Habari

KZU yawaonya watakaokataa majengo yao kukaguliwa

September 13, 2018

NA HANIFA RAMADHANI

KIKOSI cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU), kimetoa tahadhari kwa wamiliki wa majengo ambao hawatokuwa tayari kutoa ushirikiano katika ukaguzi unaofanywa na kikosi hicho.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa wa sheria wa Zimamoto, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kilimani.

Alisema, ukaguzi wanaofanya katika majengo mbalimbali ni kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 1999 chini ya kifungu cha 7 (1) ambacho kinampa mamlaka Kamishna wa Zimamoto kufanya ukaguzi katika majengo.

Alisema, ukaguzi huo ulianza Agosti 12 mwaka huu na wamefanikiwa kukagua hoteli 11, mikahawa mitatu, maduka 10, maghala ya kuhifadhia chakula matatu, hosteli moja, duka moja na ofisi ndogo moja kwa upande wa mkoa wa mjini magharibi.

Aidha alisema, lengo la kufanya ukaguzi huo ni kuhakikisha kuna usalama katika majengo hayo ikiwa ni pamoja na kuwashauri wamiliki wa majengo kuweka mtungi wa kuzimia moto.

Hata hivyo, alisema, ukaguzi huo ni wa kawaida ambao upo kisheria na ni moja ya kazi ambazo zinatakiwa kufanywa na kikosi hicho.

Zanzibarleo

Share: