin Haroub angepata umri mrefu zaidi hadi leo hakuna ambae angeyatamani mapinduzi”. Ukweli ni kinyume na inavyodaiwa kwamba waarabu waliwafanyia maovu makubwa na matupu raia wa Zanzibar bali pamoja na mapungufu waliokuwa nayo walijitahidi kuwatendea raia zao wema wakiongozwa na misingi na itikadi ya dini yao ya kiislamu.

“Wakati wa Seyyid Khalifa bin Haroub mie nilikuwepo na nakumbuka sana. Nakumbuka kila Ijumaa kila anaetoka msikitini au kila atakae akenda kwake kwa kutafuta rizki. Mimi niliwahi kufuatana na wenzangu tukenda kwake, mimi nikapewa pesa nne. Na halafu alikuwa akipita mitaani watu wakikusanyika akiwagaia chochote” (Mahojiano na Bwana Mbaruk Saleh, miaka 72).

Hata hivyo utawala wa kifalme wa Zanzibar ulikuwa na makosa kasoro zake. Baadhi ya wafalme walitenda makosa nyakati za utawala wao. Wako waliowazingatia waarabu kama ni raia bora zaidi na hawakuwazingatia waswahili na waafrika kama ni watu waliokuwa na thamani sawa na wao. Wao walijipachika hadhi na kujiona kundi la watu wa daraja ya kwanza kuliko watu wa makabila mengine. Bwana Mbarouk Saleh anasema tena:

“Upungufu wa chakula unapotokea palikuwa pakitolewa reshen kali. Ikiwa mwarabu atapata kilo mbili za mchele, mwafrika anapata kilo moja. Ikiwa wao waarabu watapata kilo tatu nyie waswahili mutapata kilo mbili alimradi hamwendi sambamba ijapokuwa hakuna afae na njaa. Waswahili lazima watakuwa chini kidogo kuliko wao”.

Hata hivyo ifahamike utaratibu wa kuwagawa wazanzibari kwa madaraja ya ubora ulisimikwa na Muengereza katika jitihada zake za kuona anaendelea kuvumiliwa utawala wake na Sultani. Staili ya kuwaweka mbele na kuwapendelea waarabu katika kila jambo kama umiliki wa ardhi, mgao wa chakula wakati wa njaa, utowaji wa huduma za elimu, na utowaji wa huduma za mahospitali. Mambo yote haya aliyatungia sheria, chambilecho wazee wakisema “kupasisha sheria” katika serikali yake ya kikoloni ambapo mwarabu (mfalme) hakuwa na mamlaka yoyote. Baadae tutakuja kuona kuwa yeye Muengereza ndie aliyekuja kuwajaza hamasa na chuki watu weusi na kuwambia eti waarabu waliwabagua na waliwafanya watumwa.

Share: