Habari

Kuna baya zaidi katika muungano kuliko kero

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Uzini, Mohamed Raza (CCM) akimuelezea jambo Rais wa Zanzibar na Mwenyekti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein wakati wakiwa kwenye sherehe za ufunguzi wa moja ya matukio katika jimbo hilo.

Mohamed Raza kwa nyakati tofauti awapo kwenye Vikao vya Baraza la Wawakilishi amekuwa mkosowaji mkubwa wa Muungono wa Tanzania dhidi ya Zanzibar: Picha kutoka Mzalendo.net

Na Rahid Abdallah – Gazeti la Mwananchi
Jumapili, Mai 5, 2019

Wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano yameandikwa mambo mengi. Yametajwa mazuri na kero kadhaa. Leo nitaangazia jambo baya zaidi lililopo kuliko hizo kero chache zilizosalia.

Moja ya kero za Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ambayo inaendeleza kutajwa ni ile inayohusu ushiriki wa Zanzibar katika masuala ya kimataifa.

Ya pili, ni kutoka kwa Naibu Waziri, ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Sima aliyoitoa bungeni Aprili 16 mwaka huu wakati akijibu swali la Mbunge wa CCM Zanzibar, Abbas Ali Hassan, juu ya kero za Muungano zilipatiwa ufumbuzi katika awamu hii.

Jibu lilikuwa ni kero mbili; moja ni utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi. Pili, kutotoza kodi ya VAT kwa umeme unaouzwa na Tanesco kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Pamoja na majibu hayo zimeshafanyika juhudi za kuhakikisha Muungano unakuwa wa usawa kwa pande zote, lakini hazijawahi kufanikiwa kuzima malalamiko ya Wazanzibari juu ya Muungano. Kumekuwa na harakati nyingi kutoka Zanzibar, kuhakikisha mabadiliko makubwa yanapatikana.

Nitakupa mifano miwili kama sehemu ya harakati hizo: Oktoba 25, 2018, Kamati ya Hoja ya Kura ya Maoni Zanzibar iliandika barua ikiitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuitisha kura ya maoni kuhusu Muungano.

Sehemu ya barua hiyo inasema: “Katika taarifa tumeeleza kwa ufupi jinsi Zanzibar ilivyokuwa ndani ya siku 137 baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza Desemba 10, 1963.”

“Zanzibar ilipotea tena ilipotumbukizwa ndani ya Muungano na Tanganyika bila ya mashauriano yoyote na watu wa Zanzibar na wawakilishi wao”.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kamati hiyo, nakala ya barua ilipelekwa pia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, mkuu wa mabalozi nchini Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Pia, taarifa juu ya uwepo wa barua hiyo zimefikishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Pili, ni ile taarifa ya uwepo wa kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliyofunguliwa na Wazanzibari 40,000 wakihoji juu ya uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kesi bado ipo.

Haya yote yanaashiria uwepo wa harakati kubwa Zanzibar kuhakikisha kile wanachoamini ni haki yao kuhusu Muungano kinapatikana ama kupitia mahakama au kura ya maoni.

Hapo sijazungumzia Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na harakati za kutaka mabadiliko juu ya Muungano.

Kwa nyakati tofauti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, zimekuwa katika jitihada za kupoza malalamiko kuhusu Muungano.

Swali la kujiuliza, kwanini bado malalamiko hayapungui na badala yake ndio kwanza yanaongezeka, hasa kutoka Zanzibar?

Nataka niwe mkweli hapa; ni matarajio ya ajabu, kufikiria kwamba Wazanzibari watanyamaza kuulalamikia Muungano siku tu zikifutwa kero zote. Kama hujanielewa, twende wote utaelewa tu.

Kuna wanasiasa na wasomi wakubwa ambao hudhani kufutwa kwa kero za muungano ndiyo suluhisho la kila kitu. Kuamini hivyo ni kujidanganya.

Tatizo kubwa na baya kuhusu huu muungano ni hali mbaya za kiuchumi (umasikini uliokithiri) hata baada ya nusu karne ya uwepo wake.

Hali mbaya za kimaisha kwa raia, hufanya wajiulize Muungano una faida gani? Ukichunguza wengi wao hawahoji tena kuhusu kero, ila wanahoji uhalali wake, kura ya maoni na uhuru wa Zanzibar.

Na binadamu akiwa haoni faida ya jambo fulani, hata ulipambepambe bado hutobadilisha maamuzi ya moyo wake.

Ubovu wa maisha unaotokana na mikakati isiyokidhi ya watawala, ndio jambo baya mno kuliko hata hizo kero. Watu wameishi katika umasikini kwa miaka mingi, wakiwa ndani ya chombo kiitwacho Muungano.

Waafrika wengi wana njaa na mafukara. Kelele za maandamano ya raia hutokana na kuchoshwa na ugumu wa maisha, unaotokana na kushindwa kwa viongozi kuyabadilisha maisha yao.

Tengeneza picha ya Zanzibar iliyoneemeka. Wananchi wako bize wakifurahia maisha yao, mtu hula atakacho kwa wakati atakao.

Umasikini unatokomea, watoto wanasoma vizuri na huduma za kijamii zipo muda wote. Hayo yote yakawa yametokana na uongozi bora wa pande zote huku rais wa Muungano akiwa ndiye kaka mkubwa wa mambo yote.

Naamini malalamiko kuhusu Muungano yasingekuwapo, na hata kama yangezushwa basi si kwa hoja hizi za sasa kutoka Zanzibar, kwamba Zanzibar inanyonywa.

Ikiwa bado Wazanzibari wanaishi katika umasikini uliokithiri. Katu tusifikirie wataacha kuulalamikia Muungano hata kero zote zikiondoshwa. Huo ndio ukweli!

Kuna wakati utawala unakosa haki ya kulaumu raia wake pindi wakianzisha harakati fulani. Hizi harakati hazianzi kwa bahati mbaya, ni matokeo ya kukosekana utawala bora wa kuwanufaisha wananchi kwa kuwakwamua katika tope la umasikini uliokithiri.

Sina maana kero zisiondoshwe, ila wale wanaofikiria kuziondosha itakuwa suluhisho, waache fikra hizo. Ili malalamiko juu ya muungano yapungue, kufuta hizi kero kuende sambamba na maendeleo ya wananchi. Pengine itasaidia!

Tena si maendeleo ya nambari na kwenye karatasi, ila yaonekane na wananchi wajione kweli umasikini umepungua, vinginevyo tutarajie harakati na miamko mingi zaidi ya kuhoji uhalali wa Muungano, kesi mahakamani na kudai kura ya maoni.

Share: