Habari

Maalim Seif: Haturudii uchaguzi Mkuu Z’bar ng’o.

Na Rahma Suleiman
6th November 2015

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema CUF inaendelea kutafuta haki ya Wazanzibar ya kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya CUF Mtendeni juzi, baada ya kurudi safari yake ya kuonana na rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Aliwaambia wanachama hao kuwa hakuna kurudi nyuma katika kudai haki yao kwa njia ya amani na utulivu ili matokeo yatangazwe na mshindi wa urais ajulikane.

“Niwahakikishieni vijana na wanachama wa CUF kuwa hakuna kurudi nyuma, tunaendelea kudai haki yetu na tunashukuru dunia nzima inatuunga mkono kwa hili,”alisema Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Alisema kuwa wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mpango wao ni kutaka kuendelea kuwa katika madaraka wakijua kuwa muda wa Dk. Ali Mohammed Shein wa kukaa madarakani umekwisha, lakini wanang’ang’ania aendelee kinyume cha Katiba.

Aidha, alisema kuwa hakuna dawa yoyote ya kumaliza mgogoro ulipo Zanzibar isipokuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu ili mshindi ajulikane na kuapishwa.

“Wanaosema kuwa uchaguzi urejewe waachieni wenyewe, sisi katika CUF hakuna msamiati huo kwa sasa kurejea uchaguzi, huo ndio msimamo wetu,” alisisitiza Maalim Seif.

Alisema kuwa kwa uwezo wa Mungu haki yao wataipata na kuwataka vijana kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kutunza amani ya nchi kwa kutokubali kuchokozeka. Alisema CUF na viongozi wake hawatakubali kuwa chanzo cha kuvuruga amani ya nchi na wataendelea kuhubiri amani wakati wote.

Mvutano wa kisiasa unaoendelea Zanzibar ulisababishwa na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar wa rais na wawakilishi Oktoba 28, kwa madai kuwa ilibaini kuwapo kwa kasoro kadhaa kisiwani Pemba.

Hata hivyo, waangalizi wa nje na ndani wameeleza kushangazwa ha hatua ya Jecha, kwa kuwa hawakushuhudia kasoro zozote hadi walipotoa ripoti ya awali.

Aidha, asasi za nchini na mataifa kadhaa yakiwamo Uingereza, Ireland na Marekani yameshatoa taarifa ya kushangazwa na uamuzi wa Jecha na kushauri mchakato wa kutangaza matokeo uendelee.

MTOTO WA KARUME AIBUA MAPYA

Mjadala kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na Jecha, umechukua sura mpya, baada ya mmoja wa watoto wa Rais wa zamani, Dk. Amani Abeid Karume, kuibuka na kufichua kile anachoamini kuwa ni sababu ya utata uliojitokeza sasa.

Mtoto huyo ni Mwanasheria, Fatma Karume, ambaye akiwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, waliuambia umma kupitia mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha televisheni jijini Dar es Salaam juzi kuwa sababu mojawapo ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni muundo wa uongozi unaomruhusu rais wa visiwa hivyo kuwa mmoja wa wajumbe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akifafanua, Fatma alisema kuwapo kwa nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Mawaziri kunaibua mgongano inapotokea mshindi wa upande mmoja akiwa ni wa kutoka chama kingine na hiyo ni sababu mojawapo wanayoamini kuwa imechangia kufutwa kwa uchaguzi na pia kukwaza ukuaji wa demokrasia visiwani humo.

Alisema ni dhahiri hali huwa ngumu kwa baraza la mawaziri linaloundwa na watu wa itikadi ya chama kimoja kuchanganyika na mwingine mwenye itikadi tofauti, hasa katika mazingira ya kuwa na usiri katika baadhi ya mambo na kwamba, hilo huchangia kusuasua kwa maendeleo ya kidemokrasia visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, ili kuondokana na mgogoro kama uliopo sasa, Fatma alisema ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini na kwingineko barani Afrika kuzingatia sheria na katiba zilizopo.

Awali, ilisisitizwa na wanasheria hao kuwa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Zec peke yake, haukuzingatia sheria na katiba na ndiyo maana sasa kumeibuka mgogoro wa kikatiba kwani kifungu kinachotumika kuhalalisha hoja ya kuendelea kubaki madarakani kwa Dk. Shein kimekuwa kikitafsiriwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa.

Akielezea zaidi, Awadh alisema hakuna kifungu chochote kinachomruhusu Jecha kufuta uchaguzi na ndiyo maana hadi sasa hakuna mtu aliyethubutu kutaja kwa uwazi ni sheria ipi imempa nguvu mwenyekiti huyo wa Zec kufuta uchaguzi wa Zanzibar.

CHANZO: NIPASHE

Share: