Habari

Maalim Seif: Sina mpango kuhamia Chadema wala kuacha siasa

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad

By Muhammed Khamis – Mwananchi
Sunday, October 28, 2018

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema hana mpango wa kuhama chama hicho licha ya kuwapo kwa mgogoro aliouita wa kutengenezwa ambao umedumu kwa miaka miwili sasa.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa ni siku 47 tangu Baraza la Wazee wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wake, Hashim Juma walipomkaribisha agombee urais wa Zanzibar kupitia chama chao kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“CUF na Chadema ni kitu kimoja, CUF ikianguka Zanzibar, Chadema tunachukua nafasi na Maalim atachukua nafasi yake ileile ya kuchukua fomu ya urais Zanzibar pamoja na wabunge wake wote watachukua fomu kwa tiketi ya Chadema,” alisema Hashim.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Chadema na CUF walishirikiana na mmoja wa vigogo wa CUF, Juma Duni Haji alilazimika kuhamia Chadema ili kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho.

Kama Maalim Seif ataamua kukimbia mgogoro CUF na kujiunga na chama kingine, hatakuwa wa kwanza. Augustine Mrema alipofukuzwa uwaziri ndani ya Serikali ya CCM alihamia NCCR-Mageuzi ambako aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 1995.

Hata hivyo, ulipotokea mgogoro wa uongozi ndani ya NCCR-Mageuzi, Mrema na wafuasi wake walihamia Tanzania Labour Party (TLP) ambako pia aligombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2000.

Kabla ya Maalim Seif kutoa msimamo wake, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande alisema katibu mkuu wao alikwishatoa msimamo wa kutohama chama.

Alisema kiongozi huyo alishasema kuwa mgogoro uliopo ndani ya chama hicho hauwezi kuwafanya wafikirie mkakati mwingine (plan B) nje ya CUF kwa kuwa wana uhakika wa kuushinda.

Hata juzi, akiwa katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisi kwake Vuga mjini Unguja, Maalim Seif a alisema licha CUF kuwa katika mgogoro, haitakua sababu ya yeye kukihama.

Alisema huenda baadhi ya watu hawajui chama hicho kilipoanzia ndiyo maana wamekuwa wakiota kuwa siku moja ataondoka na kukiacha kikiongozwa na wengine, jambo alilosema haliwezi kufanyika.

“Chama hiki mimi na wenzangu ni miongoni mwa waasisi, sitaweza kuhama kamwe na wanaowaza kuhusu hilo wasahau kabisa,” alisisitiza. Alisema anaamini mgogoro ulipo kwenye chama chake utamalizika na hatimaye kitabaki salama.

Maalim Seif alisema migogoro kwenye chama wakati mwingine ni jambo la kawaida na CUF imewahi kuingia kwenye mgogoro mkubwa wakati wa James Mapalala alipokuwa mwenyekiti ambao ulimalizika na chama kikasonga mbele.

Hatima yake ulingo wa siasa
Akizungumzia kuhusu hatima yake kwenye ulingo wa siasa, Maalim Seif alisema hadi sasa bado hajafikiria kuacha kujihusisha na kazi hiyo akisema anaamini kuwa ana uwezo wa kuendelea kuwatumikia wanachama wake na Wazanzibari wote.

Alidai kigezo cha umri kwa mwanasiasa si hoja ya kumfanya astaafu kwa sababu wapo hadi wanasiasa wenye umri wa miaka 90 na wanaendelea na nafasi zao bila matatizo.

Maalim Seif alisema kwenye chama chake bado wananchi wanampenda na wanaendelea kuwa na imani naye, ndiyo maana amebaki na nafasi yake hiyo hadi sasa.

Alisema anaweza kuacha siasa na kuwatumikia wanachama wake hadi pale watakapokataa kuongozwa naye, lakini hawezi kuacha kwa sababu tu ya maneno na fikra za watu.

Share: