Habari

Madaktari bingwa wa Hispania waanza kutoa huduma Pemba

IMEANDIKWA NA SHAIBU KIFAYA, PEMBA

TIMU ya madaktariI bingwa kutoka nchini Uhispani wanatarajiwa kuwasili kisiwani Pemba katika hospitali ya Chake chake, kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wananchi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa mishipa kwa wanawake na wanaume, kazi inayotarajia kuanza Machi 2 hadi Machi 12 mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake daktari Atiki Omar Suleiman, anayeshughulika na mambo ya ganzi na usingizi, alisema wanatarajia kupokea madaktar hao 10 kutoka Uhispania wakishirikiana na madaktari wazalendo wa hospitali hiyo.

Alisema lengo la kushirikiana na madaktari wazalendo ni kuweza kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi zaidi, ambapo watakuwepo kwa muda wa wiki mbili.

Alifahamisha kuwa, matibabu yatakayo fanyika hospitalini kwa upande wa akina mama ni Uvimbe katika mayai ya uzazi, Bawasili, Hania pamoja na Mayoma kwa wale ambao watahitajika kufanyiwa upasuaji huo na kwa upande wa akina baba watafanyiwa upasuaji wa mabusha na kesi za ngiri .

Alisema kuwa matibabu hayo kwa kipindi chote cha wiki mbili, watakachokuwepo hospitalini hapo itakuwa ni bure hakuna gharama yoyote ambapo mwananchi atahitaji kuchangia gharama, hivyo ameahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuitumia fursa hiyo.

“Madaktari hao kwa kweli watafanya kazi hiyo kwa muda wa wiki mbili, na matibabu itakuwa ni bure tofauti na kipindi cha nyuma, mtu kuchangia kiasi cha fedha, jambo ambalo ilikuwa ni kikwazo kwa wananchi na kushindwa kumudu gharama,’’alisema.

Hata hivyo alisema katika utoaji wa matibabu atakuwepo daktari bingwa wa magonjwa ya meno na kuwataka wananchi wanaosumbuliwa na matatizo hayo, wafike ili nao waweze kupatiwa matibabu na kupewa dawa pamoja na maelekezo yatakayowasaidia kupunguza kuumwa matatizo ya meno mara kwa mara .

Aidha alisema madaktar hao wamekuwa wakifanya matibabu hospitali ya Chake chake kutokana na ukaribu wa wananchi hao kutokana na mazingira ya Kisiwa cha Pemba kilivyo ili iwe rahisi kwa wananchi wote kupata matibabu.

Mwisho .

PembaToday

Share: