Habari

Mahakama kuamua pingamizi la Uamsho

Na James Magai, Mwananchi
Jumatano, Decemba 10 2014

Dar es Salaam. Hatima ya usikilizwaji wa maombi ya marejeo ya viongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), inatarajiwa kujulikana leo, wakati Mahakama Kuu Dar es Salaam itakapotoa uamuzi wa pingamizi la awali la Jamhuri dhidi ya maombi hayo.

Washtakiwa hao walifungua maombi hayo Mahakama Kuu, Dar es Salaam Oktoba 13, 2014, kupitia kwa jopo la mawakili wanaowatetea, pamoja na mambo mengine wakiomba mahakama hiyo iwafutie mashtaka ya ugaidi yanayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo, mjibu maombi (Jamhuri) iliweka pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo, ikiomba maombi hiyo kuyatupilia mbali kwa madai kuwa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ina dosari za kisheria na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza maombi hayo.

Jaji Dk Fauz Twaib alipanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo leo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote juma lililopita, yaani hoja za pingamizi kutoka kwa Jamhuri na majibu ya hoja hizo za pingamizi kutoka kwa watoa maombi.

Ikiwa Jaji Twaib atakubaliana na hoja za pingamizi hilo la Serikali, basi maombi hayo yatatupiliwa mbali na hivyo washtakiwa hao kuendelea na mashtaka hayo, au watalazimika kuchukua hatua nyingine kadri Mahakama itakavyoelekeza katika uamuzi wake.

Pia, kama Mahakama itatupilia mbali hoja za Serikali za pingamizi lake basi itaendelea na usikilizwaji wa maombi ya msingi na hatimaye kutoa uamuzi wa kuyakubali au kuyakataa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), Jamal Noorid Swalehe, Nassoro Hamad Abdallah, Hassan Bakari Suleiman, Anthari Humoud Ahmed, Mohamed Isihaka Yussuph na Abdallah Hassan Hassan.

Wengine ni Hussein Mohamed Ally, Juma Sadala Juma, Said Kassim Ally, Hamis Amour Salum, Abubakar Abdallah Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Othuman Amir, Rashid Ally Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Salum Nassoro, Said Shehe Sharif na Mselem Ali Mselem.

Katika maombi yao, pamoja na mambo mengine wanaiomba mahakama hiyo itupilie mbali hati ya mashtaka waliyofunguliwa, wakidai kuwa imefunguliwa bila ya ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwamba hati hiyo haielezi makosa ya ugaidi wanayotuhumiwa.

Tagsslider
Share: