Habari

MAFUTA KUACHIWA WENYEWE WAZANZIBARI

WAKATI mjadala kuhusu Muungano wa Tanzania ukishika kasi, Kamati ya pamoja ya kutatua kero za Muungano huo iliyokuwa inakutana Zanzibar, imeeleza kuwa baadhi ya mambo yamepatiwa ufumbuzi.

Akiyataja mambo hayo Waziri wa nchi ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud alisema miongoni mwa mambo ambayo yamepatiwa ufumbuzi ni mgawanyo wa misaada kutoka nje.

Aidha, Waziri Aboud alisema kero nyingine ambayo imepatiwa ufumbuzi na Kikao hicho, ni pamoja na kupatiwa kwa ajira kwa Wazanzibari ndani ya Taasisi za Muungano.

Mkutano huo wa siku mbili, ni mfululizo wa majadiliano ya kila mara, ulifanyika Hoteli ya ‘Zanzibar Beach Resort’ na kuongozwa na Makamo wa Rais wa Muungano, Dk Mohammed Gharib Bilal.

Viongozi wengine waliyohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri Mkuu, Mhe Mizengo Pinda na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Waziri Aboud ambaye pia anasimamia mambo ya Muungano, alisema licha ya kuwepo na kasoro, bado Muungano ni muhimu kuendelea kutokana na faida zake kuwa nyingi kwa nchi zote mbili.

Aliongeza kusema: Serikali zote mbili zitaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya faida ya kuwepo kwa Muungano huo, ambao unatimiza miaka 49 ifikapo Aprili 26, mwaka huu.

Kuhusu suala la mafuta na gesi asilia, Waziri Aboud alisema Serikali zote mbili zimefikia hatua nzuri ya kuiyondoa rasilimali hiyo katika orodha ya mambo ya Muungano. Waziri Aboud, hakufafanua kwa undani suala la uhusiano wa Zanzibar na nchi za nje.

Baadhi ya Mawazi wa Serikali zote mbili, pamoja na Wakurugenzi wa Idara ambazo zinasimamia masuala ya Muungano yanayolalamikiwa, pia wameshiriki na kutoa ufafanuzi kuhusu namna ya kuziondosha kero hizo.

Wajumbe hao walikutana katika utaratibu wao wa  kawaida, ambapo walipitia kumbukumbu za kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Januari 28, mwaka jana mjini Dar es salaam, pamoja na kupokea taarifa za utekelezaji wa masuala ya Muungano.

Pia, wajumbe hao walipitia na kuridhia mapendekezo kuhusu utaratibu wa muda wa mgao wa ajira kwa Taasisi za Muungano kwa Serikali ya Zanzibar pamoja na kuangalia makubaliano ya kero zilizopatiwa ufumbuzi.

Wakichangia hoja mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo, baadhi ya Wajumbe wameelezea kuridhika kwao na hatua zinazochukuliwa, chini ya usimamizi wa wanasheria wakuu wa pande zote mbili za Muungano.

Walisema ushauri wa Maraisi  wa Serikali zote mbili kuridhia hatua hizo, umewezesha na kuwapa nguvu wanasheria wa pande hizo, kuangalia namna ya kuandaa utaratibu utakaokidhi mahitaji ya sheria ya kuyaondoa mafuta na gesi asili ndani ya mambo ya Muungano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Muungano, Samia Suluhu alisema mwenendo mzima wa utekelezaji wa masuala yanayoleta kero za Muungano unakwenda vyema kufuatia vikao vinavyoendelea.

Waziri Samia alisema hata hivyo yapo baadhi ya masuala  ambayo huchukuwa muda mrefu kupatiwa ufumbuzi kutokana na mfumo wa sheria unaohitaji mabadiliko ili kwenda sambamba na makubaliano yaliyokubaliwa.

Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda akitoa shukrani zake aliipongeza Serikali ya Zanzibar kwa maadhimisho mazuri ya sherehe za Mapinduzi za mwaka huu zilizokuwa za mfano wa aina yake.

Pinda alisema jamii ingependa kuona sherehe za mwakani za kutimia nusu karne, zikawa za mafanikio makubwa zaidi na Serikali ya Muungano, inaandaa fikra ya namna ya kuongeza nguvu za ushiriki na mchango wake katika kufanikisha sherehe hizo.

Naye, Balozi Seif alifahamisha kwamba, wajumbe wa kikao hicho wameweza kupokea na kuridhia masuala mbali mbali waliyoelekezwa na kikao chao kilichopita, na yalikuwa kero katika mambo ya Muungano.

Akikifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Mohamed Gharib Bilal alishauri Viongozi  wa Wizara za  Serikali zote mbili kuendelea kushirikiana ili kuleta ufanisi zaidi.

Dk Bilal alisema ushirikiano huo utashirikisha pia watendaji na wataalamu wa sekta zinazohusika, utasaidia kupunguza na hatimaye kuondosha kabisa  kero zinazosababisha kuleta mitafaruku ndani ya Muungano.

Masuala yaliyowasilisha  katika kikao hicho, kupokewa na kuridhiwa na wajumbe hao, ni pamoja na ruhusa kwa Serikali ya Zanzibar, kukopa nje ya nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa ushuru mara mbili, kodi ya mapato na suala mafuta na gesi asilia, kutaka lisiwemo katika mambo ya Muungano.

Mkutano mwengine wa Kamati hiyo ya ya pamoja ya kutatua kero za Muungano, unatarajiwa kufanyika mara baada ya sherehe za Muungano huo, hapo Aprili 26, mwaka huu..

Share: