Habari

Maaskofu wajikosha baada ya kutoa waraka mzito!

Baraza la Maaskofu Zanzibar limekanusha halihusiki na waraka wa vitisho dhidi ya Wapemba na mpango wa kuhujumu Waislam kwenye miskitini kwa kutumia mabomu.

Tamko hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo Zanzibar, Askofu Michael Hafidh wakati akizunguimza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Kanisa la Pentekoste huko Mwanakwerekwe mjini Unguja jana.

Askofu Hafidh alisema waraka huo umewashtua na kuamua kuitisha kamati ya utendaji ya Baraza hilo kuujadili na kutoa tamko maalum kwa niaba ya makanisa na waumini wake visiwani Zanzibar.

Alisema kwamba waumini wa Kikristo na waumini wao kamwe hawatafanya vitendo vya kulipiza visasi na kanisa halihusiki na waraka huo uliolenga kuvuruga amani, mshikamano na umoja wa kitaifa Tanzania.

“Tunachukua nafasi hii kukanusha vikali kuwa taarifa hizo si za kweli, tunalaani kwa nguvu zetu zote, watu, mtu yeyote aliyehusika kueneza taarifa hizi za kizushi, zisizokuwa na msingi wowote zenye lengo la kuchafua kanisa na kuwatia hofu wananchi”, alisema Askofu Hafidh ambaye ni Askofu wa kanisa la Anglikana jimbo la Zanzibar.

Alisema kazi ya kanisa ni moja tu ambayo ni kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu na kamwe kanisa halitafanya umafia au kuingia katika mtego wa kijinga wenye malengo ya kuvuruga misingi ya umoja wa kitaifa na kuwataka waumini wake kuwa wahubiri wa amani.

“Tunapenda kuwahakikishia watanzania, uzushi na thuhuma zinazotolewa kupitia kipeperushi hicho hazitotuvunja moyo bali zitatuunganisha na kutuimarisha katika azma yetu ya kuhakikisha nchi yetu inabaki katika salama na amani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama”, alisema Askofu huyo.

Akielezea ujumbe wa vipeperushi hivyo vyenye kichwa cha habari “barua ya wazi ya wakristo na wabara wanaoishi Zanzibar kwa Kadinali Pengo”, Askofu Hafidh alisema tayari wameshachukua hatua ya kuvitaarifu vyombo vya ulinzi ili kuwasaka watu waliohusika kufanya vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Padri Cosmas Shayo alisema vitendo vya usambazaji vipeperushi vimekuwa vya kawaida na haviwezi kudharauliwa, siku za nyuma vilisambazwa na baadae matukio mabaya yakafuatia.

Padri Shayo alisema kwamba vyombo vya ulinzi lazima vichukue hatua za kuwatafuta watu wanaotoa vitisho na kuleta mitafaruku isioleta sura nzuri wakati waumini wa kikristo na kiislam wamekuwa wakiishi kwa maelewano kwa miongo mingi visiwani Zanzibar.

Naye Mchungaji wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania(KKKT) Malonda Shukuru Stephen, alipongeza hatua ya Serikali ya kukaribisha wachunguzi na wapelelezi wa kimataifa dhidi ya watu wanaofanya hujuma ya makanisa na kuwahujumu viongozi wa dini visiwani humu.

Kwa mujibu wa vipeperushi hivyo vinawataka wakristo na wabara wanaoishi Zanzibar kuungana na kuanza kuwahujumu watu wenye asili ya pemba wanaoishi Tanzania Bara pamoja na kuhujumu mali zao.

“Sisi wakristo na watu wenye asili ya Bara tunaoishi Zanzibar tunakutaka uelewe kwamba huku Zanzibar hususan Wapemba hawatutaki tuishi huku”, sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Kadinali Pengo imemeeleza.

Waraka huo unaiowataja baadhi ya wanasiasa wakiwemo baadhi ya viongozi waliko kwenye Serikali ya Umoja wa Kiataifa kuwa ndiyo wanaohusika na vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini,makanisa na baa.

Akizungumzia tamko hilo la Baraza la Maaskofu Zanzibar, Mkurugenzi wa Makosa ysa Jinai Zanzibar Yussuf Ilembo alisema ni kweli vipeperushi hivyo vimesambazwa, jeshi la polisi linaendelea kufanyia uchunguzi watu wanaotoka vipeperushi hivyo.

Alisema katika kupambana na tatizo hilo wapelelezi bingwa kutoka Marekani(FBI) wameshafika Zanzibar ili kusaidia mpango kazi wa kuwasaka watu wanaofanya vitendo hivyo vya hujuma na kwamba utaalam wao utasaidia upelelezi wa ndani kuweza kulifikia lengo.

CHANZO: NIPASHE

Share: