Habari

Magufuli atakiwa kupasua ” BUSHA ” la Zanzibar

Kwa ufupi

Wakizungumza jana katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) kujadili changamoto za kisheria zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25 mwaka 2015, wanasheria hao walisema Rais Magufuli anaweza kutumia nafasi yake kumaliza sintofahamu hiyo.

By Peter Elias, Mwananchi

Dar es Salaam. Wanasheria nchini wamemtaka Rais John Magufuli atumbue jipu la Zanzibar kwa sababu sintofahamu inayoendelea kutokea visiwani humo ni aibu ya Tanzania mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Wakizungumza jana katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) kujadili changamoto za kisheria zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25 mwaka 2015, wanasheria hao walisema Rais Magufuli anaweza kutumia nafasi yake kumaliza sintofahamu hiyo.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kumekiuka Katiba na sheria mbalimbali za uchaguzi zinazosimamia uchaguzi.

“Ingawa haya yanatokea Zanzibar, lakini ni suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamtaka Rais Magufuli katika kutumbua majipu alione na hili la Zanzibar tunataka alipasue kabisa.”

Aliongeza kuwa, “kuendelea kutembea nalo linakuwa mzigo mkubwa, kwa hiyo tunamtaka kulipasua ili kutua hilo zigo.”

Othman alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi.

Alisema hata vifungu alivyovitumia Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha wakati anatangaza kufuta uchaguzi, vinazungumzia mambo mengine kabisa.

“Ni vema Rais Shein (Ali Mohamed) akajiuzulu kwa sababu yeye ni sehemu ya tatizo la Zanzibar. Hawezi kuendelea kugombea wakati yeye ndiye aliyesababisha mkwamo huo wa kisiasa,” alisema mwanasheria huyo.

Wakili Fatma Karume ambaye pia ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema kuna haja ya kubadilisha kifungu cha 119 (10) kinachotaja sifa za mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi kwamba anatakiwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu au mtu yoyote mwenye kuheshimika.

“Ni jambo la kushangaza kabisa, yaani Jecha anapewa uenyekiti wa Tume wakati hajui mambo ya kisheria halafu makamu wake ndiyo jaji. Hapa kuna tatizo na amewekwa hapo kwa ajili ya kulinda maslahi ya watu,” alidai wakili huyo.

Fatma alisema hakushangazwa na kitendo cha wanasheria kushindwa kwenda mahakamani kufungua kesi ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi kwa sababu anajua hawana imani na mahakama. Alisema yule aliyemteua Jecha (Rais Shein) ndiye aliyewateua pia majaji.

Mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa alisema Jecha ni kada wa CCM, hivyo hafai kuongoza Tume hiyo kwa sababu anaonyesha maslahi yake wazi wazi kwa chama hicho.

“Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Jecha aligombea katika jimbo la Amani kupitia CCM akashindwa. Shein akaona amteue kuwa mwenyekiti wa ZEC ili kulinda maslahi yake.”

Jecha alitangaza kufuta uchaguzi huo wa rais, wawakilishi na madiwani visiwani humo akisema kanuni na taratibu zilikiukwa.

Uchaguzi huo kwa sasa umepangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.     
CHANZO: MWANANCHI

Tagsslider
Share: