Habari

Mahakama Kuu ya Tanzania..’si bure na mkono wa mtu’

Al Nofli
Jumatatu, Februari 25, 2019

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ‘si bure kuna mkono wa mtu.’ Mahakama ya ngazi yoyote ndani ya nchi ni kimbilio la wananchi katika kutafuta haki zao.

Mahakama Kuu ya Tanzania imeanza kuonekana kituko na wananchi wanaopeleka mashauri yao wameanza kuigwaya na matarajio yao ya kupata haki yameanza kufifia na kupotea.

Kwa ufupi, Mahakama Kuu ya Tanzania inatia kichefuchefu kutokana na kuanza kupoteza muelekeo wake na kuyumba katika utowaji haki kwa muda unaotarajiwa. Muda mwafaka.

Haiyumkini kuwa kesi moja ya kutafsiri sheria inachukua miaka mitatu bila kutolewa hukumu au kuahirishwa mara kwa mara bila sababu za msingi.

Kila ikipangwa kutolewa huku kunatolewa visingizio na sababu za kipuuzi ili kupoteza muda. Kwa mataifa yaliyoendelea muda ni muhimu sana. Dakika 5 kuzipoteza ni gharama kubwa. Mahakama Kuu ya Tanzania hawalioni hilo.

Muhimili wa mahakama hasa mahakama kuu au mahakama ya rufaa ndiyo kimbilio la kuaminika kutafuta haki sasa umeanza kutiliwa mashaka na unatia kichefuchefu. Si bure kuna mikono ya watu kwa maslahi yao binafsi.

Kesi ya mgogoro wa uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) imeshindwa kutolewa hukumu na badala yake hata kusomwa huku inapigwa danadana.

Imepelekwa mbele hadi Jumapili ya Machi 17, 2019 siku ambayo kwa utaratibu wa kiutumishi wa Tanzania si siku ya kazi. Yaani ni jambo la aibu sana linalochafua taswira nzima ya muhimili wa mahakama.

Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa Ijumaa ya Februari 22, 2019 na Jaji Benhajj Masoud (Doctor) aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.

Kuahirishwa kwa hukumu hiyo kulitangazwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Sharmillah Sarwatt.

Akiahirisha hukumu hiyo Naibu Msajili huyo, alisema Jaji Masoud ambaye alitarajiwa kuisoma anakabiliwa na majukumu mengine.

“Hivyo nina ahirisha usomaji wa hukumu hii hadi Machi 17 mwaka huu,” alisema Naibu Msajili Sarwatt akitaja tarehe hiyo. Hata hivyo, tarehe hiyo itakuwa ni siku ya Jumapili siku ambayo hakuna shughuli za kimahakama.

Kuahirishwa kusomwa hukumu hiyo na siku iliyopangwa kusomwa kuangukia kuwa siku ya Jumapili ni baadhi ya maswali yanayohojiwa na watu wengi na hasa viongozi wa CUF na wafuasi wao, walifungua kesi hiyo.

Profesa Lipumba ambaye Agosti 5, 2015 aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo lakini, Juni 5, 2016 aliandika barua nyingine ya kutengua barua yake ya kujiuzulu na kutangaza kurejea rasmi katika wadhifa wake huo huku, bila kufuata utaratibu wa kurudi kwake.

Kesi hii dhidi ya Profesa Lipumba, kwa mara ya kwanza ilikuwa imepangwa kutolewa hukumu Oktoba 30, 2018 ikaelezwa kuwa hukumu haijawa tayari, kwa maana bado haijakamilika.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Januari 15, 2019 ikajitokeza hoja, upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeomba kupewa muda kujibu hoja.

Jaji Dk Benhajj Masoud ilipanga kutoa hukumu Ijumaa wiki iliyopita , Februari 22, 2019 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Sharmillah Sarwatt alipoeleza kuwa pasina kuwepo Jaji mhusika kuwa hukumu hiyo haitasomwa.

Akaongeza: “Jaji kapangiwa majukumu mengine na imepangwa kutolewa hukumu Machi 17, 2019” Hapa ndiyo kuna ukakasi Jumapili, ni siku ambayo ni mapumziko ya mwisho wa wiki.

Baada Sarwatt kueleza hayo baadhi ya watu waliohudhuri mahakamani hapo walishtuka kwamba tarehe 17 Machi itakuwa siku ya Jumapili.

Baadhi ya watu walianza kusema hapo hapo mahakamani kuwa hili si bure isipokuwa kuna kitu kinachotengenezwa dhidi ya hukumu iliyokwisha taarishwa na Jaji Dk Benhajj Masoud.

Narudi nyuma kidogo katika kesi iliyofunguliwa na Ally Saleh (Mbunge wa Mjimkongwe), aliyeomba mahakama itamke ni ipi bodi halali kati ya bodi mbili, Bodi ya Wadhamini CUF Lipumba au Bodi ya Wadhamini CUF Taasisis? Katika hukumu naweza kusema kuwa Jaji Benhajj Masoud chupuchupu ajichanganye.

Hukumu iliyotolewa, ilionekana kana kwamba hukumu iko ‘draw’ yaani hakuna mshindi. Kawaida ya hukumu za kimahakama zinapotolewa ni kushinda kesi na kushindwa.

Narudia, katika kesi hakuna ‘draw’ ya hukumu ndiyo sababu ikaruhusiwa kukata rufaa kama ikitokea upande mmoja haukuridhika au kukubali matokeo. Hukumu ni mmoja tu kushinda au kushindwa.

Kwa hukumu ile ya kesi ya Ally Salehe, ndiyo sababu CUF Lipumba, wakadai kuwa hakuna mshindi. Kitu ambacho siyo sahihi. Nilivyomsoma Jaji, alitaka kujichanganya.

Wanasheria pekee hasa wale wa upande wa mlalamikaji ndiyo waliyoifahamu hukumu iliyotolewa na Jaji Masoud. Baadhi ya watu waliona kuna utata.

Sasa tuangalie mfano wa mahakama zinazojiamini

Jaji Mkuu David Maraga wa Mahakama ya Juu nchini Kenya, hadi sasa ameweka rekodi inayoendelea kutikisa Barani Afrika na Dunia.

Jaji Maraga akiwa pamoja na jopo la majaji wengine sita, kujiridhisha juu ya matokeo ya uchaguzi ya urais, yalioyafutwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ulifanyika Agosti 8, 2017.

Matokeo hayo yalibatilishwa baada ya Mahakama ya Juu kujiridhisha kuwa uchaguzi huo ulivurugwa.

Uamuzi huo wa mahakama uliandika historia ya kipekee kwa nchi za Afrika na hata Dunia. Namaanisha kwa mataifa ya magharibi ambayo yalipongeza hatua ya mahakama ya juu ya Kenya..

Jaji Maraga, alikuwa amesimama pamoja na majaji wengine kadhaa waliojiridhisha pasina shaka kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), haikuwajibika ipasavyo.

Katika tangazo lake la kubatilisha matokeo hayo, Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga aliamuru uchaguzi mpya wa urais ufanyike ndani ya siku 60.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilighadhibika na uamuzi huo. Haikutarajia kama mambo yangeenda kombo.

Ilidhani hoja zilizoletwa na kambi ya akina Raila Odinga zingepuzwa (zingetupwa) kama ilivyowahi kutokea katika chaguzi za nyuma.

Kama alivyonukuliwa wakati huo, Rais Kenyatta alikiri kuvunjwa moyo lakini akasema hana njia nyingine mbali ya kurejea tena kwenye kampeni.

Alisema amekubali kutekeleza uamuzi wa mahakama lakini alihifadhi jambo fulani moyoni. Kwa lugha nyingine alikubali kurejea katika uchaguzi huo kwa ‘shingo upande.’

Kwa muhtasari Mahakama za Tanzania hasa mahakama kuu, umefika wakati wa kujitafakari katika utendaji kazi wake ili kuweza kuwa wa viwango na kuaminika, siyo kukubali watu wengine kuingiza mikono yao kuharibu taswira ya mahakama.

Mahakama ni muhimili unaopaswa kuhakikisha unatenda haki sawasawa kwa daraja zote za watu, taasisi na vyama vya siasa bila kuwa na upendeleo, woga, hofu na majaji kuwa tayari kukabiliana na vitisho kutoka katika mamlaka nyingine.

Chambilicho Wapemba na msemo wao wa ‘kinyaka msewe’: Kesi ya Bodi ya Wadhamini wa CUF Taasisi, iliyosongzwa mbele, naibu msajili wa mahakama kuu, kasema itasomwa tarehe 17 Machi ambayo ni siku ya Jumapili. Hapo ndiyo kuna ‘kinyaka msewe.’

Ni aibu kuwa mahakama kuu ya Tanzania, hata kalenda haina. Watumishi wa serikali siku hizi wanaangalia kalenda kupitia simu za mikononi. Watumishi wa mahakama za Tanzania basi, hata simu hawana?..

Share: