Habari

Maalim Seif afungua kongamano la pili la kitaifa la maridhiano

 

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Hassan Nassor Moyo (kushoto) na Mjumbe wa kamati hiyo Ismail Jussa Ladhu, wakibadilishana mawazo kabla ya ufunguzi wa kongamano la maridhiano lililofanyika hoteli ya bwawani
Na Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema dhamira ya msingi ya ukombozi wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya Januari 12, 1964, ni Zanzibar kuweza kujitawala yenyewe na kuwa na mamlaka kamili.
Maalim Seif ameeleza hayo katika ukumbi wa salama hoteli ya Bwawani, wakati akifungua kongamano la pili la kitaifa linalohusu Maridhiano ya Wazanzibari.
Amesema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliipunguzia Zanzibar mamlaka yake.
Amesema wakati Wazanzibari wanapodai kuwa na mamlaka kamili wanatetea haki na maslahi ya nchi yao, na kwamba hakuna sababu ya kubezwa wala kupuuzwa.
Amefahamisha kuwa akiwa ni kiongozi wa Zanzibar, atasimamia na kutetea mawazo ya wazanzibari waliowengi katika kupata haki zao za msingi ndani na nje ya Zanzibar.
Akifafanua zaidi kuhusu msimamo wake amesema hiyo haina maana kuwa Wazanzibari hawataki Muungano, bali wanataka kuwepo kwa Tanzanyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili, halafu kuwepo na muungano wa mkataba, ili kila nchi iweze kuendesha mambo yake kwa uhuru.
“Kuwa na mamlaka kamili sio kwa maslahi ya watu wachache bali kwa watu wote, ni kama mvua, yaani inaponyesha mimea yote inanawirika”, alifafanua Maalim Seif na kuongeza,
“Tunataka kurejesha heshima ya nchi yetu, tuwe na sera na Wizara yetu ya mambo ya nje, bendera yetu ipepee nchi za kigeni, Umoja wa Mataifa na Jumuiya nyengine za Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Amewataka wanakongamano hao kuwaongoza wajumbe wa mabaraza ya katiba katika kutetea maoni na maslahi ya Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya maridhiano amesema yamerejesha umoja wa wazanzibari na kuondosha uhasama na chuki miongoni kwa wananchi.
Ameipongeza kamati ya maridhiano chini ya Mwenyekiti wake Mzee Hassan Nassor Moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuyaendeleza maridhiano hayo na umoja wa wazanzibari.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Mzee Hassan Nassor Moyo amesema maridhiano hayo yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar dkt. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitna na chuki zilizodumu kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi.
Amesema kamati yake inaisubiri kwa hamu kubwa rasimu ya Katiba mpya itakayotolewa, ili waweze kuichambua kuona kama imezingatia maoni ya wananchi na maslahi ya Zanzibar.
Akiwasilisha mapendekezo ya kamati hiyo Mzee Moyo amesema kila nchi katika Muungano inapaswa kuwa na uraia wake, sera yake ya mambo ya nje na Muungano uwe na JINA la “Muungano wa Jamhuri za Tanzania” au “United Republics of Tanzania”.
Zanzinews
Share: