Habari

Magufuli abebeshwa zigo zito la Zanzibar

Rais John Magufuli akizungumza jambo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein katika sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

By Boniface Meena na Fidelis Butahe, Mwananchi
Wednesday, January 13, 2016

Hakuna shaka kwamba mwarobaini wa mgogoro wa Zanzibar kwa kutumia jitihada za ndani, sasa ni Rais John Magufuli baada ya jitihada za viongozi wa kisiasa Zanzibar kukwama, wadau waliozungumza na Mwananchi wameshauri.

Mgogoro wa uchaguzi Zanzibar, imekuwa kawaida kuibuka kila baada ya Uchaguzi Mkuu, na mgogoro wa safari hii uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wote Oktoba 28 na kuahidi kuitisha uchaguzi mwingine ndani ya siku 90.

Lakini kufuatia hatua hiyo ya Jecha, CUF imeipinga ikidai kuwa mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad alishinda na haikubaliki uchaguzi huo kurudiwa.

Tangu wakati huo, Maalim Seif, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo ambayo mapema wiki hii yamedhihirika kuwa hayajazaa muafaka.

Kauli na matukio kadhaa ya hivi karibuni yametoa picha kwamba hakuna maelewano kwenye mazungumzo hayo, huku sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi zikiibua mazito zaidi.

Akizungumzia kukwama kwa mazungumzo huyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema mgogoro wa kisiasa unaoendelea Zanzibar, ulikuwa ni wa Kikwete ambaye amemtwisha Rais Magufuli.

Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alisema kutokana na hali hiyo, Dk Magufuli ndiye anayeshikilia kete ya utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa kuwa ndiye mwenye sauti ya kusema nini kifanyike.

Lissu, ambaye alikuwa akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu, alisema kutokana na jinsi muundo wa Muungano ulivyo, Tanzania Bara ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwenye mgogoro huo.

“Kama Magufuli akisema ZEC watangaze matokeo yatatangazwa mara moja,” alisema Lissu huku akionyesha kusikitishwa na yale yanayoendelea Zanzibar.

Lissu alisema Dk Magufuli amerithi mgogoro mkubwa wa Muungano na kisiasa ambao mataifa ya Magharibi hayapo upande wake.

“Hayakuwahi kuweka msimamo wa wazi wakati wa (Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa na Kikwete, lakini wakati huu yamesema hapana na yameshikilia msimamo,” alisema wakili huyo maarufu nchini.

Rais Magufuli ameshakutana na pande zote kwenye mgogoro huo, akianza na Maalim Seif na baadaye Dk Shein. Juzi, Maalim Seif alimnukuu Balozi Idd akisema baada ya mazungumzo na wawili hao, aliwaambia wafuasi wa CCM kuwa Rais ameagiza pande zote mbili zirudi Zanzibar kukubaliana kurudia uchaguzi, kauli ambayo Maalim Seif aliikana vikali.

Dk Shein ameshaeleza kuwa msimamo wa kurudia uchaguzi wa Zanzibar ni wa chama chake cha CCM na hivyo kuwataka wafuasi wasubiri tarehe itakayotangazwa na ZEC.

Kwa sasa, Rais Magufuli ni mjumbe wa kawaida wa vyombo vya juu vya CCM, ambavyo ni Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, lakini anatarajiwa kuachiwa uenyekiti wakati uchaguzi mkuu wa chama hicho utakapofanyika miaka miwili ijayo, au iwapo Kikwete ataamua kuachia mapema wadhifa huo kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Kauli ya Lissu ya kumtaka Rais kuingilia kati inalingana na wito alioutoa Maalim Seif juzi mjini Dar es Salaam, aliposema ana imani na Dk Magufuli kumaliza tatizo hilo.

Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Magufuli hakuwahi kuwaambia kuwa warudi Zanzibar kukubaliana kurudia uchaguzi, bali wazungumze na kufikia muafaka.

Wito wa kutaka Rais Magufuli aingilie kati mgogoro huo, pia imetolewa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholaus Mgaya akisema heshima ya Dk Magufuli inaweza kusaidia kutatua mgogoro huo.

“Naona Rais Magufuli ana nafasi kubwa ya kumaliza mgogoro Zanzibar kwa sababu ni kiongozi anayeheshimika na pande zote mbili zinazotofautiana,” alisema Maalim Seif.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema Rais anaweza kutatua mgogoro huo, lakini ni iwapo pande zote mbili zitataka aingilie kati.

“Kama wakiendelea hivi kila mtu kushikilia msimamo wake, Rais Magufuli hataweza kutatua,” alisema Bana, ambaye amebobea kwenye sayansi ya siasa. “Wakikaa kwanza na kukubaliana Magufuli awasuluhishe, hapo itakuwa rahisi kuingilia kati na kumaliza mgogoro.”

Dk Bana pia alizungumzia ushiriki wa vyama vingine kwenye mazungumzo hayo: “Wanapaswa kutafakari upya. Nadhani ni wakati wa kushirikisha vyama vingine vilivyoshiriki uchaguzi Zanzibar.”

“Vyama hivi vihusishwe kwenye mazungumzo maana CUF wanaweza kususia uchaguzi, lakini vyama vingine vikashiriki. Wanapaswa kukaa kwa pamoja na kukubaliana kama uchaguzi unarudiwa wote washiriki na kama haurudiwi asiwepo hata mmoja atakayekwenda kinyume,” alisema Dk Bana.

Hadi sasa, pande hizo zimeshafanya vikao vinane ambavyo havijafikia muafaka. Kwa mujibu wa Maalim Seif, CCM wamekuwa wakieleza kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi, lakini hadi sasa wameshindwa kuwasilisha uthibitisho kwenye vikao hivyo.

Kauli za wasomi
Akizungumzia mkwamo huo, Profesa Mwesiga Baregu alisema wanaojadili muafaka wanapaswa kukumbuka machafuko ya kisasa ya mwaka 2001 yaliyosababisha watu kupoteza maisha.

“Mazungumzo yaanze upya kwa kumshirikisha mtu wa tatu. Tunachokiona sasa ni CUF na CCM pekee kukutana. Hawa wanaonekana wameshindwa kufikia muafaka kutokana na kauli wanazozitoa. Tunahitaji uwepo wa watatuzi wa migogoro kutoka nje ya nchi,” alisema Profesa Baregu ambaye amebobea kwenye masuala ya uhusiano wa kimataifa.

“Tanzania imekuwa hodari kwa kutatua matatizo ya nchi jirani…Sasa ni wakati wa kuzishirikisha nchi hizo kumaliza hali ya kisasa inayotishia kuitafuna Zanzibar.” alisema,” alisema Profesa Baregu.

Kuhusu hilo, Dk Bana alisema tatizo la mgogoro wa Zanzibar ni muundo wa Muungano: “Tungekuwa na muundo wa Muungano wa Serikali moja, tusingeona malumbano kama haya yanayotokea Zanzibar”.

Lakini hakukubaliana na hoja ya Profesa Baregu kuwa mataifa ya nje yashiriki kutafuta muafaka: “Matatizo ya Zanzibar yatamalizwa na Wazanzibari wenyewe…Watu wa nje wanaweza kutoa ushauri tu na rasilimali fedha,” alisema Dk Bana.

Alisema ni lazima mazungumzo yafanyike sasa kufikiwa muafaka kwa sababu mgogoro huo una athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alihoji kwani tatizo la Zanzibar ni uchaguzi pekee. “Mpasuko Zanzibar upo muda mrefu na inaonekana hakuna njia muafaka zilizochukuliwa. Je, Zanzibar tatizo ni uchaguzi pekee?” alihoji Mhadhiri huyo.

Alisema hata ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, bado Zanzibar ilikuwa na tatizo kubwa kwa kuwa wanaoshirikishwa katika mazungumzo hayo ni CCM na CUF pekee, wakati jambo hilo linawahusu Wazanzibari wote.

“Mnapotatua migogoro lazima muweke misingi ya makubaliano yenu na lazima mjifunze cha kusema wakati mazungumzo yakiendelea.”

“Si kila mtu kusema lake na kuonekana wazi mnatofautiana…taasisi na mashirika yasiyo ya kiserika nayo yana nafasi kubwa ya kumaliza mkwamo huo wa kisiasa,” alisema Hamad Salim.

Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo naye alionyesha wasiwasi wake juu ya kauli zinazokinzana za viongozi hao. Alisema siku zote migogoro hutatutiliwa katika meza ya mazungumzo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisis ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema kinachoendelea sasa si dalili nzuri kwa amani ya nchi.

“Kauli za viongozi wanaotueleza kuwa wapo katika mazungumzo hazileti matumaini ya amani. Nashauri kuanza upya kwa mazungumzo kwa dhamira ya hali ya juu ya kufikia muafaka,” alisema Profesa Wangwe.

Share: