Habari

Mabodi wa CCM atekeleza ahadi yake kwa vikundi 14 vya TASAF Pemba

IMEANDIIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

CHAMA cha Mapinduzi CCM Zanzibar, kimesema kitandelea kutekeleza ahadi zake wanazoziweka kwa wananchi, kwa vile chama hicho ndio kiongozi wa vyama vyengine kidemokrasia, hivyo haitapendeza kutotekeleza ahadi zake.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi fedha zilizoahidiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, kwa vikundi 14 vya shehia ya Kibokoni wilaya ya Chakechake, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Khamis Salum Ali, alisema kama muungwa ni vitendo viongozi wa CCM hilo linawahusu.

Alisema daima CCM kwa vile ni chama kikubwa na kimeshapevuka kidemokrasia, hakuna budi kila wanaloliahidi kutekeleza, kama alivyofanya Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Abdalla Mabodi, wakati alipovitembe vikundi hivyo vinavyowezeshwa na TASAF mwezi uliopita.

Alisema utekelezaji wa ahadi hiyo, unatokana na viongozi wa CCM kuwa na uchu wa maendeleo, pasi na kujali kabila, dini, chama wala eneo wazanzibari na watanzania walipo, bali ni kuona wanaishi katika maisha mazuri.

Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Chakechake, alieleza kuwa hakuna namna kwa alieweka ahadi kuitekeleza, na ndio maana Naibu Katibu mkuu wao, aliwatuma wao kwenda Kibokoni kuitekeleza ahadi aliyoiweka ya msaada wa fedha.

“Leo0 (jana) tumekuja sisi viongozi wa CCM wilaya ya Chakechake, kuja kutekeleza ahadi ya Naibu Katibu Mkuu wetu wa CCM Zanzibar Mhe: Mabodi, aliowaahidi ya kuwapatia fedha wakati alipowatembelea,”alieleza.

Katika hatua nyengine, Katibu wa CCM wilaya ya Chakechake Mafunda Khamis Ali, alisema CCM kinafaa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo, maana chama na viongozi wake ni wapenda maendeleo.

“Wananchi endeleeni kukiunga mkono kwa nguvu zote chama chetu cha CCM, maana viongozi wake wamekuwa na uchu wa maendeleo, kuanzia diwani hadi rais wetu wa Zanzibara na yule ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisisitiza.

Awali Mratibu wa TASAF Pemba, Mussa Said Kisenge, alisema kwa shehia ya Kibokoni pekee kwa kipindi cha miaka mitano, wameshatumia zaidi ya shilingi milioni 260 kwa kuwalipa walengwa 227 waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini.

Fedha hizo zimelipwa na TASAF kwa mizunguruko 31, ambazo hulipwa walengwa hao kila baada ya miezi miwili, kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2018, kwa ajili ya kuhamasisha elimu, afya na lishe.

Aidha Mratibu huyo wa TASAF Pemba, alisema kuwa wameshatumia shilingi milioni 101, kwa walengwa hao kupitia ajira za muda, kwa ile miradi walioiibua wao, na kuitekeleza na kujiunga kwenye ajira za muda mfupi.

“Walengwa wa kaya maskini waliomo kwenye mpango wa TASAF, wameamua kuanzisha vikundi vya kujiendeleza ambavyo ndio hivi leo (jana), vitakavyokabidhiwa msaada wa fedha kwa ajli ya kujiendeleza,”alieleza.

Hata hivyo Mratibu huyo, aliwataka wanavikundi hivyo, kuzitumia vyema fedha hizo, ili kuona wanasonga mbele kimaendeleo na wanaondokana na umaskini ambao, ndio lengo la serikali kupitia Ilani ya CCM kuupunguza.

Walengwa waliokabidhiwa msaada huo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, walisema utakuwa ni mwanzo mzuri wa kuendelea vikundi vyao.

Walisema, wanamshukuru sana kuona, kiongozi anaweka ahadi na kuitekeleza, na wao wamepata faraja na nguvu za kuendeleza shughuli zao za vikundi.

Mmoja kati ya wanufaika wa msaada huo ni Fatma Faki Ali, wa kikundi cha “subira minallah” alisema kwanza ni jambo la faraja kuona kiongozi anatimiza ahadi zake.

“Fedha hizi tulizopewa zitasukuma mbele biashara zetu ndani ya kikundi, chetu maana ilikuwa tumeshaelekea kukwa, lakini kwa kiongozi huyu wa CCM kutumiza ahadi yake ni faraja kwetu,”alifafanua.

Nae Chema Mjaka Juma, alisema waliamua kuanzisha kikundi chao cha ushirika, ili kuongeza nguvu na kutunisha mfuko wao, baada ya kukabidhiwa ruzuku na kila baada ya miezi miwili TASAF.

Shehia ya Kibokoni yenye walengwa 227, waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, kupitia TASAF kwa kukabidhiwa fedha kila baada ya miezi miwili, kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka jana, na wastani wa shilingi milioni 260 wameshalipwa.

MWISHO

PembaToday

Share: