Habari

Maalim Seif: kukosekana SUK kumeleta ubaguzi Zanzibar

By Muhammed Khamis – Mwananchi
Jumapili, Disemba 2, 2018

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamadi amesema maridhiano ya Wazanzibari yaliyoasisiwa na kupelekea kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) yamepotezwa na watu wasioitakia mema Zanzibar, kwa maslahi yao.

Alisema wananchi wa Zanzibar kwa kipindi kifupi cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), walijawa na matumaini mengi na yalipotea ghafla baada ya serikali ya mfumo huo kutokuwepo.

Maalim Seif aliyasema hayo Mjini London mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza.

Akitaja madhara ambayo yametokea baada ya serikali ya mfumo huo kutokuwapo, Maalim Seif alisema ni kuwapo kwa ubaguzi mkubwa katika sekta ya ajira na kudai hivi sasa ili uajiriwe unalazimika kuwa na kadi ya CCM.

Sambamba na hilo, Maalim Seif aligusia mbinu zinazofanyika hivi sasa ikiwemo kuwanyima vitambulisho wananchi wasiounga mkono CCM.

“Tunaambiwa wakimaliza uandikishaji huu wa vitambulisho watakuja na uandikishaji mpya wa Tume ya Uchaguzi huku malengo yao yakiwa ni kupunguza wapiga kura wa chama chetu kwa asilimia 30 ili waweze kushinda,” alisema Maalim Seif.

Sambamba na hilo, Maalim Seif alisema kuwa licha ya uwepo wa mazingira hayo, CUF itaendelea kubaki imara na itashinda kila uchaguzi utakaofanyika.

Alisema mazingira ya ushindi kwenye chama chao hutokana na wananchi waliyowengi Zanzibar, kuchoshwa na CCM na ndio maana wamekuwa wakimpa yeye kura nyingi zaidi.

Pia, alisema kukosekana kwa SUK kumesababisha kuwapo kwa maisha magumu kwa wananchi na kukithiri kwa rushwa na ufisadi.

Aidha, Maalim Seif alidai kuwa mazingira hayo yamepelekea kuibuka kwa wimbi la ufisadi na huku kila mmoja akiwa ‘busy’ kujilimbikizia mali.

Alizungumzia pia kile alichokiita ‘kukandamizwa kwa siasa za upinzani Tanzania’ jambo ambalo alisema ni wazi kwamba CCM imedhamiria kutaka kuumaliza upinzani.

Akizungumzia madai ya Maalim Seif, Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Dk Hussein Khamis Shabani alisema hayana ukweli kwa kuwa mamlaka yake imeweka utaratibu maalumu kwa mujibu wa sheria zao.

Alisema utaratibu huo unaruhusu kila aliyefikisha umri wa miaka 18 na kuwa mkaazi wa eneo husika analotaka kuandikisha anaandikishwa.

Alisema kuboreshwa kwa vitambulisho hivyo ni jambo la kawaida na si kama wanavyodhani baadhi ya watu kuwa vinahusishwa na uandikishwaji wa daftari la wapiga kura.

Aliwataka wananchi wafahamu kwamba kuna tofauti baina ya vitambulisho hivyo na daftari la wapiga kura na si vyema kuchanganya mambo hayo mawili pamoja.

Kuhusu ubaguzi wa ajira, Katibu wa Tume ya Utumishi Serikalini, Mohamed Khamis alisema kila kitu wanachokifanya kuhusu ajira kipo wazi na tume hiyo hutoa matangazo kila sehemu na watu hujitokeza kuomba bila kujali itikadi zao.

Alieleza kushangazwa na wanaosema kuna ubaguzi kwenye ajira wakati matangazo hutolewa na usaili hufanyika na wanaokidhi vigezo na kufaulu huajiriwa.

Share: