Habari

MAALIM SEIF AWASILI SENEGAL KUSHIRIKI MKUTANO MKUU WA 62 WA LIBERAL INTERNATIONAL:

MAALIM SEIF AWASILI SENEGAL KUSHIRIKI MKUTANO MKUU WA 62 WA LIBERAL INTERNATIONAL:

THE CIVIC UNITED FRONT [CUF-CHAMA CHA WANANCHI]
TAARIFA KWA UUMA NA VYOMBO VYA HABARI

TAREHE: 29 NOVEMBA, 2018

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui wamewasili Dakar, Senegal jana usiku tayari kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa 62 wa Liberal International unaoanza leo.

Maalim Seif pia amepewa heshima kubwa ya kuhutubia Mkutano huo kesho Ijumaa, tarehe 30 Novemba, 2018 katika mjadala wa kupitisha maazimio utakaofanyika kuanzia saa 9 mchana hadi saa 10 jioni (kwa saa za Senegal). Kwenye jopo litakalozungumza wakati wa mjadala huo wa maazimio, Maalim Seif ataungana na Rais wa Liberal International, Juli Minoves, na Makamu wawili wa Rais wa Liberal International ambao ni Karl Heinz Paque na Abir Al-Sahlani.

Mkutano Mkuu huo unashirikisha wajumbe takriban 300 kutoka vyama vya kiliberali vya nchi mbali mbali duniani kutoka Amerika ya Kaskazini na Kusini, Ulaya, Afrika, Asia na Australia.

Rais Macky Sall wa Senegal, Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast, Rais Adama Barrow wa Gambia, Rais George Weah wa Liberia pamoja na Waziri Mkuu Charles Michel wa Belgium ni miongoni mwa wanaohudhuria Mkutano Mkuu huo wa Liberal International.

Kesho hiyo hiyo, Maalim Seif atakuwa ni miongoni mwa viongozi wakuu 20 ambao ni pamoja na Marais na Mawaziri Wakuu wanaoshiriki Mkutano Mkuu huo watakaokuwa na kikao maalum kitakachofuatiwa na dhifa ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na Rais Macky Sall wa Senegal.

Mbali na kushiriki Mkutano Mkuu huo wa Liberal International unaotarajiwa kumalizika kesho usiku, mnamo siku ya Jumamosi ya tarehe 1 Desemba, 2018, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Naibu Katibu Mkuu, Mhe. Nassor Mazrui wamealikwa kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha APR cha Rais Macky Sall ambao unatarajiwa kumthibitisha Rais huyo kuwa Mgombea Urais wa Senegal kwa kipindi cha pili katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2019.

Baada ya kumaliza shughuli hizo, viongozi hao wa CUF watarudi London kwa ajili ya kuunganisha na safari ya kurejea nyumbani.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari CUF Taifa kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Ismail Jusa Ladhu.-+255 777414100

HAKI SAWA KWA WOTE

SALIM BIMANI
MKURUGENZI HABARI
+255 777 414112
+255 655314112

MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI HABARI
maharagande@gmail.com
+255 715062577
+255 767062577

Share: