Habari

Lissu anavyomuumbua Profesa Kabudi

Lissu: Prof. Kabudi usiwadanganye watu, Waliopiga risasi marais wa Marekani walipatikana

Imeandikwa na Tundu Lissu:

Nimesikia alichokisema kaka yangu Profesa Palamagamba Kabudi juu ya jaribio la mauaji dhidi yangu la tarehe 7 September iliyopita.

Sijashangazwa na alichokisema Prof. Kabudi. Ninamfahamu vyema baada ya kumtazama kwa karibu miongo mitatu.

Kabudi ni profesa wa sheria (bahati mbaya yangu sikuwahi kuwa mwanafunzi wake!!!) na msomi na mwerevu sana. Usipomfahamu vyema, anaweza kukulisha ‘matango pori’ kwa usomi wake, huku ukidhani amesema ukweli mtupu.

Naomba kuthibitisha ‘matango pori’ aliyowalisha wasikilizaji wake juzi kuhusu marais wa Marekani waliouawa na wauaji wao kutokujulikana mpaka leo. Yeye alisema wako wawili. Ni ‘matango pori.’

Rais wa kwanza kuuawa Marekani alikuwa Abraham Lincoln, mnamo tarehe 14 Aprili, 1865. Muuaji wake John Wilkes Booth alitoroka lakini aliuawa baada ya kutafutwa kwa siku 12.

Washirika wake watatu walikamatwa, kushtakiwa kwa uhaini na walihukumiwa adhabu ya kifo na kunyongwa.

Rais wa pili kuuawa Marekani alikuwa James Abram Garfield, aliyepigwa risasi na Charles Guiteau tarehe 2 Julai, 1881. Alifariki dunia tarehe 19 September, 1881.

Muuaji wake alikamatwa pale pale, alishtakiwa na kuhukumiwa kifo na alinyongwa mwaka mmoja baadae.

William McKinley alikuwa Rais wa tatu wa Marekani kuuawa akiwa madarakani. Alipigwa risasi na Leon Czolgosz tarehe 6 September, 1901, na kufariki tarehe 14 September, 1901. Czolgosz alihukumiwa kifo na aliuliwa kwa kiti cha umeme.

Rais John Fitzgerald Kennedy, Rais wa 35 wa Marekani, aliuawa na Lee Harvey Oswald tarehe 23 November, 1963. Alikuwa Rais wa nne wa Marekani kuuawa akiwa ofisini. Oswald alikamatwa na kuuawa na Jack Ruby, askari wa FBI, siku hiyo hiyo.

Rais Ronald Reagan alipigwa risasi na kujeruhiwa na John Hinckley Jr. tarehe 30 Machi, 1981. Alikuwa Rais wa tano wa Marekani kushambuliwa kwa risasi kwa lengo la kumuua.

Lakini Reagan hakufa. Na wala muuaji mtarajiwa wake Hinckley Jr hakupatikana na hatia yoyote kwa sababu ya ugonjwa wa akili. Aliwekwa hospitali ya wagonjwa wa akili hadi mwaka 2016 alipoachiliwa huru.

Taarifa zote hizi ziko mitandaoni na Prof. Kabudi angeweza ku-google na kupata cha kusema ukweli. But he’s an intellectual bully who, like all bullies, did not expect to be confronted with the truth.

Anasimama hadharani Marekani, na kusema uongo mbele ya watu wanaoishi Marekani, kuhusu mambo ya kihistoria ya Marekani, huku akitegemea hakuna mwana-diaspora anayeishi Marekani atakayembishia, kwa sababu yeye ni profesa mbobezi wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam!!!

Hawa ndio wasaka tonge waliopewa uwaziri na Magufuli!!!

Share: