Habari

MABADILIKO TABIANCHI YAATHIRI PEMBA

KISIWA cha Pemba kinatajwa kuathirika na mabadiliko ya tabianchi ambapo baadhi ya vijijini vimeathirika moja kwa moja na baada ya kuwepo tishio la maji ya bahari kuvamia makazi ya wananchi.

Hali hiyo imewafanya wananchi wa vijiji hivyo kuanza kuchukua hatua ya kupanda miti aina ya mikoko ambayo ni maarufu kwa ajili ya kuzuia nguvu za maji ya bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi, alishiriki katika kampeni za kupanda miti aina ya mikoko katika mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Dadi alishiriki kupanda miti aina ya mikoko ipatayo 50,000 katika vijiji vya Micheweni, Tumbe na Kojani.

Alisema njia pekee ya kukinusuru Kisiwa cha Pemba na mabadiliko ya tabianchi ni kupanda miti ya aina mbalimbali ambayo itazuia nguvu za bahari kuvamia nchi kavu. “Hizi ni juhudi muhimu sana za kupanda miti aina ya mikoko kwa ajili ya kupunguza kasi ya maji ya bahari kuvamia nchi kavu….vijiji vingi vya Pemba vipo katika tishio hilo,” alisema Dadi.

Alisema kazi za kupanda miti itakayozuwia mmomonyoko wa ardhi ni muhimu kwani ndiyo njia pekee ya kuviokoa visiwa vya Pemba. Baadhi ya miji mbalimbali ya kisiwa cha Pemba iliopo karibu na bahari tayari imeanza kupata athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo maji kuvamia sehemu za kilimo na makazi.

Share: