Habari

Maalim Seif: Nikipitishwa tena nitagombea urais

Ijumaa, Novemba 2, 2018

Gazeti la Mwananchi la siku ya Jumatano, Oktoba 31, 2018 kupitia Mwandishi Muhammed Khamis, liliandika mahojiano yake aliyomfanyia Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF), kuhusu mustakabali wa kiongozi huyo kuelekea uchaguzi mkuu, takriban muda wa miaka miwili ijayo.

Mwandishi Muhammed Khamis, alianza makala yake:

Siasa ndio mfumo wa maisha kwa baadhi ya watu, wengine wakiamini ndio njia sahihi ya kuwatetea walio wengi katika shughuli zao za kila siku.

Unapotaja au kuzungumzia siasa kwenye ukanda huu wa Afrika hutaacha kuizungumzia Zanzibar ambapo wengi huamini ndiyo kitovu cha siasa kwenye ardhi ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Zanzibar ni maarufu kwa vuguvugu la siasa za upinzani, kinara wake akiwa mwanasiasa mkongwe wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye wakati wa uenyekiti wa Musobi Mageni, yeye (Maalim) alikuwa makamu mwenyekiti. Mageni alikuwa mwenyekiti wa CUF kati ya 1995 hadi 1999.

Wakati Profesa Ibrahim Lipumba alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, katibu mkuu wake alichaguliwa Maalim Seif ambaye ameendelea kushika wadhifa huo hadi sasa.

Gazeti hili limefanya mahojiano maalumu na kiongozi huyo ambaye tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 amekuwa mgombea urais Zanzibar mara zote.

Swali: Unazitazamaje siasa za Zanzibar na zile za Bara. Je, zina tofauti zozote?

Jibu: Zanzibar ina historia na utamaduni wa ushindani hata kabla ya uhuru ambapo kulikua na vyama vilivyokuwa imara na vyenye nguvu, mfano wa Afro-Shirazi Party, Hizbuz, ZPP pamoja na Umma Party na vinginevyo.

Hata baada ya Mapinduzi ya Zanzibar vyama vingi havikuruhusiwa kuendelea na kulibakia chama kimoja pekee, lakini wananchi waliendelea kubaki na vyama vyao ndani ya moyo kwa muda mrefu na walikuwa wanaendelea kuviamini licha ya kutokuwepo rasmi.

Mara baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania jambo hilo kwa Wazanzibari halikuwa geni kwao na mara baada ya kuanzishwa kwa chama cha wananchi CUF, wananchi waliowengi waliunga mkono chama cha CUF.

Na hapo ndio uliporudi tena ushindani wa vyama vya siasa baina ya CUF na CCM, sasa wenzetu wa Tanzania Bara hawana historia hii ya kisiasa kwao.

Tanzania Bara hata kabla ya uhuru kulikuwa na vyama vidogovidogo, lakini zaidi chama ambacho kilikuwa na nguvu ni Tanu, hivyo baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, wananchi wa bara bado mazoea yao yalibaki kwenye chama kimoja pekee na ni Tanu ambayo mwaka 1977 iliungana na Afro-Shirazi na kuunda CCM, hivyo watu wengi waliendelea kubaki na kuijua CCM.

Kwa upande wa vyama vingine vilivyokuja baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kwa kweli havikuwa na mizizi madhubuti na isitoshe hawakupata wafuasi wengi na CCM kubaki kuwa na nguvu.

Lakini, baadaye mabadiliko yalianza kujitokeza hususan kutoka makundi ya vijana, walipata mwamko na kujiunga na vyama vingine vya upinzani ikiwemo CUF, Chadema na NCCR Mageuzi.

Swali: Kwa maoni yako unafikiri ni kwa nini vyama vingine vya upinzani visiwani Zanzibar havionekani kuwa na nguvu kama chama chenu?

Jibu: Chama chetu kimekua na nguvu kwa sababu ya kuwa na mizizi na mikakati imara ambayo vyama vingine havina na hata hao viongozi wanaongoza vyama, wananchi hawana imani nao na wamekuwa wakionekana wababishaji na wenye kutafuta maslahi yao.

Licha ya mazingira hayo, hata hao CCM kwa miaka yote wamekuwa wakijua kuwa CUF ndio chama tishio kwao na hii ni kutokana na wimbi kubwa la vijana wadogo wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kujiunga na chama chetu na hata watoto wa viongozi wakubwa wa CCM wanaunga mkono chama chetu.

Swali: Mwakani nchi yetu inaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. Je, chama chenu kitakuwa tayari kushiriki uchaguzi huo?

Jibu: Naamini bila shaka ikiwa kesi zetu zilizoko mahakamani zitamalizika na haki kutendeka tutaingia kwenye uchaguzi, tena tukiwa na ari mpya pamoja na mipango ya kukijenga chama chetu.

Swali: Joto la kisiasa Zanzibar halijawahi kupoa, unadhani nini kifanyike ili wananchi waendelee kufurahia maisha yao ya kila siku?

Jibu: Jambo ambalo linasababisha hali hii ni watawala kutokuwa tayari kuachia madaraka, chaguzi zote ambazo zimefanyika tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, chama chetu kimekuwa kikishinda, lakini wenzetu hawapo tayari.

Wenzetu wangekuwa na uungwana na kukubali maamuzi ya wananchi na kukubali kufanya kazi pamoja chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mimi nadhani joto hili la kisiasa lingepungua au kumalizika kabisa visiwani hapa.

Kwa sababu katika mfumo wetu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hakuna upande wowote ule ambao ungepoteza kwani wote wangekuwamo kwenye serikali. Sote tungekuwa washindi na tunafanya kazi kwenye serikali kuwatumikia wananchi wetu kwa salama na amani.

Swali: Kwa maoni yako unadhani Wazanzibari bado wanahitaji Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)?

Jibu: Naam, Wazanzibari wanahitaji kuendelea na mfumo huu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu waliona wenyewe katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, nchi ilikuwa na amani sambamba na ukuaji mkubwa wa maendeleo bila ya watu kubaguana.

Ni wazi kuwa wananchi wengi wanatamani kuendelea na mfumo huu, hata wale ambao awali walikuwa wanapinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa walifika wakati wakaelewa umuhimu wa umoja tuliouanzisha.

Nina hakika hata kesho ikiwa kutaitishwa kura ya maoni kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa bila Tume au Serikali kuingilia, zaidi ya asilimia 80 watapiga kura ya kutaka mfumo huu uendelee.

Swali: Kwa umri wako ulionao sasa unadhani kuna haja ya wewe kustaafu uongozi wa chama na kubaki kama mshauri?

Jibu: Bado mapema sana na sijawaza kuhusu hilo, kwani kwenye siasa kuna watu wanafikisha hadi umri wa miaka 90 wanaendelea kuongoza vyama vyao na hata kuwa sehemu ya serikali, seuze mimi mwenye miaka 70 sasa.

Naamini bado wanachama wetu wananipenda na wana imani na mimi na pindi wakiamua wao basi nitaondoka, lakini sitaondoka kwenye chama na kubaki kuwa mstaafu.

Swali: Mara CUF imekuwa imara upande wa visiwani, unadhani nini kinasababisha uimara uliopo Zanzibar ushindwe kuwapo bara?

Jibu: Nilishasema huko mwanzo kwamba Wazanzibari kwenye siasa ni tofauti kabisa na wenzao wa Tanzania bara, wakiamini jambo na kukubali kitu huwezi kuwabadilisha kabisa.

Sasa wenzetu wa Tanzania bara kwenye ulingo huu wa siasa hawakujengwa kwenye misingi mizuri ambayo ingeweza kuwafanya kuwa imara zaidi na kukuza chama chetu kule upande wa Tanzania bara kama ilivyo hapa Zanzibar.

Swali: Ulipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa SUK, changamoto zipi ulikutana nazo?

Jibu: Changamoto zilikuwa hazikosi maana mfumo wenyewe wa serikali ulikuwa mpya kinyume na ulivyozoeleka huko nyuma, pia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikwenda zaidi katika imani za watu.

Alisema wapo wengine hawakuwa na udhati ndani ya moyo wao wa kujenga umoja kwa Wazanzibari, hivyo ilikuwa changamoto kwa kiasi fulani maana wenzetu walianza kujigawa na wakati mwingine walishindwa hata kuja kwenye kazi ambazo mimi nilikuwa nahudhuria kama Makamu wa Kwanza wa Rais.

Wenzetu bado walikuwa na mawazo muda wote kwamba lazima CCM itawale na si wengine, hivyo kuingia kwa chama chetu serikalini wengine hawakupenda.

Pia, wenzetu wa CCM walikuwa woga wa mfumo wa Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, wakiamini kuwa huenda chama chetu kingeongeza nguvu zaidi kwa wananchi na chama chao kitadhoofika.

Swali: Kwa migogoro iliyopo ndani ya CUF, unadhani imefika wakati wa kumuiga Augustine Mrema, aliyeamua kuhama NCCR-Mageuzi na kukimbilia TLP?

Jibu: Siwezi kutoka kwenye chama hichi kwa sababu ya mgogoro huu wa kutengezwa na mtu aliekuwa mwenyekiti wetu kwa kusaidiwa na msajili, bali nitaendelea kubaki kwenye chama hichi hadi mwisho wangu.

Kwa sasa tunasubiria kesi zetu na tunaamini kesi hizi ipo siku zitamalizika na chama kurudi kuwa imara zaidi, hivyo sitaondoka na nitabaki kuwa CUF kwenye maisha yangu yote.

Wengine hawajui chama hiki kilipotoka maana mimi na wenzangu ni miongoni mwa waasisi wa chama hichi tangu harakati za kuanzishwa kwake.

Swali: Kwa muda mrefu umekuwa ukiwahimiza wafuasi wako wavumilie mambo mazuri yanakuja, ni mambo gani yanakuja na lini?

Jibu: Siasa sio vita kama wanavyodhani au kutamani wengine bali siasa ni mfumo wa kuwaeleza wananchi sera za chama chako, ndio maana nimekuwa nikiwasisitiza wanachama wetu kuendelea kutulia licha ya haki yetu kwa miongo kadhaa kuporwa.

Nafikiri wapinzani wetu katika siasa bado wanaendelea kuamini hadi leo hii siasa ni vita au ugomvi, lakini ukweli siasa haipo hivyo bali, ni mfumo mzuri na wenye kunadi sera sahihi kwa wanachama wako.

Tukirudi kwenye msingi wa suala lako kwamba nimekuwa nikiwaambia wananchi wa Zanzibar, mambo mazuri na watulie, kwanza niseme ni kweli nimesema kwa mara kadhaa suala hilo huku, nikiwa na matumaini makubwa kwamba wenzetu wa CCM pamoja dola watatambua msingi imara wa demokrasia lakini kwa makusudi wamekuwa wakiikanyaga demokrasia bila ya hofu.

Mfano wa wazi kabisa hivi nani asiyejua kama chama chetu kilishinda uchaguzi wa 2015, lakini kwa utashi wao bila kipengele chochote cha sheria walifuta uchaguzi na kuitisha mwingine ambao sisi hatukushiriki.

Sasa mimi binafsi na viongozi wengine tutaendelea na msimamo wa kudai haki yetu bila ya woga tukiamini kwamba siku moja haki itasimama.

Swali: Imesalia miaka miwili kabla mwaka 2020. Je, unajiandaa kugombea tena urais wa Zanzibar?

Jibu: Wanachama wa chama chetu ndio wenye jukumu la kuchagua nani awe mgombea urais kama ilivyo kwenye wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge, sasa ukifika huo wakati wa kufanya hivyo wanachama ambao ni wajumbe wa mkutano mkuu wa chama ndio wenye maamuzi ya mimi nigombee au nisigombee.

Lakini, niseme wazi iwapo wanachama wetu watakuwa tayari niendelee kugombea nafasi hiyo na nikijaliwa kuwa mzima wa afya, basi sioni sababu ya kukataa maamuzi ya chama changu.

Na nilishasema huko awali umri mkubwa si sababu ya kumfanya mtu asigombee nafasi za siasa au kuwa kiongozi kuna watu wanafikisha hadi miaka 90 wanaendelea na nyadhifa zao za kuongoza wengine.

Swali: Siku za hivi karibuni Wazee wa Chadema walionekana hadharani kukukaribisha kwenye chama chao. Je, hujafikiria kujiunga nao hadi sasa?

Jibu: Hapana sipo tayari kujiunga na Chadema wala chama kingine chochote kile kwa sasa zaidi ya CUF.

Nafahamu na nimesikia hilo kwamba wazee hao walitoa kauli ya kunikaribisha ila kwa sasa sipo tayari kufanya hivyo, kwani matumaini yangu makubwa yapo ndani ya CUF.

Najua kila mtu kwa mujibu wa katiba anayo haki ya kwenda chama chochote, ila mimi nitabaki kwenye chama hiki hadi maisha yangu yote.

Swali: Baada ya Julius Mtatiro kuondoka CUF na kujiunga na CCM huoni kwamba chama chenu sasa kimerejea kwa Profesa Ibrahim Lipumba?

Jibu: Hapana na hilo kamwe haliwezekani maana wanachama wetu wanafahamu ukweli kila kitu kuhusu yanayoendelea kwenye unaoitwa mgogoro ndani ya chama chetu, hivyo haiwezekani leo wala kesho kwamba chama kirejee kwa Lipumba ambaye si mwanachama wetu tena.

Watu wanashindwa kufahamu kwamba chama ni taasisi yenye kukusanya watu wengi na si watu wachache au mtu mmoja, sasa kutoka kwa mtu mmoja hawezi kukiyumbisha chama.

Hivi umesahau Lipumba alipojiuzulu kuwa mwenyekiti wa chama chetu tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu na mbona hatukuyumba na tuliendelea kuwa imara zaidi ya mwanzo.

 

Tagsslider
Share: