Habari

Lipumba: ‘CUF tutashiriki uchaguzi wa Jang’ombe’

Mwenyekiti wa CUF anaetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, 16/8/18 katika Ukumbi wa Baitul Yamiyn, Bwawani mjini Zanzibar. Picha kutoka mitandao ya kijamii.

Bwawani, Zanzibar
Alhamisi, Agosti 16, 2018

MWENYEKITI wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho kitashiriki katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe, Unguja unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Kadhalika, Lipumba amemtaka Maalim Seif kufuta kesi zilizopo mahakamani kwa sababu hazina mashiko, na kuepuka hasara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Agosti 16, 2018 katika ukumbi Baitul Yamiyn, Bwawani, mjini Zanzibar, Lipumba, alieleza msimamo wa chama hicho wa kushiriki katika uchaguzi mdogo kwa nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Nafasi hiyo imekuwa wazi tangu mwezi wa Mei mwaka huu baaada ya mwakilishi wa jimbo hilo kuvuliwa uanachama wa CCM, kufuatia kuliambia Baraza la Wawakilishi kuwa ushindi wa CCM ulipatikana kutokana na hisani ya Jecha.

Katika hotuba yake, Lipumba alisema kwa kuwa CUF ni sehemu ya vyama vya siasa ambavyo vina haki ya kushiriki uchaguzi huo, hivyo ni wazi kuwa hawataacha kushiriki ili kuwapa fursa wananchi kukichagua chama chao hicho.

Alisema uongozi wa chama chao hivi sasa upo katika michakato ya kumpata mgombea atakaye peperusha bendera ya kuwania uwakilishi kupitia chama chao cha CUF.

“Hatuwezi kuwacha fursa ya kushiriki uchaguzi mdogo kwa kisingizio cha mgongano uliopo baina yetu, sisi lengo letu ni kutumikia wananchi hivyo tunaahidi kuwa tutashiriki uchaguzi bila ya wasi wasi wowote,” alisema Lipumba na kuongeza:

“Kutokushiriki uchaguzi ni sawa na kuwasusia wanachama wetu hivyo kwa upande wetu sisi hatuwezi kuwasusia wanachama hata kidogo, bali nguvu zaidi tutazitoa ili kuhakikisha tunafanya vyema katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo.”

Katika hatua nyingine, Lipumba alimtaka Maalim Seif kufuta kesi zisizo na mashiko walizofungua mahakamani ili kuepukana na hasara ambazo zinaweza kuepukika

Alisema si jambo la busara hata kidogo kwa wakati huu ambao nchi ipo katika kipindi kizuri cha amani na utulivu huku kundi la watu likaibuka na kuanza kufungua kesi za kisiasa ambazo kuwepo kwake ni kupoteza muda kwa kundi lililofungua kesi hizo.

“Nawaomba sana ndugu zangu akina Maalim Seif wafute kesi zao Mahakamani kwani kinyume chake wataendelea kuwanufaisha mawakili tu wala hakutakuwa na jambo jipya juu ya kesi hizo,” alisema Lipumba.

Akizungumzia mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika hivi karibu amesema kuwa viongozi wapo katika mipango ya kuandaa mkutano huo ambao utakuwa ni fursa pekee kwa wanachama kuwania nafasi za uongozi wanazozitaka.

“Kwa kuwa chama chetu kipo kwa ajili ya kutumikia wananchi ndio maana hivi sasa tumo katika maandalizi ya kufanya mkutano mkuu ambao utatoa viongozi wapya wa kukitumika chama bila ya ubaguzi,” alisema Lipumba.

Mwishoni mwa mwezi wa Mei mwaka huu, NEC ya CCM ilimvua uanachama mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe, Abdalla Diwani kwa madai ya kukiuka maadili na kwenda kinyume na miiko ya chama hicho.

Sababu za kuvuliwa uanachama ilidaiwa kuwa mjumbe huyo aliwaambia CCM ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kuwa wapo hapo kwa hisani ya ‘Jecha’, lakin hawakushinda uchaguzi.

Abdalla Diwani, alisema: “CCM ilifanyiwa ‘favour’ (hisani) na Jecha, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi lakini ukweli CCM haikushinda.”

Alipotakiwa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuomba radhi…aliwauliza: “Kwani Jecha hakufuta uchaguzi?.

Share: