Habari

Makala: Watembeza watalii waonesha hofu yao juu ya utafiti wa mafuta Jozani

IMEANDIKWA NA JUMA JUMA-Zanzibar

HAJI Ali Makame (42) anapakia abiria wake wanane, kuelekea mbuga ya taifa ya Jozani, iliopo kusini kwa kisiwa cha Unguja, kwa ajili ya utalii.

Abiria hawa ni wazungu kutoka Italia-wanakwenda kwenye mbuga hii kuangalia Kima Punju.

Kazi ya kutembeza watalii imemfanya Haji kujenga nyumba ya vyumba vinne na kusomesha watoto wake wawili katika skuli ya kulipia. Kazi hii anaifanya kwa miaka 12 sasa.

Lakini ana wasi wasi kwamba, huenda shughuli hii asiifanye tena katika kipindi cha miaka mitatu au minne ijayo, kama msitu wa Jozani utakuwa moja ya maeneo yatakayogunduliwa mafuta, kwa sababu utalii unaweza kuathirika pakubwa.

“Hatujui kitakachotokea kesho, lakini nafikiri sitakuja tena kuleta watalii hapa kama mafuta yatagunduliwa,” anasema.

Mbuga ya Jozani ni moja ya maeneo yaliyolengwa katika utafiti wa mafuta, uliofanywa na kampuni ya RAK GAS inayomilikiwa utawala wa kifalme wa Ras al Khaimah. Mbuga hii inatembelewa na watalii wasiopungua 50,000 kwa mwaka, wengi wakija kuangalia Kima Punju, mnyama wa jamii ya Kima anaepatikana Zanzibar pekee.

“Kila mwezi nakuja kwenye mbuga hii mara tatu, mapato yangu yanawategemea watalii wanaokuja kuangalia Kiama,”anasema Haji.

Hofu ya Haji ni uharibifu wa mazingira unaoweza kutokea katika mbuga hii iwapo uchimbaji wa mafuta utafanywa. Uharibifu huo unaweza kuwakimbiza Kima ambao ndio kivutio cha watalii wanaotembelea msitu huu.

Kwa mwaka 2018, watalii waliotembelea mbuga hii walichangia zaidi ya shilingi 1.06 bilioni. Fedha hizi zilitumika kwa shughuli za maendeleo, ikiwemo kusaidia wanavijiji wanaoishi kando ya msitu.

Hofu ya uharibifu hii haiko kwa Haji pekee. Wahida Juma Msanifu (44), mjumbe wa Umoja wa Wakulima Wenyemashamba Jozani (UWEMAJO), anafikiria kwamba shughuli za uchimbaji mafuta zinaweza kusababisha uharibifu katika mbuga hii ambayo kwake ni tegemeo kubwa.

“Tutaathirika kwa sababu hatutakuwa na nafasi tena kama hii tuliyonayo, ila tuko tayari kupokea mabadiliko. Lolote litakaloamuliwa tutakubali kwa sababu maendeleo ndio tunayohitaji,” anasema Wahida wakati akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili.

Kati ya shilingi milioni 559.03 zilizokusanywa kuanzia Julai-Disemba 2018, UWEMAJO ilipata shilingi 100.6 milioni sawa na asilimia 18.8.

“Fedha hizi tunalipwa kama fidia kutokana na mazao yetu kuliwa na Kima. Zinatusaidia kufanya shughuli nyengine za maendeleo, hatuna hakika kama zitapatikana kama hakuna watalii watakaokuja kuangalia Kima,” anasema.

Katibu wa UWEMAJO, Rajab Omar Khatib (Mchumi), anasema ili kukabilia na uharibifu wa msitu wa Jozani, wanawapatia mafunzo ya kuanzisha kilimo cha kisasa wanachama wake.

“Msitu wa Jozani umeharibiwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu na ukosefu wa ajira. Wananchi wengi wanatumia misitu kwa ukataji kuni, mkaa na miti ya kujengea. Tuna hofu sekta ya mafuta na gesi inaweza kusababisha athari mbaya zaidi,” anasema.

Anasema joto limeongeza kwa 32c na kwamba mafuta ndio chanzo kikuu kinachosababisha joto, hivyo,mikakati madhubuti inahitajika kuhimili athari zinazoweza kusababishwa na mafuta hasa kwenye msitu huu,” anasema.

Hata hivyo, anaunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia sekta ya mafuta.

“Jozani ni sehemu kuu ya kivutio cha utalii na kipato cha wananchi, lakini hatuwezi kuzuia maendeleo yanayofanywa, hata hivyo, tunaamini serikali inaweza kuchukua hatua kudhibiti uharibifu utakaotokea. Tunataka mafuta yapatikane na mazingira yalindwe,” anasema.

Mmoja ya wakaazi wa kijiji cha Jozani, Haji Shaaban, ana hofu sawa na ya Wahida na Khatib.

“Msitu wa Jozani ni muhimu sio kwa Kima Punju lakini pia kwa wakaazi wa vijiji tisa wanaoishi kando ya msitu, nina hofu tunaweza kukosa chakula na maji kama hatua za kudhibiti uharibifu zitachelewa kuchukuliwa,” anasema.

Awesu anasema uharibifu wa mazingira katika nchi zinazochimba mafuta uko wazi akitolea mfano Angola na Nigeria.

“Ni vigumu kuepuka tatizo hili, lakini tunapaswa kuchukua tahadhari ili kulinda mazingira yetu hasa misitu ambayo ni tegemeo kwa sekta ya utalii,” anasema.

Uchunguzi umebaini, hekta 65 za msitu wa Jozani ziliharibiwa kunzia 2013-2015, kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji.

“Wasi wasi wangu kama shughuli za uchimbaji mafuta zitafanywa, uharibifu unaweza kuongezeka mara nne,”anasema.

Mtafiti Fatma Juma katika utafiti wake, ‘Forest fire in Zanzibar; a case of Jazani Chwaka Bay National Park’, anasema uharibifu wa msitu huu umesababisha athari kwa maliasili zilizomo ndani yake.

Katika mahojiano na gazeti hili, Fatma anasema, uchimbaji wa mafuta na gesi unaweza kuwa mwimba mkali kwa misitu mengi, ikiwemo mbuga ya Jozani.

“Cha kufanya kwa kampuni za mafuta ni kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, lakini kuzuia athari zake ni vigumu,”anasema.

Hafidh Maulid Ali, mjumbe wa kamati ya ulinzi wa msitu wa Jozani, anasema uharibifu wa mbuga unafanywa kila kukicha licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali na asasi za kiraia lakini ana wasi wasi kama uchimbaji wa mafuta utafanywa, athari zitakazojitokeza itakuwa shida kuzizuia.

Hata hivyo, Meneja wa RAK GAS Zanzibar, Moamen Madkour, anasema kampuni yao inajidhatiti kupunguza athari za uharibifu mazingira,hata hivyo, anakiri kwamba ni vigumu kuzuia uharibifu moja kwa moja.

“Tunataka kufanya kazi hii bila kuathiri mazingira lakini wakati mwengine ni vigumu kuzuia moja kwa moja hata hivyo,tutapunguza kwa asilimia kubwa,” anasema.

Mkurugenzi idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka, Soud Mohammed Juma, anakiri kwamba msitu wa Jozani unakabiliwa na chanagamoto kubwa ya uharibifu na hofu yake uharibifu unaweza kuwa mkubwa siku za usoni kama hatua hazitachukuliwa mapema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Utafiti wa Mafuta na Gesi Zanzibar, Omar Zubeir Ismail, anasema mamlaka inachukua kila hatua kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo kuandaa miongozo itakayosaidia kuepusha uharibifu wa mazingira,” alisema.

“Tunashuhudia baadhi ya nchi jirani jinsi zinavyokumbwa na majanga ya kimazingira, hali inasababisha kukwama kwa juhudi za upatikanaji wa maendeleo,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Mitawi, anatoa wito kwa taasisi zinazosimamia sekta ya mafuta na gesi, kuandaa mkakati ambao utasaidia kupunguza athari za mazingira.

“Kuna umuhimu kwa taasisi zinazoshungulikia rasimali hizi kuchukua hatua kupunguza athari za uharibifu mazingira yakiwemo ya bahari,” anasema.

“Tuangalie uzoefu wa nchi nyengine zenye rasilamali hizi, ili kuhakikisha mazingira yetu hayaathiriki,” alisema.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mazingira kutoka nchi 10 za Afrika, Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Juma Makungu Juma, alisema serikali itakabiliana na athari zinazotokana na mafuta.

“Uchimbaji mafuta unahitaji taaluma ili usilete athari kwa jamii, hivyo mafunzo haya yataongeza uelewa na kujua jinsi ya kutekeleza mradi huo kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Sheha Mjaja Juma, alisema athari zozote za mazingira zinaweza kuathiri shughuli nyengine za kiuchumi.

PembaToday

Share: