Habari

Magari madogo aina ya Cary kupigwa marufuku

Ali Othman Ali

Jeshi la polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limepiga marufuku magari madogo aina ya Cary kufanyakazi ya kubeba abiria kama dalala kutokana na magari hayo kukosa vigezo vya kufanya biashara hiyo na badala yake magari hayo yataruhusiwa kubeba mizigo kama ilivyo kawaida.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Wete tarehe 8 Septemba 2014, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Sheikhan Mohammed Sheikhan amesema dereva yeyote ambae atakwenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Sheikhan amesema, tayari jeshi lake limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba agizo hilo linatekelezwa kwa kuwaandaa askari wa kikosi cha usalama barabarani kusimamia utekelezwaji wa agizo hilo.

Wakati huo huo, Kamanda Sheikhani amesema, Jeshi la polisi Mkoa wa Kaskaini Pemba linamshikilia dereva wa gari dogo aina ya Cary Pius Benedict Lucas (35) kwa kosa la kumshambulia dereva mwenzake Hamad Kombo Ali (28) na kumsababishia maumivu makali.

Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo, Kamanda huyo amesema madereva hao walianza mzozo wakiwa barabarani mzozo ambao uliendelea hadi kituo cha magari Konde ambako walianza kupigana hadi dereva Hamad Kombo Ali kupata maumivu makali sehemu ya puani.Vyanzo vya habari hizi vimedokeza kwamba Bwana Pius alikua amelewa pombe kabla ya tukio hilo.

Hivi karibuni kumekuwepo na kasi ya ongezeko la magari madogo aina ya Cary ambapo yamekuwa yakitumika kwa shughuli za kubeba abiria katika barabara mbalimbali za mkoa wa Kaskaini Pemba. Miongoni mwa barabara zitumiazo magari madogo aina ya Cary kwa kubeba abiria ni barabara inayounganisha maeneo ya Konde – Makangale na Madenjani – Likoni.

Share: