Habari

Maalim Seif akiwa ziarani Pemba

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad akiwa juu ya jengo la ghorofa, tawi jipya la CUF Makoongwe, Wilaya ya Mkoani Pemba.

Februari 22, 2017

CHAMA cha Wananchi (CUF) na vyama vingine vya upinzani kama CHADEMA na NCCR- mageuzi, havina kawaida ama utaratibu wa kufanya sherehe za kuadhimisha kuundwa kwa vyama hivyo. Chama cha Mapinduzi (CCM), pekee ndiyo kina utaratibu huo. Ni chama dola kina fedha za kufuja na kuharibu.

Chama cha Wananchi (CUF) ambacho, baadaye mwaka huu kinatimiza miaka 25 tangu kilipoanzishwa mwaka 1992. Sijui kwa kufikisha miaka 25 watafanya sherehe au la. Lakini, si dhani kwa sababu chama chenyewe kwa sasa kimo ndani ya matatizo.

CUF baada ya kupata usajili wa muda kiliitisha mkutano wa hadhara wa kwanza kwenye Uwanja wa Malindi, Unguja ambao ulitumika kuwakabidhi baadhi ya viongozi wake wakuu na waanzilishi, kadi za uwanachama.

Mkutano huo wa hadhara wa CUF uliyofanyika siku chache baada ya chama hicho kupata usajili wa muda haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kuweza kuamini kuwa CUF ni chama kipya cha siasa na bila kuwa na wanachama kama ilivyokuwa kwa CCM.

Uwanja wa Malindi, ulifufurika umati wa Wazanzibari kutoka kila pembe ya Unguja. Kutokea Msikiti Mabuluu, njia ilifungwa, kutokea Darajani Marikiti, njia ilifungwa na eneo lote la barabara ya Darajani kuelekea Kituo cha Polisi cha Malindi, mlijaa umati wa watu. Pakutema mate ilikuwa shida.

Sijasahau, nakumbuka Bumbwini, zilitoka gari 16 (malori) na nyingine zilikuwa zina-kwenda na kurudi kubeba watu. Nungwi, Shangani Mkokotoni, Mkwajuni na vitongoji vyake, zilitoka gari 58 na zaidi.

Tumbatu na Mkokotoni yake, na mbali ya waliyo kwenda kwa gari ambazo hazikuwa na hesabu lakini, jahazi, mashua, ngarawa, mitumbwi na madau vyote vilitumika usiku kucha na asubuhi yake, kuwapeleka watu Malindi.

Mkoa wa Kusini, Unguja hasa Ndijani, kwa mujibu wa hesabu za siku ile gari 17, Chwaka gari 8, Makunduchi na vijiji vya jirani, hasa Kizimkazi, Unguja-Ukuu na Uzi, walipeleka zaidi ya gari 40.

Maeneo ya kandokando ya mji, kama Mfenesini, Mwera, Fuoni na Dimani pamoja na ndani ya mji kuanzia Jang’ombe hadi Bububu na eneo lote la Mji Mkongwe umati wa watu ulimiminika. Dk Omar Ali Juma (Waziri Kiongozi) wa siku hizo, alipata kiwewe. 

Mkutano huo ndiyo ambao ulitoa ujumbe kwa CCM na Serikali ya Dk Salmin na kuanzia hapo Dk Salmin, kila alipo akipanda kwenye majukaa katika mikutano ya hadhara ya CCM, alikuwa na tabia ya kurusha vijembe na maneno ya mafumbo, kama vile MWARI mpevu.

Sasa narudi katika mada yangu:  Maalim Seif wakitaka…wasitake anapendwa na watu wengi wala haijapata kutokea kwa kiongozi yoyote wa Zanzibar, baada ya Mapinduzi.

Hata, Wazanzibari waliyoko nje, kuanzia Tanganyika, Uarabuni, Ulaya, Mareknai na Canada na nchi nyingine ambazo wapo watu wenye asili ya Unguja na Pemba. Maalim Seif, wanampenda. Akifika humpa mapokezi makubwa ya heshima.

Akiwa katika ziara yake nchini Uingereza, hivi karibuni alipokutana na Wazanzibari, neno lake la kwanza Maalim Seif, alisema: “Nilidhani niko ukumbi wa SALAMA, Bwawani.”

Kauli hii ya Maalim Seif, iliashiria kwamba watu waliyomiminika kwenye ukumbi wa ‘Barking Abbey School’ hakutarajia.

Kauli yake ya kwanza alisema alidhani kwamba yuko ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, Unguja ambao ni maarafu kwa shughuli za mikutano.

Nikirudi kwa Wapemba na ziara za Maalim Seif: Jambo jema Wapemba, hawako tayari kutawali na Tanganyika. Kila uchaguzi hata uwe katika vitisho vya kijeshi, hawatetereki wala kutishika hawamchagui CCM.

Tukio ambalo liliwafanya wa-Pemba kushikamana zaidi ni mwaka 1988, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rashid Kawawa alipowambia Wapemba kuwa, asiyeitaka CCM ahame.

Tukio lenyewe lilikuwa hivi: Rashid Kawawa, mwaka 1988 alikuwa ni Katibu Mkuu wa CCM, alifika Pemba, kwa lengo la kuimarisha chama. Ni baada ya kufukuzwa CCM akina Maalim Seif na wenzake wengine sita wote kutoka Zanzibar.

Hali ya uhai wa CCM Unguja na Pemba, lakini hasa Pemba, ilikuwa mbaya. CCM ilielekea kufa kifo cha mende miguu juu. Wapemba, walikasirishwa sana na hatua ya CCM ya kuwafukuza viongozi wao.

Kwa upande wa Pemba, waliyofukuzwa walikuwa Maalim Seif, wenzake wengine ni Maalim Soud Yussuf na Suleiman Seif (Mwenyezi Mungu awarehemu) na Hamad Rashid Mohamed ambaye siku hizi kajiunga katika Serikali ya Dk Shein.

Kutoka Unguja, waliyofukuzwa CCM ni Shabaan Khamis Mloo (Mwenyezi Mungu amrehemu), Ali Haji Pandu na Khatib Hassan ambao wote baadaye wakaja wakawa ni waanzilishi wa CUF.

Itaendelea part lll

Share: