Habari

Mabodi:Hatuna muda kuzungumza na wapinzani

January 22, 2018

NA MWAJUMA JUMA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakina muda tena wa kukutana na wapinzani kuzungumzia masuala ya uchaguzi na kazi iliyo mbele yao ni kupanga maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Mabodi, alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa shirikisho la vyuo vikuu ofisi kuu CCM Kisiwandui.

Alisema wakati ambao kulikuwa na muda wa kufanya hivyo waliwazungusha na kufikia hata kuwahangaisha wazee wao na sasa muda haupo tena na kilichobakia ni kuangalia namna gani wanaweza kukiimarisha chama na kupanga mikakati ya kuwaletea wananchi wao maendeleo.

“Hakuna mazungumzo tena kwa sasa, tukutane 2020 katika uchaguzi, washaona mambo yanakwenda vizuri wanaleta vidudu mtu,” alisema Mabodi.

“Tuliwaita mpaka wazee wetu wakatuzungusha sasa hivi wanataka nini hatuna muda tena,” alisema.

Aliwataka wanaCCM wa shirikisho hilo kujitahidi kuwa mabalozi wazuri katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuingiza wanachama wapya na kuwashaiwishi kwenda kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa wale wote ambao tayari wamefikisha umri wa kupiga kura.

Alisema CCM pamoja na kuwa na wafanyakazi wengi ndani ya ofisi na jumuiya zao lakini bado nguvu za wanachama wa nje zinahitajika ili kukiletea ushindi.

“Kama hatujawatumia wanaCCM waliopo nje ya ofisi zetu hatutofika mbele, lazima tutumie jeshi la wanaCCM hawa kuwaelezea watu ili kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka wanashirikisho hilo kusoma katiba na kanuni za chama na kujenga ushirikiano na viongozi wao katika kujijenga chama na inapotokea matatizo wayatatue kulingana na katiba na kanuni zinavyoelekeza.

Zanzibarleo

Tagsslider
Share: