Habari

Makala : Hali ya Matumbawe Zanzibar

December 14, 2018 – by Manager

Imeandikwa na Salmin Juma ,Zanzibar

salminjsalmin@gmail.com

Tel : +255772997018

MATUMBAWE ni maliasili zinazopatikana baharini na kuna mahusiano makubwa kati ya maisha ya viumbe vya majini na matumbawe

Maliasili hii hutegemewa sana na nchi mbalimbali kwa shughuli za uzalishaji unaosaidia kuongeza pato la taifa.

Kimsingi, mamilioni ya viumbe viishivyo baharini hutegemea matumbawe ili kuzaliwa na kukua vizuri na hatimae binadamu kunufaika navyo , samaki ambao ni chakula maarufu duniani kote, ni miongoni mwa viumbe hivyo.

Inafahamika kuwa miamba ya matumbawe ni mojawapo ya vitu vya kuvutia katika maumbile ya dunia.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanafikiri kuwa matumbawe ni aina ya mawe, lakini sio ukweli kwani huo ni mkusanyiko wa wanyama wadogo sana wanoitwa ‘polipu’ (polyps), ambao wana kiunzi cha mfupa mgumu kwa nje mithili ya jiwe.

Polipu ambao wamehusiana na jejeta (mdudu wa bahari wa yavuyavu) na anemone, wana mikia yenye kuchoma wanayoitumia kwa kulia (plankitoni).

Kitaalamu, mwamba wa matumbawe unafanyika kutokana na matumbawe yenyewe kama ilivyoelezewa huko juu kuwa ni wanyama wadogo wadogo walio wengi na wanaoishi pamoja na idadi yao ni kubwa, aghlabu hufikia hata maelfu au mamilioni.

Wanyama hawa hukaa pamoja muda mrefu na wana uwezo wa kuzalisha jasi ambalo baadae hujitengeneza kuwa jiwe na ndilo linaloitwa matumbawe.

Aina nyingi za matumbawe huota vyema mahali ambapo joto la bahari ni kuanzia nyuzi joto 23- 29 na hayawezi kuishi katika maji yaliyo na joto la chini ya nyuzi joto 18.

Pia yanahitaji maji safi yasiyochafuka ambayo yanapata mwangaza mwingi wa jua na yenye mkusanyiko wa chumvi asilimia 3-4. Mahitaji haya maalum yanamaanisha kuwa aina nyingi sana za matumbawe na miamba hupatikana katika bahari za nchi za joto kwenye kina cha mita 30-50.

Dk. Mohammed Suleiman Mohammed, ni mkufunzi kutoka Idara ya Sayansi Asilia na mratibu katika kituo cha utafiti wa bahari, mazingira na rasilimali za asili chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Mkufunzi huyo anaelezea mgawanyiko wa matumbawe kisayansi kuwa yamegawika katika aina nyingi zinazoweza kufikia hata 300.

“Kwa kawaida tunaweza kuyagawa kwa mujibu wa yanavyoota, kuna matumbawe yanayo tambaa, kuna yanayoota kwa kutoa matawi na mengine huota mithili ya jabali kubwa, na uoto huu hutegemeana ni wapi yalipoota,” alisema Dk. Mohammed.

Anaendelea kufahamisha kuwa, katika aina zote hizo za matumbawe, mepesi yao ni yale yanayoota kwa matawi ambayo kwa kawaida ni mepesi sana kuvunjika.

Kutokana na wepesi wake, amewanasihi wananchi na wavuvi kuchukua tahadhari kubwa wanapokuwa kwenye shughuli zao ili kuhakikisha aina zote hizo zinabaki salama.

Tafiti mbalimbali za sayansi ya bahari zinaonesha kuwa, asilimia 25 ya uhai wa viumbe vya baharini hutegemea matumbawe kwani ni sehemu salama kwa mazalia, makuzi, makaazi, malezi na malisho kwa baadhi ya viumbe vya baharini wakiwamo samaki.

Matumbawe yanakisiwa kuwa ni asilimia 0.1 ya bahari yote duniani. Zanzibar imebarikiwa kuwa na maliasili hii na miaka mingi sana imefaidika na viumbe hivi. Lakini katika miaka ya karibuni, kumejitokeza uharibifu mkubwa na umekuwa ukiendelea kila uchao.

Mtalaamu wa utafiti wa baharini, mazingira na rasilimali za asili Zanzibar Dk. Mohammed anasema, visiwa vya Unguja na Pemba vimeajaaliwa maliasili hiyo kwa upande wa mashariki na magharibi yake.

Anafahamisha kuwa, mtu hawezi kuzungumzia matumbawe katika nchi ya Zanzibar bila kutaja kisiwa cha Misali kwani ndipo yanapopatikana kwa wingi sana.

“Upande wa mashariki kuna mwamba mkubwa wa matumbawe, kuanzia kaskazini ya visiwa hadi kusini, lakini matumbawe ya upande wa mashariki hayajaota sana ikilinganishwa na magharibi,” alieleza mtaalamu huyo.

Ameongeza kuwa hali hiyo inasababishwa na nguvu za maji ya bahari kuwa ni kubwa.

Viumbe matumbawe hutoa mchango mkubwa kwa maisha ya watu hasa wanaoishi pembezoni mwa bahari.

“Matumbawe yana umuhimu mkubwa sana kwa sababu sehemu zenye uoto wa matumbawe kuna mazalia ya samaki, hizo ni nyumba zao,” anabainisha Dk. Mohammed.

Zanzibar inategemea sana shughuli za uvuvi kuendeshea maisha, na uvuvi unaofanywa mara nyingi ni katika miamba ya matumbawe.

Ndio, kwa sababu matumbawe yako karibu sana na juu, ikizingatiwa kwamba wengi wa wavuvi wa visiwani hawana uwezo wa kwenda mbali ya bahari kutokana na udhaifu wa vyombo vyao.

“Kwa asilimia kubwa uvuvi wa hapa hufanyika katika sehemu za matumbawe. Leo hii kama yataondoka basi upatikanaji wa samaki utakuwa mashakani, wavuvi watapoteza ajira na wananchi watakuwa hasarani,” alieleza Dk. Mohammed.

Kwa mujibu wa Dk. Mohammed, bado matumbawe baharini yanaendelea kuharibiwa ingawa si kwa kiwango kikubwa, hasa kutokana na uvuvi usiozingatia kanuni zilizowekwa.

Alifahamisha kuwa, matumizi ya nyavu katika miamba ya matumbawe ni miongoni mwa mambo yanayoharibu mazingira ya bahari kwa sababu viumbe hivyo ni laini sana na ni lazima yavunjike yanapotiwa nyavu.

Kwa muktadha huo, pia alisema sekta ya utalii itaathirika na hakuna mgeni atakaekwenda kutazama samaki na wanyama wengi wanaoishi katika miamba ya matumbawe, kwani watakuwa wamepotea, kwa maana ya ‘biodiversity’.

Sambamba na hilo, alifahamisha kuwa, matumbawe yanazikinga fukwe zisimong’onyoke kwa sababu ukali wa mawimbi ukifika katika miamba hupungua nguvu.

Kwa namna hiyo, alisema fukwe zitanusurika kutokana na mmong’onyoko wa ardhi, na kinyume chake ni mtihani katika maisha.

Tafiti zilizofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa kushirikiana na wataalamu wa viumbe vya baharini, zimegundua kuwa sababu nyengine inayopelekea viumbe matumbawe kuvunjika ni utupaji wa nanga ovyo habarini.

“Wapo wavuvi wanaotupa nanga za vyombo pasi na kuzingatia eneo wanalotupa kama yapo matumbawe au la. Wakati mwengine hupelekea kuyauwa. Aidha wapo wanaowapeleka watalii katika visiwa tofauti, na pasi na uelewa, hudondosha nanga na kuyavunja matumbawe,” alifafanua mtaalamu huyo.

Hakika mwamba wa Matumbawe una faida kubwa sana katika maisha, mfano kuna aina (spishi) zipatazo 845 za matumbawe yanayojenga miamba duniani kote.

Matumbawe haya huwapatia makazi maelfu ya samaki wa miamba, halikadhalika chaza, kombe, kaa, kamba koche, spongi na mwani.

Miamba ya Zanzibar ni makazi ya mamia ya spishi za samaki wa miamba ya mawe. Samaki hutoa asilimia 60 ya protini ya wanyama inayoliwa Zanzibar, na kwa hivyo samaki ni chanzo muhimu cha chakula cha visiwa hivi.

Wengi wa samaki hawa wanalazimika kuishi sehemu ya maisha yao katika miamba ya matumbawe.

Sura na rangi tofauti zinazopendeza za miamba ya matumbawe na samaki wa matumbawe ni kivutio kizuri sana kwa watalii kuja Zanzibar kuzamia kwa kutumia gesi na kupiga mbizi.

Wavuvi na kila mwenye kuitumia bahari katika harakati zake za kimaisha hakuna budi kuwa makini, kujiepusha na uharibifu wa viumbe hivyo kwani hasara yake ni kubwa katika maisha ya binadamu.

Asilimia 25 ya Wazanzibari hupata ajira kutegemea sekta ya uvuvi na ndio wanaotajwa kuwa ni wahusika wakuu kwa kuyaharibu mazingira ya bahari ikiwamo kuyauwa matumbwe.

Lakini wapo baadhi ya wavuvi wanayatunza kwa sababu wanajua umuhimu wake.

Omar Haji Faki ni mvuvi kutoka Malindi mjini Unguja, anasema samaki wanapokua katika matumbawe wanaona raha na huendelea kubakia sehemu hiyo kwa kuwa hapo ndipo ilipo nyumba yao, lakini yakiondoka hawawezi kubakia.

“Samaki huona raha hasa wakiwa katika matumbawe, wala hawaondoki lakini yakiwa hayapo hawawezi,” alisema Faki.

Nae Ussi Suleiman Makame, mvuvi kutoka bandari ya Kizingo anasema, matumbawe ni sehemu salama ambayo samaki wanapata kupumzika.

Aliongeza kuwa, kutokuwepo kwa matumbawe kutawafanya wavuvi waende maeneo ya mbali kutafuta samaki na huko hakuna uhakika wa kuwapata.

Wakati huo huo, wametoa wito kwa wenzao waache kabisa kuvua kwa kutumia nyavu ndogo zinazokata matumbawe, sambamba na kupata taaluma ya bahari kabla ya kuanza kazi ya uvuvi.

Ukiachilia mbali uvuvi, lakini pia kuna baadhi wa wananchi hasa wasafiri (wa meli, boti, jahazi n.k.) huchafua mazingira baharini kwa kumwaga maji machafu, takataka zisizooza kama vile chupa za plastiki, mifuko, nepi za watoto, na vinywaji vya kemikali ambavyo husababisha kuathiri viumbe vya baharini hasa matumbawe.

Faifa za viumbe hazimithiliki kwa maisha yetu, kwani pia ni kivutio kikubwa cha watalii ambao hutoka nchi mbalimbali duniani kama vile Italia, Ujerumani, Ufaransa, Uchina, Korea na kwengineko kuja kuitembelea Zanzibar ili kushuhudia neema hii.

Watalii hao huja kujionea uzuri wa kipekee wa visiwa hivi na mandhari yake ya baharini, na kuongeza fedha za kigeni katika mfuko wa serikali ambazo ni muhimu kwa kukuza uchumi.

Micholl Grange ambaye ni mzamiaji mwelekezi kutoka kituo cha One Ocean, anaeleza kuwa wanayajali sana matumbwe kwa vile wanafahamu umuhimu wake.

Anasema kabla ya kumruhusu mgeni kuzamia, kwanza humuelekeza kuwa asiguse kitu chochote zaidi ya kuangalia tu.

Pia huwaelekeza wageni, aina gani za mafuta wanayoweza kutumia kwa kujipaka wanapozamia, maana mafuta mengine wanayotumia watu huwa na kemikali mbaya ambayo ni tatizo kwa viumbe vya baharini.

“Tunawafahamisha mapema, kuna mafuta wasijipake wala sabuni nyengine wasitumie maana wakizamia, kemikali hizo zitakwenda kuathiri bahari na viumbe vitaharibika. Tunafanya haya kwa kuwa tunayapenda mazingira,” alisema Grange.

Ikiwa wageni kutoka nje wanatambua na kuthamini umuhimu wa maliasili hii, iweje wazawa wawe ndio wa kwanza kuyaharibu, lazima mamlaka zichukue hatua madhubuti kuzuia jambo hili.

Matukio mbalimbali ya wavuvi kukamatwa wakivua uvuvi haramu kwa vyavu ndogondogo zenye kuharibu mazingira ya bahari ikiwemo kuyakata matumbawe, yamewahi kushuhudiwa kote Unguja na Pemba.

Suala la kujiuliza, ni nani atakuwa mtetezi wa viumbe hivi vinavyofaidisha mamilioni ya watu?

Ukiachilia Zanzibar, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kuna uharibifu mkubwa unaoendelea wa maliasili hiyo duniani kote.

Takwimu zinaonesha kuwa, tayari asilimia 11 ya matumbawe imeshaathiriwa na wataalamu wanasema, iwapo hakutakuwa na uhifadhi mzuri, asilimia nyengine 30 za matumbawe yataangamia kuanzia miaka 20 hadi 40 ijayo.

Sambamba na hilo, utafiti uliofanywa mwaka 2011 uliopewa jina la Reefs at Risk, umeonesha asilimia 75 ya matumbawe duniani yanaathiriwa na shughuli za wanadamu pamoja na athari za kimaumbile.

Katika sababu za kimaumbile zinazotajwa kuchangia uharibifu wa maliasili hii, ni pamoja na ongezeko kubwa la joto na kiwango cha acid ambacho hakijawahi kutokea kwa miaka laki nne (400,000) iliyopita.

Shughuli za kibinadamu nazo zinatajwa kuwa zinachangia kuhatarisha uhai wa matumbawe kwa asilimia 60 kote duniani.

Uvuvi haramu na usiozingatia viwango umeathiri zaidi ya asilimia 55.

Kwa kuwa bado wapo wanaoendeleza uharibifu wa viumbe hivyo muhimu duniani, Serikali ya Mapindizi Zanzibar imekuja na mikakati madhubuti ya kulinda na kuhifadhi rasilimali hiyo.

Mkuu wa doria kutoka Idara ya maendeleo ya uvuvi Zanzibar Haji Shomari, anasema serikali imeshaanza kutoa elimu ya kina inayofahamisha nini matumbawe, thamani yake pamoja na athari zake pindi yatakapotoweka.

“Makongamano yanafanyika wakishirikishwa wavuvi ili kuwapa elimu kuhusiana na mambo yanayoweza kuharibu matumbawe endapo yanafanyika,” alifahamisha.

Shomari alisema, idara pia imeandaa programu za kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na watumiaji wa bahari katika maeneo tofauti kwa lengo la kwenda kuona namna bora ya kuvitunza viumbe hivyo.

Akitolea mfano alisema idara inashirikiana na wawekezeji kwenye visiwa kama vile Chumbe na Mnemba ili kuhakikisha wanayalinda matumbawe kwa kutumia njia sahihi.

Mfano wa njia hizo ni kuweka maboya yanayoashiria kuwa maeneo hayo hayaruhusiwi kupita vyombo vya baharini.

“Pia kikosi cha KMKM ni mdau wetu mkubwa ambae hutusaidia sana kulinda bahari na hasa wavuvi wasiozingatia kanuni za uvuvi bora,” alisema.

Ni ukweli usiofichika kwamba matumbawe yako hatarini kutoweka.

Asilimia 95 ya matumbawe yaliyopo kusini mashariki mwa bahari ya bara la Asia yako hatarini, huku asilimia 75 katika bahari ya Atlantiki inayojumuisha nchi 20 na vinga vyake nayo yakikabiliwa na hatari kama hiyo.

Aidha asilimia 65 katika bahari ya Hindi na Mashariki ya kati na karibu asilimia 50 katika eneo la bahari ya Pasifiki, huku Australia ikionesha kiwango kidogo cha asilimia 14.

Kwa mantiki hiyo wataalamu wa sayansi ya bahari wanakadiria ifikipo mwaka 2050 zaidi ya asilimia 90 ya matumbawe duniani yatakufa na kwa sasa dunia tayari imeshapoteza nusu ya msitu wake wa baharini yaaani matumbawe.

Matumbawe ni muhimu sana lakini pia ni rahisi kuvunjika na yanaweza kuharibika kwa urahisi kwa hiyo ni lazima tufanye kila tuwezalo na tushirikiane kuyalinda na kuyahifadhi.

Waogeleaji, wapiga mbizi na watumiaji gesi chini ya bahari wawe waangalifu wasiguse matumbawe na katu wasisimame juu ya miamba.

Ni muhimu kukaa mbali na matumbawe, na kuwa na tahadhari nz usiyapige mateke au kuvuruga mchanga.

Waendeshaji mashua na ngarawa wakae kwenye maji ya kina kirefu, na sio, kwenye miamba ya maji haba, na watie nanga kwenye mchanga au watumie boya lililotulia kuweka alama ya wapi wafunge au kuweka nanga.

Wavuvi lazima waepuke au waache kutumia njia za uvuvi zinazoharibu miamba ya matumbawe, iwapo yataharibiwa samaki watatoweka.

Tuyalinde, tuyatunze na tuyaenzi matumbawe kwa faida ya viumbe vya baharini na maisha ya mwanadamu, uzuri wetu, asili yetu tusiipoteze. Kitunze kilicho chako.

PembaToday

Share: