Habari

MABISHANO YAKISHERIA YAANZA KESI YA VIONGOZI WA HARAKATI YA JUMUIYA NA TAASISI ZAKIISLAM ZANZIBAR

DAR-ES-SALAAM.

 

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili  amiri mkuu wa jumuiya ya maimamu zanzibar  samahatu sheikh Faridi Hadi Ahmed (41), na wenzake 9, umedai kuwa Jaji aliyesikiliza maombi ya washtakikwa hao hakuwa na mamlaka hayo kisheria.

Mawakili wa Serikali walieleza katika Mahakama ya Rufaa wakati wa kusikiliza rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar kupinga uamuzi wa Jaji Abraham Mwampashi, katika maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na washtakiwa hao.

Rufaa hiyo namba 96, ya mwaka 2013, ilisikilizwa juzi  jijini Dar es Salaam na jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, linaloongozwa na Jaji Edward Rutakangwa, akisaidiana na Jaji Bernard Luanda na Jaji William Mandia.

Mawakili hao wa serikali wakiongozwa na Fatma Abdallah Hassan kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama kuwa Jaji Mwampashi alikosea kisheria na kiukweli kusikiliza na kuyatolea uamuzi maombi hayo kwa kuwa hakuwa na mamlaka hayo.

Walidai kwamba kifungu cha 3 (1) cha Mahakama Kuu Zanzibar kilichotumika kuwasilisha maombi hayo hakimpi mamlaka ya kuyasikiliza na kuyatolea uamuzi maombi hayo.

Akijibu hoja hizo, wakili wa utetezi, Salum Taufiq alisema kifungu hicho kinatoa mamlaka mapana kwa Mahakama Kuu na kwamba katika uamuzi wake Jaji Mwampashi alieleza sababu za kufanya hivyo ambazo wao waliridhika nazo.

Shehe Faridi na wenzake wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, wakikabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya uchochezi na hujuma za uharibifu wa mali na kusababisha hasara ya Sh milioni 500.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Msellem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azzan Khalid Hamdani, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman na Hassan Bakari Suleiman, Ghalib Hamada Omar, Abdallah Saidi Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.

Hata hivyo Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za rufaa za pande zote pamoja na hoja za pingamizi la awali, iliahirisha shauri hilo hadi siku ya hukumu, ambayo pande zote watajulishwa

 

Tagsslider
Share: