Habari

MAALIM SEIF: NIKO TAYARI KUFA

Mwandishi wetu (TANZANIA Daima) Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema  hayuko tayari kuvumilia vitimbi vya kiuonevu vya serikali na yuko tayari kufa  ikibidi.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Upenja juzi, Maalim Seif  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alilaani hatua ya kuzuiwa kufanya mkutano wake huko Kitope, Kaskazini Unguja wiki iliyopita licha ya kuwa na vibali vyote.

“Nimewasiliana na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na kumueleza  kuwa sikubaliani na mkutano wangu kufutwa na nipo tayari kupoteza maisha,” alisema Maalim Seif.

Hata hivyo, akizungumza kadhia hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Ikulu) Dk  Mwinyihaji Makame Mwadini alisema mkutano huo ulizuiwa kwa sababu za  kiusalama.

Alisema kuwa viongozi wa mkoa walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya  wafuasi wa CCM na CUF kuzua mzozo mkali kuhusu umiliki wa kiwanja cha  mkutano.

Dk. Mwadini alikiri kuwa kibali cha kufanyika kwa mkutano huo kilikuwa  kimetolewa, lakini baada ya kuzuka kwa mzozo huo, serikali ikatumia busara  kuuzuia kwa madhumuni ya kuepusha uvunjifu wa amani.

“Mvutano wa wananchi wa eneo hilo ulitupa wasiwasi sana kuhusu uwezekano wa  kuwepo uvunjifu wa amani na usalama wa kiongozi huyo, ndiyo maana mkuu wa mkoa  akatupa taarifa na sisi tukazuia kufanyika kwa mkutano huo hapo Kitope,” alisema  Dk. Mwadini.

Akifafanua, alisema walipokea ushauri wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo  ndivyo vyenye mamlaka ya kusimamia usalama wa raia na mali zao kwa mujibu wa  katiba.

Alisema kwamba baada ya mashauriano mazito ya viongozi wa mkoa na  Jeshi la Polisi, mkutano huo uliamuliwa kufanyika sehemu nyingine katika Uwanja  wa Upenja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Nawaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wafahamu vizuri sababu  zilizopelekea kuahirishwa kwa mkutano wa Makamo wa Kwanza wa Rais hapo Kitope,  ni suala la usalama baada ya kutokea kutoelewana kwa wananchi na kutishia  uvunjifu wa amani,” alisema.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaheshimu misingi ya demokrasia na  utawala bora, na serikali itaendelea kuheshimu mfumo wa vyama vingi na kulinda  misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

Wakichangia bajeti ya wizara hiyo, wawakilishi wa CUF walisema kuwa haikuwa  muafaka mkutano wao kuzuiwa wakati taratibu zote zilikuwa zimekamilika na kudai  uamuzi huo ulitawaliwa na mizengwe ya kisiasa.

Share: