Habari

Maalim Seif: Kuna njama za kutunyang’anya chama

Muhammed Khamis – Mwananchi
Jumapili, Februari 10, 2019

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amedai kuna mikakakti inapangwa kuwapokonya chama hicho na kusema njama hizo hazitafanikiwa wala kuwavunja nguvu ya kudai haki yao mahala popote.

Akizungumza Mkoa wa Mjini Magharibi baada ya kuhitimisha ziara yake ya ujenzi wa chama katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, wiki iliyopita, Maalim Seif alisema kuna njama zinaratibiwa za kumkabidhi Profesa Lipumba chama.

“Ninafahamu zipo njama mbalimbali zenye lengo la kunyang’anywa chama na kundi linalomuunga mkono mwenyekiti wa zamani Profesa Ibrahim Lipumba.”

“Hata kama watafanikiwa hatutanyamaza tutaendelea na harakati za kudai haki kwa misingi ya kikatiba kwani ndiyo kazi ya siasa,” alisema Maalim Seif.

Alisema anasikitishwa na wanaofanya na kuratibu mkakati huo wakishindwa kujua kuwa wanaminya demokrasia pamoja na kupalilia chuki miongoni mwa wananchi.

“Hili na mengine mengi hayataturudisha nyuma na mapambano yataendelea kama kawaida, hilo nataka kila mtu ajue ingawa njia ni nyingi,” alisema Maalim Seif.

Awali, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF upande unaomuunga mkono Maalim Seif, Omar Ali Shehe aliwataka wanachama wa chama hicho kutovunjika moyo na waendelee na mshikamano.

“Yanayoendelea kutokea sasa yote ni kwa sababu ya nguvu ya chama chetu jambo ambalo limekuwa likiwakera baadhi ya watu na ndiyo maana wanaratibu mikakati kukihujumu,” alisema Omar.

Akizungumza na Mwananchi juu ya tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa CUF upande wa Profesa Lipumba, Nassor Seif Amour alisema kauli za Maalim Seif na wenzake hazina ukweli kwani hawana nia ya kunyang’anya chama.

Alisema kinachofanyika ni kutaka kuona katiba ya chama hicho inafuatwa na kutekelezwa badala ya kuwaachia baadhi ya watu kuendesha kwa matakwa na maslahi yao binafsi: “CUF ni chama cha wananchi wote.”

Share: