Habari

Magufuli ajue kuwa: akimuudhi mchinja mbuzi…

Dk Ali Mohamed Shein, akila kiapo cha utii kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman. Hafla ya kuapishwa kwa Dk Shein, ilifanyika mapema mwaka jana 2016.

Mwandishi Maalumu
Jumapili, Januari 15, 2017

WIKI nzima iliyopita, baadhi ya watanzania kupitia kwenye Mitandao ya Kijamii, wemekuwa wakijadili kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli kutokuhudhuria sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

Wapo baadhi wanajiuliza kwa nini hakuuhudhuri na haikuzoeleka kuwa hivyo. Wapo wanaomuunga mkono kulingana na wadhifa wake. Lakini pia, wapo wanaodhani kuwa kutokuhudhuria amekosea kutokana na mazoea tangu kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar.

Hata hivyo, Magufuli mwenyewe binafsi hilo aliliona na kulitolea maelezo na sababu. Haijulikana kwamba sababu alizozitoa ni za kweli au ametunga tu. Watu wazamani walinena: ‘msema pweke hakosi.’

ALIVYONUKULIWA
Rais John Magufuli, ameeleza sababu zilizomfanya asihudhurie sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika uwanja wa Amani, siku ya Alhamisi, tarehe 12 mwezi huu.

Amesema serikali imejiwekea utaratibu wa kuadhimisha sikukuu za kitaifa ziwe zinaadhimishwa kwa  pande zote za  Muungano wa nchi hizo, yaani Zanzibar na Tanganyika. 

Akizungumza katika mkutnao wa hadhara akiwa Shinyanga, Magufuli alisema  katika utaratibu mpya waliyojipangia ni kuwa, si viongozi wote watakwenda eneo moja la maadhimisho:

“Sote tunawajibika kwa nchi moja ya Tanzania, chochote kitakachofanywa upande mmoja wa Muungano, hakuna budi upande mwengine kuonesha mshikamano.”

Kwenye uwanja wa Amani, Zanzibar yalikofanyika maadhimisho ya sherehe hizo, viongozi kadhaa wakiwamo ma-rais wastaafu, walihudhuria. Magufuli, alikuwa pamoja na Waziri wa Vikosi vya Ulinzi wa SMZ, Haji Omar Kheir katika mkutano wake wa hadhara, Mkoani Shinyanga. MWISHO WA KUNUKUU
  
NYERERE:
Inakaribia kuwa miaka 18 tangu kufariki kwa Julius Nyerere, ambaye alikuwa Rais wa TANU chama kilichoongoza Tanganyika baada ya kupata uhuru wake kutoka kwa Muingereza, Desemba 9, 1961.

Miaka mitatu baadaye, Aprili 26, 1964 Nyerere na Karume (Abeid Amani), walikubaliana kuunda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania). Ndiyo Muungano huu ulipo hadi sasa. Uliojaa utata na mashaka. Hii ilikuwa ni hatua ya haraka sana lakini, iliyoridhiwa na viongozi hao kwa wakati huo.

Kuna siku niliwahi kumsikia Nyerere katika hotuba yake kwamba, alipotoa wazo la kuunganisha nchi zao (Tanganyika na Zanzibar). Anasema, Karume hakuwa na pingamizi. Alitaka muungano huo ufanywe siku hiyo hiyo, hapo hapo.

Nyerere anasema kuwa: “Karume alinambia kuwa tuungane sasa hivi, na mimi (Nyerere) ndiyo niwe Rais na yeye (Karume) atakuwa Makamu wa Rais.”

Sijui kama kauli hii ina ukweli au ndiyo ule msemo: ‘msema pweke hakosi.’ Kauli hii aliitoa baada ya Karume kuuawa. Ingawa ndivyo ilivyokuwa, Nyerere Rais na Karume, Makamu wa Rais kwa muda wote.

Nyerere anasema kwamba, Karume alitaka Muungano wa Serikali Moja. Lakini, anasema, alihofia kuonekana kuwa nchi kubwa kuimeza nchi ndogo na ndipo alipotoa wazo kwamba Zanzibar, ibakie na serikali yake.

Katika hotuba yake, Nyerere anafafanua: “Tuliunganisha baadhi ya mambo na ndiyo maana Tanzania ina muundo wa Muungano wa Serikali mbili…kwenda moja.’

Hapa, nilivyomuelewa Nyerere, ni kwamba Zanzibar ina serikali yake kwa kufanya shughuli zake za ndani ya Zanzibar tu. Muda ukifika inaweza kufutwa na kuwa na serikali moja.

Kwa hivyo, baadhi ya watu wanahisi kuwa Magufuli, kutokuhudhuria Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, yuko ‘wrong’, amewapa viongozi wenzake wa Serikali na CCM, picha mbaya.

Kutoka Shinyanga hadi Zanzibar, kwa ak’ali ni mwendo wa saa moja na nusu. Ni masafa ya kwenda na kurudi na hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya wenzake tangu enzi za Nyerere.

Kwa kauli ya kistaarabu, ni kana kwamba kawaona viongozi waliyomtangulia kuanzia Nyerere hadi Kikwete, kuhudhuria sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, walikuwa wapuuzi wala haikuwa sahihi. Hiyo ndiyo maana yake, hata kama wenyewe wamekaa kimya.

Katika kikao kimoja cha Baraza la Wawakilishi lilipokuwa katika muundo wa ‘Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wakati wa kujadili ujio wa uundwaji wa katiba mpya na uhalali wa Muungano wa Tanzania, nilimsikia Abubakar Khamis Bakari (Waziri wa Sheria wa SUK), anasema:

“Kitu chochote kikizoeleka kwa miaka mingi, kuwepo kwake ni kama kipo kisheria.” Hapa alikuwa anafafanua swali lililouzwa kuhusu uhalali wa Mungano, ambao mikataba yake haionekani na iliyopo inatiliwa wasi wasi kuwa ni mikataba ya kughushi ili kuwaziba watu macho na akili. 

Magufuli anasema kuwa serikali imejiwekea utaratibu wa kuadhimisha sikukuu za kitaifa, ziwe zinaadhimishwa pande zote mbili za Muungano. Kauli hii ya Magufuli, pia inatiliwa shaka.

Kwa nini imetolewa siku yenyewe ya sherehe. Swali: Makubaliano haya yamefikiwa lini?. Au ndiyo ule msemo: ‘msema pweke hakosi.’ Tutaona ukweli wake siku zijazo: ‘njia ya muongo ni fupi.’

Baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii, wamekuwa na maoni tofauti kwa Magufuli kutokuhudhuria, kitendo ambacho hakikuwahi kutokea kwa Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Mimi nahisi kuna tatizo?.

Kuna mtu mmoja kazungumzia kuhusu itifaki na kupigiwa mizinga. Magufuli hofu yake kuingia mwanzo uwanjani, kumpokea Shein, kama mkuu wa nchi ya Zanzibar, na Shein kuondoka uwanjani, akaachwa yeye aondoke baadaye kama itifaki inavyoelekeza.

Baadhi ya watu wanasema hizo ni baadhi ya sababu zilizomfanya kufutuka kutokuhudhuria sherehe hizo kwa sababu zinamdhalilisha. Magufuli, anaona GHERA (fedheha) kutangulia ndani ya uwanja kumpokea mjumbe wa Baraza lake la Mawaziri katika serikali yake. Kwa Magufuli, imemwia vigumu.

Hapa ndipo tunapata maana halisi ya ule msemo wa wahenga: ‘ukimuudhi mchinja mbuzi utakosa mchuzi’: Magufuli, nadhani usemi huu umempitia mbali au kausahau.

Watangulizi wake wote, kuanzia Nyerere na waliyofuata baadaye siyo kwamba walikuwa wanahudhuria sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kwa hiari au kuwa walikuwa wanapenda, hapana…isipokuwa walikuwa wanajilazimisha kufanya hivyo, ili kumridhisha mchinja mbuzi.

Hofu kubwa waliyokuwa nayo ni kuogopa kuwakera viongozi wa Zanzibar, ndiyo maana ma-Rais wa Muungano na wastaafu wamekuwa wakihudhuria sherehe za Mapanduzi, kila mwaka.

Lengo ni kuwafurahisha, kuwahadaa na kuwaziba macho viongozi wa Zanzibar, ili wasishtuke wasikasirike, wabaki wapofu wa akili na macho.

Washindwe kupata mawazo mapya na fikra kuweza kuamua kuungana pamoja na Wazanzibari wengine kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili na kuachana na ukoloni mweusi wa Tanganyika.

Mkoloni Tanganyika, kila kukicha anapandikiza chuki na kupalilia fitina za kuwagawa Wazanzibari washindwe kutambua heshima na raha ya kujitawala bila kuingiliwa na mtu au taifa jingine.

Mkoloni Tanganyika, hapendi kuwaona wazanzibari wameshikamana pamoja,  nguvu moja wanaendesha wenyewe nchi yao: Wahenga wanasema: ‘vita vya panzi neema ya kunguu.’

Mkoloni Tanganyika, anajuwa kuwa umoja ni nguvu. Anajuwa kuwa Wazanzibari wakiwa wamoja wakishikamana, atakuwa hana tena nafasi. Kwa ufupi, kutawaliwa ni utumwa na mtawala ananufaika zaidi kuliko watawaliwa.

Kutokuelewana miongoni mwa Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe kuhusu nchi yao kuwa na mamlaka kamili ndiyo neema ya mkoloni Tanganyika, aliyevaa koti la Muungano, hata kama anajidhalilisha kila inapofika Januari 12, siku ya kumbukumbu ya Mapinduzi.

Ni vigumu kwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri, aliyeapishwa na (Rais wa Muungano na Amiri Jeshi Mkuu), lakini kwa siku moja ndani ya mwaka anakuwa mkuu wa nchi, mkoloni mwenyewe akawa dhalili na thakili, kukubali kudogoshwa. Inataka moyo na ujasiri.

Kwa mimi naona hiyo ni shani kubwa, siku zote yeye anakuwa mdogo tena Mjumbe wa Baraza la Mawaziri, lakini kila tarehe 12 Januari, anakuwa yeye ndiye mkubwa na mkoloni anaridhia…hiyo ni shani kubwa haijawahi kutokea popote duniani, isipokuwa Unguja, Tanzania.

Lakini, Mkoloni enegefanya nini wakati anaonekana dhahiri kuwa ndiye mwenye kuuhitaji Muungano, maana kama hauhitaji engekuwa ameachana nao kitambo, hasa ikizingatiwa kuwa ana nchi kubwa inayotoa Zanzibar (Unguja na Pemba) zaidi ya laki moja au lukuki. Kuing’ang’ania Zanzibar, taba’an kunampa maslahi.  

Kwa lugha nyingine, tunaweza kusema Magufuli, kakataa kumpaka Shein mafuta kwa nje ya chupa huku, akijuwa kuwa Zanzibar si nchi na huo ndiyo msimamo wa Mkoloni Tanganyika. Mizengo Pinda, alizidi kupigilia msumari ndani ya bunge lao, Dodoma.

Sipati picha na ni mageni kutokea; Najaribu kujiuliza kwa nini Magufuli hakwenda Zanzibar, badala yake kenda Shinyanga. ‘Anadanganya toto’ anajidai kusema ati anavunja miiko ili kutanua wigo mpana, sherehe ziwe za kitaifa zaidi.

Tukiangalia mahudhurio ya viongozi wastaafu kule Zanzibar, tunapata shida kidogo, kwani ile ilikuwa fursa adhimu iliyowakutanisha ma-raisi wote wastaafu wa Muungano na Zanzibar.

‘Technically’ anastahili kabisa kutokwenda. Ni fedheha na aibu Mkoloni Mkuu wa Muungano na Amiri Jeshi Mkuu awepo halafu aonekane yuko chini ya Mjumbe wa Baraza lake la Mawaziri, aliyemwapisha, ni vioja na fedheha.

‘Protocol’ haikubali kabisa ‘Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Mkoloni’ (Rais wa Zanzibar), aingie uwanjani baada ya MKOLONI kuingia na kuketi. Halafu, Mjumbe wa Baraza la Mawaziri aje, akague gwaride, apigiwe mizinga mbele ya bosi wake…ahutubie umma aondoke, mkoloni abakie ndani ya uwanja. mhh hatari!.

Magufuli, hawezi kurudia kufanya kosa alilolifanya mwaka jana, kuhudhuria sherehe za miaka 52, za Janauari 12, 2016. Nadhani, alijifunza akaona haiko sawa, safari hii hakutaka kurudia kosa.

Ametafuta kisingizio cha Shinyanga, kama udhuru asihudhurie kukwepa aibu inayofanywa na watangulizi wake kwa kuogopa ‘kumkera mchinja mbuzi.’ Magufuli katafuna jongoo kwa meno, kasema potelea mbali, liwalo naliwe, sihudhurii ng’oo.

Nakumbuka, Sherehe za Mapinduzi za kutimia miaka 20 za mwaka 1984 Nyerere, alipangiwa kufungua kiwanda cha kusindika makonyo ya karafuu Wawi, Chake Chake.

Uzinduzi huo ulifanyika asubuhi na baadaye Nyerere, alihudhuria kilele cha sherehe hizo zilizofanyika jioni, uwanja wa Amani, Unguja. Kama kawaida utaratibu wa sherehe hizo ni ule ule kila mwaka.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa Aboud Jumbe Mwinyi, ambaye anakuwa wa mwisho kuingia ndani ya uwanja ki-‘protocol’.

Nyerere pamoja na ujanja wake wote, lakini katika sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, alisalimu amri, miaka yote alikuwa akiingia uwanjani kabla ya Rais wa Zanzibar, na akiondoka baada ya kumsindikiza Rais wa Zanzibar. Jambo ambalo sidhani kuwa lilikuwa likimfurahisha, ingawa aliridhia na kuonekana kuwa mtiifu.

Utaraibu wa miaka ya nyuma Nyerere, alikuwa anapewa nafasi ya kusalimia kutoa salaam za Watanganyika. Mpango huo kwa sasa sidhani kuwa unaendelea.

Sherehe za miaka 20 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ndizo za mwisho kuonekana hadharani Aboud Jumbe ambaye baada ya sherehe hizo, alijiuzulu katika machinjio ya viongozi, Dodoma.

Sherehe hizi, zilitanguliwa na kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar, hali iliyosababisha viongozi wengi wana Mapinduzi (MBM wa 1964) kwenda na maji hadi baadhi yao kufungwa vifungo vya nyumbani..

Nakumbuka katika mkutano mmoja wa hadhara uliyohutubiwa na Nyerere, uliyofanyika Tibirinzi, Chake Chake ambao madhumuni ilikuwa kuelezea dhambi za Aboud Jumbe, kuhusu Muungano.

Ni mkutano huo, aliotoa hadithi ya shoka na mti na kueleza kuwa shoka tupu bila ya mti (mpini) haliwezi kuwa adui wa mti.  Akifafanua kuwa mti utakuwa salama endapo shoka litakosa mpini. 

Mkutano huu wa hadhara wa Tibairinzi, ulifanyika miezi michache baada ya serikali ya awamu ya tatu ya Zanzibar, kuanza kazi, Rais Ali Hassan Mwinyi na Waziri Kiongozi, Maalim Seif Sharif Hamad.

Fumbo hili la Nyerere, niligundua kuwa watu wengi hawakulifahamu maana yake. Siku ya mkutano huo nilikuwapo. Nilijuwa kuwa Nyerere, kuna watu wamewapiga kijembe.

Tafsiri ya chap chapu ya fumbo la Nyerere, ni kuwa yeye ni shoka, lakini yeye  (Nyerere kama shoka) peke yake asingeweza kumuondoa Rais wa Zanzibar madarakani bila kushirikiana na watu kutoka Zanzibar, kama ndiyo miti (ndugu zake Jumbe).

Kadhalika, katika mkutano huo Nyerere alisema kwamba: “Aboud kanitumia ujumbe wa kunizuia kushudhuria sherehe hizi kutokana na hali ya usalama kuwa hairidhishi…lakini nimemwambia nitahudhuria.” Na kweli alihudhuria..

Tagsslider
Share: