Habari

Maalim Seif aeleza zuio la mikutano linavyowapa wapinzani changamoto

By Muhammed Khamis – Mwananchi
Jumatano, Disemba 5, 2018

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza kuwapo changamoto inayotokana na zuio la mikutano ya kisiasa nchini, hasa katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano.

Akizungumza hivi karibuni mjini London, kwenye mahojino na BBC ya Idhaa ya Kiswahi katika kipindi cha Dira ya Dunia, Maalim Seif alisema vyama vya siasa vinahitaji kukua kwa lengo la kuongeza wanachama.

Alisema kwa kawaida vyama vya siasa huhitaji kukua na kumea kila siku kupitia njia ya kufanya mikutano ili kuongeza wanachama wapya, jambo ambalo hivi sasa halifanyiki kutokana na marufuku iliowekwa na Rais.

“Yanayotokea sasa hayajawahi kutokea…sisi Watanzania hatujawahi kuyaona, tunayaona katika awamu hii ya tano ya uongozi,” alisema maalim Seif.

Alisema mikutano ya vyama vya siasa ndio njia pekee ya wao (wapinzani) kuhubiri sera za vyama vyao hatimaye wananchi kuona nini chama kinafanya lakini pia kuikosoa serikali pale inapokesea.

Maalim Seif alisema vyama vya siasa vina nafasi ya uongozi kwenye maeneo mbalimbali ambayo wamepewa jukumu na wananchi, hivyo wanalazimika kupata mrejesho wa ahadi ambazo wametoa kwa wananchi sambamba na maendeleo ya maeneo yao.

“Hatua hii ni sawa na kuwanyima viongozi wa upinzani kuwaeleza wananchi yale waliyofikia na kukosoa pale inapobidi, lakini yote hayo hayafanyiki.”

“Unalazimika kufuata mlolongo mkubwa kabla ya kuruhusiwa kufanya mkutano mdogo wa jimbo tu,” alisema Maalim Seif.

Alisema utaratibu huu unaoendelea sasa, wa kuzuiwa kwa mikutano ya siasa, haujawahi kutokea tangu kuasisiwa kwa vyama vya siasa.

“Kwanza suala zima la kwamba vyama vya upinzani vinazuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa. Vyama vya upinzani vinataka wafuasi na bila ya kwenda ukazungumza na wananchi ukaelezea sera zako…wananchi watakufahamuje?” alihoji Maalim Seif na kuongeza.

“Pili, ni kwamba vyama vya upinzani tunakandamizwa sana. Kwetu katika CUF umepandikizwa mgogoro huu uliopo wa Profesa Lipumba.”

Maalim Seif alisema vyama vya upinzani vimekuwa vikikandamizwa katika njia tofauti kwa lengo la kuhakikisha haviendelei kukua badala yake vimeendelea kudumaa na kurudi chini kiutendaji.

Alitoa mfano mgogoro wa miaka miwili sasa kwenye chama chake na kusema mgogoro huo umetengezwa makusudi na msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi kumrejesha Profesa Ibrahim Lipumba kwenye nafasi aliojiuzulu ya uenyekiti wa chama chao, madai ambayo Jaji Mutungi amekuwa akiyakanusha mara akwa mara.

Kesi zadhoofisha chama

Alisema mgogoro huo umesababisha kufunguliwa kwa kesi mbalaimbali umerudisha nyuma kwa kiasi kikubwa nguvu za upinzani kwenye chama chake lakini pia umoja wa vyama vya siasa ulioasisi katika Bunge la Katiba (Ukawa).

Alisema mchakato wa kujiuzulu kwa Lipumba ulitengezwa kwa dhana kuwa waliotengeza mkakati ule waliamini kwamba kutoka kwake kungeleta madhara makubwa ikiwemo kutoka na wafuasi wengine wa vyama vya upinzani.

Alisema CUF kama chama chenye wabunge na madiwani, kilitarajia kupatiwa ruzuku ili waendeleze harakati za ujenzi wa chama lakini ruzuku hiyo ilizuiliwa kwa madai ya kuwepo kwa mgogoro kwenye chama chao.

Hivi karibuni Jaji Mutungi alilieleza gazeti hili kuwa anatendelea kutoa ruzuku kwa upande wa Lipumba “Kwa sababu chama kilimwandikia kuelekeza hivyo.”

Maalim Seif alisema kilichoweza kunusuru ruzuku hiyo ya chama ni baada ya wao kwenda kufungua shauri na mahakama kuamuru kuzuia ruzuku hiyo, lakini vinginevyo ingeendelea kutoka hadi sasa.

Alisema licha ya uwepo wa changamoto hizo, wanachofikiria kwa sasa ni kuunganisha nguvu zaidi ya vyama vya siasa ambavyo anaamini vitakua na tija kubwa kwa Watanzania katika kuelekea uchaguzi wa 2020.

Kuhusu muswada wa marekebisho ya vyama vya siasa mwaka 2018, alisema msajili ndiyo atakayeweza kuamua kiongozi gani anapaswa kuendesha chama na kiongozi gani hafai kwa mujibu wa muswada ambao umewasilishwa bungeni.

Pia, alisema muswada huo umeweka mazingira magumu kwa vyama vya siasa iwapo vinataka kuungana lazima vipate idhini ya waziri husika, jambo ambalo alidai si rahisi kukubalika.

“Tunajua kwamba waziri anatoka katika chama tawala, CCM, na inajulikana wazi kuwa umoja ni nguvu na watakapoungana ni wazi itakuwa changamoto, sidhani kama watakubali,” alifafanua Maalim Seif.

Akifafanua zaidi alisema iwapo muswada huo utapita ni kwamba mtu aliyeacha chama chake na kwenda chama kingine hataruhusika kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwenye chama kipya mpaka atakapotimiza mwaka mmoja.

Maalim Seif aliweka wazi na kusema kwamba mazingira hayo yote yanatokana na baadhi ya watawala kuwa na hofu ya uchaguzi wa mwaka 2020, wakidhani baadhi ya viongozi miongoni mwao wanaweza kugombea nafasi kupitia vyama vya upinzani.

Akizungumzia kuhusu hatma yake na mbio za urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alisema muda wakusema hayo bado na utakapofika ataweka wazi kila kitu.

Share:

4 comments

 1. Tengoni 8 Disemba, 2018 at 04:23 Jibu

  Sharti la sheria mpya kwa aliehamia chama kipya kusubiri mwaka mzima kabla kugombea uwakilishi, ubunge, inelengwa kwa Maalim Seif nwenyewe pamoja na makada wa CUF ambao ni wabunge. Mpango mzima ni CUF kufutwa mwakani mwishoni kwa kisingizio cha mgogoro, hatua ambayo inahofiwa Sefu na makada wa CUF watakimbilia chama kingine ili waweze kugombea urais, ubunge na uwakilishi, lakini kwa sheria mpya watakuwa wamechelewa na sheria mpya inasema maamuzi ya msajili hayahojiwi na mahakama yeyote. CUF lazima wawe na fikra pana, vyenginevyo watakuwa mateka kila mara, kesi wanazotegemea kuwavusha zitapigwa kalenda na kuhitimishwa na msajili na sheria mpya. Mwaka 2019, lazima CUF wawe wameshaamua la kufanya.

 2. abuu7 8 Disemba, 2018 at 06:55 Jibu

  Kinachosubiriwa ni hasira za wa zanzibar. Haki haiko tena. Isipokuwa kikubwa tunaona vijana wanaona nyerere kaka tena kombe MAGUFULI.

  Tumepoteza chnsi nzuri. Pale uma ulivovamiya bwawani hotel kipindi kile. . Yaani hata jesshi la mkoloni tanganyika lingekuwa to let

 3. chatumpevu chatumpevu 8 Disemba, 2018 at 15:44 Jibu

  Ndugu zangu Tengoni na Abu 7

  Siasa za afrika ni siasa za maji taka zinazobuniwa na labda niseme siasa hizi ziko reactive. huwa, kwa kawaida zinasubiri kutokee hali fulani ndo utasikia mara sheria hii ama ile inatungwa au inafanyiwa mapitio ili kuumiza upinzani . Ni siasa za kitoto zisizo na tija. Lakn kwa CUF hususan CUF ya maalim inafaa kuwa makini kwa sababu maudhui ya kufanyiwa marekebisho sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ni kuibana CUF na chadema ili kwa namna yoyote wasiweze kupumua.

  Kwa maalim seif, yafaa aje na plan B haraka , kwa kuwa vizingiti vingi vya kisheria vimewekwa ili kumdhibiti asipumue kisiasa. kila mtego umewekwa na wanaotunga na kufanyia marekebsiho sheria hizi ni wasomi wa kibongo wanaoneemeka kwa kupewa vyeo na mkuu wa kaya.

  Jaji mutungi anasubiri saa ya mwsho ya CUF kupumulia mashine kule ICU ya magogoni. Nakubali mawazo yenu nyote kuwa mutungi anasubiri eleventh hour ya kukifuta chama cha CUF baada ya kumaliza kazi ya kumtumilia hayawani lipumba. Kwa haraka itabidi CUF waamue njia nyengine ya kufanya , na wakichelewa itakuwa too late maana mwaka 2019 ndo huo hapo. Linaloonekana dhahiri mapitio haya ya sheria ni kuumiza ukawa huku wakijua kuwa ukawa bado ni mwiba kwa CCM.

  Kesi zilioko mahakmani zinaendelea kupangiwa kalenda kwa makusudi na mtakumbuka kuwa yule jaji lyansobera aliyekuwa akiharakisha uendeshaji wa kesi za CUF amehamishiwa mtwara , makusudi ili apunguze speed ya kuendesha kesi.

  Cha kuomba ni kuwa maalim aamke mapema kwa sababu hayawani lipumba hana cha kupoteza kwa kuwa ameshashika mpunga wake billions of money. He has nothing to lose.

 4. mzeekondo 9 Disemba, 2018 at 00:44 Jibu

  Mahakama za Tanganyika zinatoa maamuzi ya kuibeba ccm,kama wanavyofanya polisi,tume ya uchaguzi,bunge na vyombo vyote vya dola,hii nchi kwa sasa inatawaliwa kwa amri za kishenzi sio sheria huu ndio ukweli.

  Tanzania kama taifa tumerudishwa nyuma miaka 50 mingine na hii awamu ya tano ya Magufuli,wengi wataogopa kusema kweli hadharani lakini sio kama hawajui kuwa huyu sio rais bali ni mkosi kwa taifa hili.

  Tanzania au Tanganyika tulikubali vyama vya siasa kuwa vingi kwa sababu tulikuwa hatutaki chama kimoja kiwe ndio muamuzi na msimamizi wa serekali huyo huyo bila mpinzani anaeweza kuwasemea wananchi pale wanapo kwenda nje ya sheria au makubaliano kama taifa,sasa huku kutumia nguvu zote kuuwa watu,kuwasweka mgerezani na wengine kuwashambulia kwa risasi hii ndio awamu ya tano inyopenda masikini?

  Kama hii ndio awamu ya wapenda masikini basi mimi naona bora nionjeshwe awamu inyopenda matajiri,labda hiyo watu watanusurika na haya mauti/misiba ya kila siku,ccm ni cham changu lakini kwa sasa naelewa kuwa hiki chama hakina maana hata kidogo kwa sababu hatuna kiongozi wala maamuzi,sisi tunasikiliza radio tu leo bwna mkubwa katoa amri gani? nani kamtukana?nani kamtumbua au kamfukuza kazi kama mbwa? kazai yake kutisha watu ovyo,ameugeuza urais kama Uungu mtu kuwa kuwa yeye rais basi iwe ndio balaa kwa nchi nzima.

  Najiuliza sana hiki chama cha mapinduzi ndio kimemkabidhi mtu huyu nchi ili aje kutufundisha kauli za kifedhuli? haya ndio matatizo ya kuwa na nchi ambazo haziongozwi na mfumo/system,kila rais atakaekuja kuongoza nchi hii, atakuwa anakuja na mdomo/kichwa chake sio mfumo, sasa kwa bahati nzuri safari hii tumepata mfano,jeee huko tunako elekea ikiwa hatukuweka KATIBA mpya inayoeleweka, basi tutaongozwa na wenda wazimu wengi.

  Ukiona kiongozi hataki katiba mpya, ujue katiba mbovu inamfaa kunyanyasia watu na kulifilisi taifa, kwa sababu katiba anayoin’gan’gania yeye na wezi wenziwe waliomtangulia, wote wanalindwa humo, duniani kote isipokuwa baadhi tu ya nchi za kiafrika, zinazoongozwa na viongozi wanaohubiri amani au demokrasia za midomoni tu, lakini wanatawala kwa mabavu na kuwatia watu hofu, ukizisoma katiba za nchi za nchi hizo utaona wote wamejiwekea sheria za kuwa RAIS HAWEZI KUSHITAKIWA ABADAN, HATA AKIUWA AU AIBE FEDHA ZA NCHI NZIMA, sasa utawezaje kuwa na haki katika nchi ambayo kila mtu yuko chini ya sheria, isipokuwa RAIS TU, huu ni uhayawani.

  Masikini Taifa langu.

Leave a reply