Habari

Lissu amvuruga tena Profesa Kabudi, hadi aache kudanganya

Tundu Lissu: Prof. Kabudi ni bingwa wa kuchapia, hasa kwa watu wasiomuelewa au waliowavivu wa kusoma au wenye uelewa wa juu juu.

Mwanahabari Huru – Jamii Forums
Jumatano, Septemba 12, 2018

Nimeona clip ya Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Pala Kabudi akitoa ‘lecture’ bungeni juu ya masuala mbali mbali ya kisheria na kikatiba.

Clip hiyo imeanzia katikati, kwa hiyo ni vigumu kwangu kufahamu hoja ya msingi iliyomfanya azungumze alichozungumza.

Hata hivyo, nimevutiwa na alichokisema juu ya mamlaka ya Rais ya kutunga sheria. Ndicho ninachotaka kukizungumzia kwa ufupi hapa.

Kabla sijafanya hivyo niseme tu kwamba Prof. Kabudi ni bingwa wa kuchapia, hasa kwa watu wasiomuelewa au walio wavivu wa kusoma au wenye uelewa wa juu juu, hasa wa masuala ya kikatiba na kisheria. Naomba hoja yake juu ya mamlaka ya Rais ya kutunga sheria kama mfano.

Prof. Kabudi amedai Rais ana mamlaka ya kutunga sheria kwa kutumia decrees, instruments na proclamations. Hajafafanua matumizi ya hizo decrees, instruments na proclamations.

Kwa kumsikiliza tu, mtu asiyejua mambo haya anaweza kufikiria, kimakosa, kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka ya kutunga sheria juu ya jambo lolote, wakati wowote kwa kutumia hizo njia tatu.

Ukweli ni kwamba mamlaka ya Rais ya kutumia instruments na proclamations yanahusu mambo mahsusi ambayo yametajwa kwenye Katiba. Instrument (waraka) au proclamation (tangazo) ni njia au namna tu anayotumia kutekeleza mamlaka yake.

Katiba yenyewe ndio inayofafanua mamlaka gani yatekelezwe kwa kutumia instrument na yapi yatekelezwe kwa kutumia proclamation.

Kwa mfano, Rais ana mamlaka ya kutangaza hali ya hatari kwa mujibu wa Katiba. Sasa Rais anatekeleza mamlaka hayo kwa kupitia tangazo (proclamation) ya hali ya hatari.

Tangazo hilo sio source ya mamlaka yenyewe, source ni Katiba na Sheria ya Ukasimishaji wa Mamlaka ya Uwaziri. Proclamation ni ushahidi tu kwamba Rais ametumia mamlaka yake ya kikatiba.

Mfano mwingine. Rais ana mamlaka kikatiba ya kuunda au kuvunja ofisi za umma, i.e. Wizara, n.k. Katiba yenyewe imeelekeza kwamba Rais atatumia instrument (waraka) pale anapounda Wizara, kufafanua majukumu yake, etc.

Maana ya kusema hivi ni kwamba kama Katiba haijasema kwamba Rais atatumia utaratibu fulani katika kutekeleza jukumu lake fulani kikatiba, yeye hawezi kujiamulia kutumia utaratibu wa instrument au proclamation katika kulitekeleza jukumu hilo.

Kwa mfano, Rais hateui Majaji au Mawaziri au Wakuu wa Wilaya au Mkoa au Makatibu Wakuu wa Wizara au watendaji wa taasisi mbali mbali za umma kwa kutumia instruments au proclamations.

Kwa upande mwingine, Rais hana mamlaka kabisa, kwa Katiba ya sasa, ya kutunga sheria kwa kutumia decrees. Decrees (amri) ni Sheria zinazotungwa pale ambapo hakuna Bunge la kawaida kwa sababu yoyote ile.

Mfano mzuri ni tawala za kijeshi au za kimapinduzi kama ilivyokuwa Zanzibar kati ya miaka ya ’64 na ’79.

Sasa ilikuwaje Mwalimu Nyerere akatunga Sheria mbili kwa kutumia decree mwaka ’64??? Jibu ni Mapinduzi ya Zanzibar ya Jan. ’64, na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Aprili ya mwaka huo huo.

Kwa sababu ya Mapinduzi, Bunge la kawaida la Zanzibar lilivunjwa na badala yake Baraza la Mapinduzi likajipa madaraka ya kutunga sheria kwa kutumia decrees.

Na mara baada ya Muungano kuzaliwa, hakukuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kutunga sheria zinazohusu masuala ya Muungano.

Hivyo Mwalimu Nyerere alipewa mamlaka hayo kwenye Hati ya Makubaliano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ili kumwezesha kutunga sheria zinazohusu masuala ya Muungano wakati wa kipindi cha mpito mara tu baada ya Muungano.

Mamlaka hayo yalifikia mwisho wake mwaka ’65 ilipotungwa Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu wakati huo Rais hana tena mamlaka ya kutunga sheria kwa amri (decrees).

Mwisho, ni muhimu kuelewa kwamba mamlaka ya Rais ya kutumia instruments na proclamations yanahusu tu mambo yaliyotajwa kwenye Katiba. Nje ya mambo hayo, Rais hana mamlaka anayoyazungumzia Profesa Kabudi.

Share: