Habari

Maalim Seif ashtukizia mpango wa kumezwa Zanzibar

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu akikabidhi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi hati miliki ya ardhi ya eka 30 kwenye eneo, maarufu ‘Mji wa Serikali Dodoma.’

Eka hizo 30 zimetolewa na Serikali ya Muungano kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zitumike kwa shughuli za majengo ya ofisi na makazi kwa viongozi wa Serikali ya Zanzibar.

Hafla hiyo ilifanyika Jumamosi, Februari 9, 2019 katika Ukumbi wa Kambarage, jengo la hazina Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Kamati ya Pamoja kilichoketi kujadili masuala ya Muungano.

Kikao hicho kimeongeza wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar juu ya khatma ya nchi yao hasa wakati huu wa uongozi wa kibabe wa Rais wa Muungano, Dk John Magufuli na ulaini wa uongozi wa sasa wa Zanzibar ambao la muhimu kwao ni madaraka si nchi.

Kuna tetesi kuwa kuna njama zinaandaliwa kuimeza Zanzibar. Na hichi kilichofanyika kupewa eka 30 ni ishara mbaya sana kwa Zanzibar na watu wake. Lisemwalo lipo au lipo njiani linakuja..

Unguja, Zanzibar
Jumatatu, Februari 11, 2019

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema wamebaini dhamira walioyonayo CCM kutaka kuifanya Tanzania yenye serikali moja itakayoongoza Zanzibar na Tanzania bara.

Akizungumza na viongozi wa CUF katika mkutano uliyofanyika Ofisi za Kilimahewa Unguja, Maalim Seif alisema Rais Magufuli hajakaa vizuri kuhusu Zanzibar. “Huyu mtu hajakaa vizuri kuhusu nchi yetu”

Maalim Seif alisema wanaamini mikakati inayoendelea kupangwa na kuratibiwa ikiwamo ya kununua wabunge inalenga kuifanya Tanzania kuwa na serikali moja.

Katika hotuba yake Maalim Seif, alimnukuu Rais Magufuli kwamba: “Yote yaliyomshinda Nyerere yeye (Magufuli) atayatekeleza ikiwa ni pamoja na kuichukuwa Zanzibar kuwa serikali moja.”

Aliongeza: “Namwambia mbele yunu na mbele ya Mungu, Magufuli unajidanganya…sawa sawa. Wazanzibari kwa ujumla wetu wale ambao wako kwenye CCM, wako kwenye CUF, wako kwenye CHADEMA madam ni Mzanzibari kwanza ni nchi yake.”

Akifafanua zaidi Maalim Seif alisema suala hilo haliwezi kukubalika kwa sababu Serikali ya Zanzibar ipo kwa mujibu wa katiba hivyo kuifuta ni kuvunja katiba:

“Mtatugawa kwa mambo mengine kama mnavyojaribu lakini tukija kwenye maslahi kwenye kupigania kuweko kwa nchi yetu ya Zanzibar, Wazanzibari sote ni kama nyuki tumeshikamana,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu migogoro ya CUF, alisema wanachama wamejiandaa na matokeo yoyote yatakayotolewa na mahakama na kwamba, iwapo watashindwa haitakuwa mwisho wa harakati za siasa kwa upande wao.

Akizungumzia madai hayo, Katibu wa Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao alikanusha madai hayo akidai hiyo si ajenda ya CCM na hawajawahi kufikiria suala hilo.

Catherine alisema kila kitu kinaendeshwa kwa misingi ya kikatiba na ilani ya CCM, hivyo suala hilo halimo katika pande zote hizo.

Alisema kila mtu anafahamu katiba imeweka wazi uwepo wa serikali mbili kwenye nchi moja na kila moja inafanya kazi kwa mujibu wa katiba.

“Hakuna sehemu yoyote kwenye katiba ya chama wala nchi inayoonyesha kuwa CCM ina ajenda ya kuleta Serikali moja Tanzania,’’ alisema Catherine.

Share: