Habari

Lissu apelekwa Nairobi kwa matibabu

Habari za hivi punde tulizozipata ni kwamba ndege ya kumpeleka Lissu Nairobi, Kenya kwa matibabu ya uhakika tayari imewasili uwanja wa ndege wa Dodoma, usiku huu.

By Waandishi wa Mwananchi
Thursday, September 7, 2017

Rais John Magufuli, amesema amepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Katika akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli amesema anamuombea Lissu kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka.

“Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hilo la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria,” amesema Magufuli.

Lissu amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojuilikana Alhamisi tarehe 07/09/17 mchana akiwa kwenye gari mara baada ya kuwasili nyumbani kwake ‘Area D’, Dododma. Anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Katika hatua nyingine, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimepokea kwa mshtuko taarifa za kushambuliwa Lissu.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika taarifa yake amesema chama hicho kinalaani tukio la kushambuliwa mbunge huyo ambalo amelielezea ‘halina utu.’

CCM imelitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta, kufanya uchunguzi wa tukio na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote waliohusika na kitendo hicho, alichokielezea kuwa ni cha kidhalimu.

“Uongozi wa CCM unamwombea Lissu kupona haraka na afya nje ili aendelee na majukumu yake ya kibunge,” imesema taarifa hiyo.

Wakati huo huo, CHADEMA Mkoani Singida, imelaani tukio hilo ikisema linatishia ustawi wa demokrasia ndani ya nchi.

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Mathew Sumbe amesema kwa sasa hawana wa kumtupia lawama isipokuwa wanaendelea kumwombea Lissu kwa Mwenyezi Mungu, aweze kupona na mambo mengine yatafuata.

Amesema Lissu ni kiongozi mwenye nyadhifa mbalimbali na amekuwa mstari wa mbele kutetea Watanzania, wakiwemo wanyonge, hivyo kuna umuhimu wa kumwombea aweze kupona na kurejea kwenye majukumu yake.

“Tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Dodoma ili kupata maendeleo ya afya ya kiongozi wetu. Baada ya afya yake kurejea katika hali ya kawaida hapo ndipo tutapata nafasi ya kulizungumzia tukio hili kwa upana,” amesema Sumbe.

Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Singida Mjini, Yahaya Ramadhani amesema tukio hilo  linatishia amani iliyojengeka kwa miaka mingi.

“Uzoefu unaonyesha siku zote kwamba, watu wema na watetezi huwa hawadumu. Hatuna jambo lingine la kuzungumzia kwa sasa zaidi ni kumwombea aweze kupona haraka,” amesema Ramadhani.

Wakati huo huo, baada ya taarifa kuenea ndani na nje ya Tanzania za kujeruhiwa kwa risasa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu Chama cha wanasheria nchini Kenya (LSK), kimelaani Lissu kupigwa risasi.

Wanasheria hao wamesema shambulio dhidi ya Tundu Lissu limewagusa watu wote Afrika na dunia kwa jumla.

Rais wa LSK, Isaac Okero amesema tukio hilo limewashtua  wanasheria wote wa Kenya: “Tunalaani vikali tukio la kupigwa risasi Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu.”

“Tumepata taarifa kwamba Lissu amepigwa risasi akiwa kwenye gari lake mjini Dodoma, kwa kweli imetushtua sana na inahuzunisha,” Okero amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

“Kwa pamoja tunalaani tukio hilo kwa kuwa hili limewagusa wanasheria wote wa Afrika na hata dunia kwa jumla. Tunasikitika kwa uvunjifu wa sheria uliofanyika,’’ amesema Rais wa LSK.

Amesema Lissu anafahamika kwa kutetea haki za binadamu, hivyo wanasheria wote wapo pamoja naye katika kipindi hiki kigumu kwake na Mwenyezi Mungu atamsaidia atarudi katika hali yake ya kawaida.

Habari za hivi punde tulizozipata zinaeleza kuwa ndege ya kumpeleka Lissu Nairobi, Kenya kwa matibabu imewasili usiku huu kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma.

Taarifa kutoka katika Uongozi wa Hospitali ya Dodoma zinasema kuwa viongozi wa CHADEMA wanafanya maandalizi ya mwisho ya kumpeleka Lissu uwanja wa ndege wa Dodoma tayari kwa safari ya Nairobi, Kenya.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel wameingia katika chumba cha upasuaji kukamilisha taratibu za kumsafirisha.

Aidha, wanachama wa CHADEMA wakiongozwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini wamefanya sala fupi kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, ili kumwezesha Lissu, kusafiri salama.

Awali, Katibu wa Wabunge wa CHADEMA, David Silinde alisema wabunge wa chama hicho wameamua kuchangisha fedha kwa ajili ya kumsafirisha Lissu kwenda Nairobi kwa matibabu ya uhakika.

Share: