Habari

Maalim Seif ampagawisha Lipumba na gengi lake

Maalim Seif Sharif Hamad mwanachama mpya/lakini mwenyeji wa ACT Wazalendo na kauli mbiu ya ‘Ulipo Tupo’

kutoka vyanzo mbalimbali

Jumanne, Machi 19, 2019

Kauli mbiu au niseme mbiu ya mgambo ya Maalim Seif: “Wakati ni huu, wakati ni sasa…shusha tanga, pandisha tanga safari iendelee.”

Ni mbiu ya mgambo ya Maalim Seif Sharif Hamad kwa wanachama na wafuasi wake akiwataka washushe bendera za CUF na wapandishe za ACT-Wazalendo. Chama kipya walichochagua kujiunga siku ya Jumatatu, Machi 18, 2019.

Siku hiyo ni ya kipekee itakumbukwa kuwa Maalim Seif alibadili historia yake akiwa miongoni mwa viongozi waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF) miaka 27 iliyopita.

Maalim Seif kiongozi asieyumba wala kukata tamaa alitangaza rasmi kujiunga na chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kilichoanzishwa mwaka 2014 chama kichanga sana kikilinganishwa na CUF.

Maalim Seif: “Nawatangazia Watanzania wote na hasa wanachama wa CUF waliyowengi waliokuwa wakituunga mkono kutoka kila pembe ya nchi, Tanzania Bara na Zanzibar, kwamba mimi na wenzangu tunajiunga na chama cha ACT Wazalendo.”

Tunawaomba na wao wote waungane na nasi kujiunga na jukwaa hili jipya kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tukiifanya kupitia CUF,” alisema Maalim Seif.

Kauli hiyo ya Maalim Seif ilifuatiwa na mwitikio wa kundi la wafuasi waliokuwa nje ya ukumbi wa ofisi ya wabunge wa CUF Magomeni, Dar es Salaam kwamba wanamfuata katika chama alichohamia.

Ofisi hiyo iliyokuwa inatumiwa na wabunge 28 wanaomuunga mkono Maalim Seif, na baada ya tangazo la kuhamia ACT Wazalendo maandishi ya CUF yaliyokuwa kwenye bango nje ya ofisi hiyo yalifutwa rasmi.

Uamuzi wa Maalim Seif aliyekuwa katibu mkuu wa CUF kwa miaka mingi ulitokana na kushindwa kesi namba 23 ya mwaka 2016 waliyoifungua kuilalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba haina mamlaka ya kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho.

Maalim Seif, ambaye safari yake ya kisiasa ilianzia CCM ambako alifukuzwa na chama hicho 1988 kabla ya kutumikia kifungo cha kisiasa jela kuanzia Mei 1989 hadi Novemba 1991.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumatatu Machi 19, Maalim Seif alisema baada ya kushindwa kesi mahakamani wameona kuna haja ya kutafuta jukwaa jingine la kuendeleza mapambano ya kisiasa waliyokuwa wakiyasimamia kupitia CUF.

Maalim Seif, baada ya kutoka jela 1991 alishiriki kuanzisha CUF 1992, kwa kuviunganisha vikundi viwili vya Kamahuru kilichokuwa kikipigania demokrasia Zanzibar na Civic Movement kundi la kupigania haki za binadamu Tanzania Bara chini ya uongozi wa James Mapalala.

Kuhusu wabunge 28 wanaomuunga mkono, alisema wamewaachia uhuru wa kuamua kama watapenda kuhamia ACT Wazalendo au kubaki CUF.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), alisema wamekwenda ACT Wazalendo kama wanachama wa kawaida na hakuna aliyefuata vyeo au kuahidiwa cheo katika chama chao kipya.

“Hatua tunayochukua leo (Jumatatu 18/3/2019) ni kuandika historia mpya ya mabadiliko ya kisiasa Tanzania, kote Zanzibar na Bara. Umma haujawahi kushindwa popote duniani….ndivyo historia inavyoonyesha kote. Hatuna wasiwasi kwamba umma wa Watanzania nao utashinda,” alisema Maalim Seif..

Maalim Seif ambaye ni gwiji wa masuala ya siasa, kiongozi mwenye upeo na kipenzi cha Wazanzibari amewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, alisema katika jukwaa lao jipya la kisiasa wao watashirikiana na vyama vyote makini.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewataja viongozi na wanachama wengine waliofukuzwa uanachama katika mkutano mkuu uliofanyika kati ya Machi 13 hadi 15, 2019.

Licha ya siku ya Jumatatu Profesa Lipumba kusema kuwa Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa waliofukuzwa kutokana na mwenendo wake wa kukidhoofisha chama hicho pia alitaja viongozi wengine.

Akizungumza Ofisi za CUF, Buguruni, Dar es Salaam Jumanne Machi 19, 2019 Profesa Lipumba aliwataja Ismail Jussa, Salim Biman, Issa Kheri, Mohammed Nur na Said Ali Mbarouk wote wa Zanzibar, Tanzania bara ni Mbarala Maharagande, Abdallah Katawi na Joran Bashange.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama hao waliofukuzwa CUF siku ya Jumanne Machi 19 walikabidhiwa kadi za chama cha ACT Wazalendo akiwamo Maalim Seif.

“Mkutano mkuu umeazimia kuwafukuza uanachama kutokana na mwenendo wao usioridhisha na kuwa karibu na Maalim Seif ambaye amesababisha CUF kudhoofika,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi, aliwataka wanachama wa CUF hasa Zanzibar kuacha kufuata mkumbo kwenda chama kingine badala yake wabakie CUF ili kuijenga

“Msimfuate Maalim Seif bakini tuijenge CUF, tumetoka mbali hasa wanachama wa Pemba. Maalim Seif ni mharibifu na ameangukia ACT- Wazalendo ambayo ipo mahututi,” alisema Profesa Lipumba.

Wakati huohuo, waliyokuwa wanachama wa CUF Wilaya ya Micheweni, Pemba wameunga mkono uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT Wazalendo kwa kubadilisha kwenye milingoti bendera za CUF na kupandisha za ACT Wazalendo. “ulipo tupo.”

Baadhi ya Ofisi za Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar zimeanza kubadilishwa bendera na kupakwa rangi inayotumiwa na Chama cha ACT Wazalendo.

Aliyekuwa Katibu wa CUF Wilaya ya Chake chake Pemba, Saleh Nassor Juma alisema wamepokea maagizo kutoka uongozi wa juu ambayo yamewataka waanze kubadilisha rangi na bendera za matawi yao.

Uamuzi huo ambao umeanza kutekelezwa katika ofisi moja ya Chake chake ni wa kubadili kutoka rangi ya awali ya CUF na kupaka ya Chama cha ACT Wazalendo.

Miongoni mwa matawi ambayo yameanza kubadilishwa rangi ni ofisi ya Jimbo ya Chake chake na kuonekana kuwa na rangi za Chama cha ACT Wazalendo.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Vijana CUF, Khalifa Abdallah alisema wanajivunia umma walionao ambao unamuunga mkono Maalim Seif.

Harakati hizo za kubadilisha bendera na rangi katika matawi mapya ya ACT Wazalendo Pemba zimepamba moto huku wanachama hao wapya wa ACT wakiomba kupelekewe bendera hizo haraka na kwa wingi.

Katika wilaya ya Micheweni, Pemba matawi mbalimbali yanaendelea kubadilishwa bendera hizo na wananchi waliyowengi wanaonekana ni wenye kufurahia hatua hiyo.

Sherehe hiyo ya kubadilisha bendera inaongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid akiwa pamoja na viongozi wezake ambao tayari wemehamia ACT Wazalendo.

Rashid alisema wanachokifanya kwa sasa ni kubadili bendera maeneo yote na kufungua matawi mengine mapya ya ACT Wazalendo katika maeneo yote ya Wilaya ya Micheweni.

Alisema hatua ya mageuzi kuachana CUF na kuhamia ACT Wazalendo ni hatua ya kushtukizia bila kujipanga baadhi ya maeneo mengine kuna ukosefu wa vifaa hususan bendera na rangi.

Kutokana na upungufu wa vifaa hivyo Rashid Khalid, aliwaomba viongozi wakuu wa ACT Wazalendo kuharakisha wanawapelekea bendera hizo kwa wingi mapema sana.

Naye, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa zamani wa Jimbo la Micheweni, Thubeit Khamis (CUF), alipoulizwa kuhusu majengo ya ofisi za CUF wanaamuaje kufanya mabadiliko alisema majengo mengi ya ofisi za chama ni ya wananchi wenyewe waliojitolea hivyo si miongoni mwa mali za CUF.

Lakini, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kuhusu hatua hiyo ya kuzibadili rangi na bendera ofisi yeye alisema, “sina maoni yoyote.”

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini alisema: “Ninachojua harakati za kudai demokrasia lazima ziendelee…Sisi tutamuunga mkono Maalim Seif kwa hatua yoyote atakayochukua.” Zitto pia alisema, “kama kuna jambo Watanzania watajulishwa rasmi.”

Share: