Habari

Maalim Seif atembelea AZAM TV

Na: Hassan Hamad (OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu mchango unaotolewa na kampuni ya Azam, katika kukuza na kuendeleza sekta ya habari nchini.
Amesema kampuni hiyo inayomilikiwa na mwekezaji mzalendo, imeonesha mafanikio makubwa tokea ilipoanzisha kituo cha televisheni cha (Azam TV) takriban miaka miwili iliyopita.

Maalim Seif ametoa pongezi hizo wakati akitembelea studio za “Azam TV” jijini Dar es Salaam na baadae kufanya mahojiano maalum na kituo hicho.

Amesema kituo hicho kimeonesha ufanisi mkubwa wa kiutendaji na vitendea kazi, hasa ikizingatiwa kuwa kimetoa kipaumbele kwa wafanyakazi wazalendo ambao wamepata fursa ya kuendeleza taaluma na vipaji vyao.

Ametoa wito kwa wawekezaji wazalendo kuiga mfano wa kampuni hiyo kwa kuwekeza miradi mikubwa hapa nchini, ili iweze kuwasaidia vijana kuondokana na tatizo la ajira linalowakabili.

Amesema hatua ya wawekezaji wazalendo kuwekeza miradi mikubwa kama hiyo, pia inaijengea heshima Tanzania katika jamii ya kimataifa na kuijengea mazingira mazuri ya ushindani wa kibiashara katika soko la ajira.

Akizungumzia kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kurejesha hali ya Amani, Utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Amesema amani iliyopo ni hazina kubwa kwa Taifa, na kuwasisitiza wananchi kuienzi na kuilinda hazina hiyo ambayo imelitengea sifa kubwa Taifa la Tanzania na wananchi kwa ujumla.

Amefahamisha kuwa Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa itaendelea kuwepo hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktobar mwaka huu, kwani imewekwa kikatiba na kwamba wananchi walio wengi bado wana imani nayo kutokana na mafanikio yake.

Kuhusu utendaji wake wa kisiasa, Maalim Seif ambaye tayari ametangazwa rasmi kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), amesema ameamua kuingia tena kwenye kinyang’anyiro hicho akiamini kuwa bado anazo nguvu za kutosha, uwezo na fikra mpya za kuwatumikia wananchi.

Kwa upande wake Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa (Azam TV) Bw. Tido Muhando, amesema kampuni hiyo imewekeza mitambo ya kisasa katika kituo hicho na kuwa na studio bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema lengo la kituo hicho ni kuwa na matangazo bora yatakayotolewa kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza kupitia (Azam TV 1 na 11) ambayo yatakidhi ushindani wa sekta ya habari kitaifa na kimataifa.

Sambamba na hilo Bw. Tido amesema kampuni hiyo pia inakusudia kuanzisha kituo cha Radio ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao, na kwamba masafa (frequency) ya radio hiyo tayari yameshapatikana kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema walishawishika kuanzisha vyombo vya habari kwenye kampuni hiyo baada ya kuanzishwa timu ya soka ya Azam, na kuona haja kuitangaza kupitia televisheni.

Amefahamisha kuwa kampuni hiyo inajipanga ili kuhakikisha kuwa inakidhi mahitaji ya wateja wake katika ulimwengu wa soka kwa kuonesha mechi zote za kimataifa baada ya kufanya mazungumzo na kampuni nyengine zinazoratibu matangazo ya aina hiyo.

Zanzinews

Share: