Habari

Maoni ya Wawakilishi mbele ya Jaji Warioba

Salma Said, Zanzibar

BARAZA la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) limeundwa kutokana na vyama viwili vikuu vya siasa hapa Zanzibar ambavyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) lenye wajumbe wapatao 81. Baraza ambalo kwa miaka kadhaa tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 wajumbe wake walikuwa wakikinzana kutokana na misimamo yake ya vivyama lakini hali hiyo ilianza kubadilika baada ya kufanyika mazungumzo ya vyama hivyo na kukubaliana kuunda kwa serikali ya mfumo wa umoja wa kitaifa hapa Zanzibar.

Baraza la Wawakilishi ni miongoni mwa vyombo vinavyoheshimika kwa wananchi kwa kuwa ni mhimili mkuu katika nchi, hivyo baraza hilo kama ilivyo taasisi zingine za kiserikali na kibinafsi na makundi maalumu nchini kupitia Kamati yake ya Uongozi wa Baraza hilo imewasilisha maoni yake mbele ya Tume ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.

Wakiwa mbele ya Tume hiyo wajumbe waliochaguliwa kuwasilisha maoni hayo ambao wameongozwa na Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho na wajumbe wenzake akiwemo Abubakar Khamis Bakari, Mgeni Hassan Juma, Hamza Hassan Juma, na Yahya Khamis Hamad.

Pamoja na mambo mengine waligusia mambo kadhaa ambayo wangependa yazingatiwe katika uandikwaji wa katiba mpya pamoja na kutaka maoni ya wananchi waliotoa yafanyiwe kazi ipasavyo na tume hiyo ambayo imeleta matumiani makubwa kwa wananchi kwamba itatenda haki katika uandikwaji wa katiba mpya.

Wawakilishi hao wa wananchi wa Zanzibar mnamo Jumanne, Februari 5, 2013 waliyataja bila kigugumizi mambo ambayo kwa maoni yao walitaka yazingatiwe zaidi ni pamoja na Usawa wa Ushirikishwaji katika Mamlaka ya Muungano, Misingi ya Muungano na Utaifa na Mgawanyo wa Mamlaka za Muungano.

Mambo mengine walisema Mfumo wa Kutunga Sera na Sheria za Muungano,
Umiliki wa Rasilimali za Muungano, Kuwa na Muungano wa Dhati na wametaka Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Hayo ndio mambo ambayo kwa mtazamo wa watunga sheria hao wameona kuna haja na kutiliwa mkazo wakati wa kutunga katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotarajiwa kumalizika mwaka wa 2014.

Spika Kificho aliwaambia wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Baraza la Wakilishi limekuwa linafuatilia kwa makini sana utoaji wa maoni ya wananchi mmoja mmoja na vikundi kuhusiana na Katiba inayohitajika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini baada ya kutafakari, katika kikao cha Wajumbe wote na katika vikao mbali mbali vya Kamati yake ya Uongozi, imeona pia kamati yake ya uongozi iwasilishe maoni kama baraza kutokana na hali halisi ya maoni yanayotolewa na Wazanzibari.

“Ni ufanisi mkubwa unaopatikana, Baraza la Wawakilishi linaamini kuwa maoni yaliyotolewa tayari yameweka wazi yale mambo muhimu ambayo wananchi wanapenda yazingatiwe katika kupata Katiba mpya,” alisema Spika Kificho.

Spika Kificho aliongeza kwa kusema kwamba “na kwa kuzingatia pia kuwa, katika hatua iliyopo sasa ya maoni ya wananchi ambapo hayajawekewa mwelekeo wake rasmi ni vigumu sana kwa Wajumbe wa Baraza kufikia makubaliano ya maoni ya Baraza kikamilifu (detailed opinion) hata kwa yale mambo ambayo kwa ujumla wake Wajumbe wa Baraza wanakubaliana kwa pamoja”.

Alisema pamoja na yote hayo lakini Wajumbe wa Baraza wameeonyesha mwelekeo wao wa kijumla juu ya mambo wanayoamini kuwa yanahitajika kuingia kwenye Katiba mpya ya Jamhuri nya Muungano wa Tanzania yakiwemo yale mambo ya msingi ambayo Wajumbe wa Baraza kwa ujumla wameyaona yanafaa.

Hata hivyo, Spika Kificho alisema Baraza lake linaamini kuwa suala la namna ambavyo Katiba mpya ya Tanzania inapaswa iwe litajitokeza wazi wazi zaidi katika maoni ya wananchi. Aidha kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, kama Taasisi ya kuwawakilisha wananchi, linajitayarisha kusimamia zaidi juu ya mambo ya msingi ambayo Wazanzibari na Watanzania walio wengi wameonyesha umuhimu wa kuingizwa kwenye Katiba ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Baraza la Wawakilishi lenyewe limeangalia baadhi ya mambo ambayo linahisi ni muhimu ambayo kama Wazanzibari wangependa yawe ni misingi muhimu ya kikatiba katika Katiba ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:

Misingi ya Muungano na Utaifa
“Kwa sababu Wazanzibari ni waumini wa Muungano haukuondoa na hautaondoa uwepo wa Zanzibar kama nchi, ni vyema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ijayo iweke wazi kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano inayotokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,” alisema Kificho.

Na alisema kwamba hali hiyo itahakikisha kuwepo na maeneo maalum ya mamlaka ambayo Zanzibar ina uwezo nayo kama nchi (yaani, Mamlaka ya Dola ya Zanzibar).

Mgawanyo wa Mamlaka za Muungano
Kwa sababu inapendekezwa kuwepo na Mamlaka ya Zanzibar huru na Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Jamhuri ya Muungano, Mamlaka ya Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake.

Usawa wa Ushirikishwaji katika Mamlaka ya Muungano
Aidha alisema uwepo wa Muungano uonekane katika hali zote – uundwaji wa Mamlaka za Muungano, ufanyaji kazi katika Mamlaka za Muungano, ufanyaji wa maamuzi katika Mamlaka za Muungano na uingizwaji na upunguzwaji katika orodha wa mambo ya Muungano hayo yote yazingatiwe kikamilifu.

Akitoa mfano Spika Kificho, alisema maamrisho kama yale yaliyopo sasa kwenye Ibara ya 64(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, ambayo yanawezesha jambo kufanywa la Muungano bila ya kuishirikisha katika maamuzi Mamlaka ya Zanzibar, yasiwe na nafasi tena ya kutokea kwa mujibu wa Katiba ijayo ya Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema katika ushirikishwaji, Katiba itamke wazi kuwa uwepo uwiano ulio wazi wa viongozi na watendaji katika utumishi wa Mamlaka za Muungano. Huku akitoa mfano mbele ya wajumbe wa tume hiyo,kwamba endapo Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, Makamo wa Rais atoke upande mwengine huku Mamlaka ya viongozi wakuu wa Muungano yawekwe bayana ndani ya Katiba.

Lakini pia Spika Kificho akasisitiza uwepo utaratibu wa ubadilishaji nafasi hizo kwa pande mbili za Muungano, yaani, upande unaotoa Rais kwa kipindi fulani, uje kutoa Makamo wa Rais kwa kipindi kingine, na kadhalika.

Mfumo wa Kutunga Sera na Sheria za Muungano
Utungaji wa sera na sheria za Muungano isiwe ni jambo la kuzingatiwa na kutekelezwa na Mamlaka za Muungano pekee na pia uwepo ushirikishwaji wa sehemu (Dola) mbili huru katika kufanya maamuzi na uendeshaji wa Mamlaka ya Muungano.

Spika Kificho ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) alisema ushirikishwaji huo ni lazima udhihirike katika maamuzi yatakayopelekea kuundwa kwa sera na sheria zote za mambo ya Muungano.

Umiliki wa Rasilimali za Muungano
Katika suala la rasilimali za taifa Spika Kificho alisema Kamati yake ya Uongozi imeona kuna haja ya rasilimali za Muungano iwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilimali hizo ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano.

Pia ugawaji wa rasilimali ufanywe kwa uwiano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano huku Kamati hiyo ya uongozi ikisema neno rasilimali katika maudhui hayo linajumuisha pia miundombinu inayojengwa kutokana na rasilimali za Muungano.

Kuwa na Muungano wa dhati
Kamati hiyo ya Uongozi wa Baraza la Wawakilishi haikuwacha kugusia suala ambalo limekuwa likitajwa sana na kupigiwa kelele mara nyingi kuhusiana na suala la Muungano wa dhati ambapo walisema jambo kubwa zaidi ya yote linalohitajika lionekane kwa maneno (maamrisho ya Katiba) na vitendo ni haja ya kuwa na Muungano wa kweli na uwepo kimaandishi.

“Hata kama ni kwa maeneo machache, kwa dhati ya wanasiasa na Watanzania kwa jumla. Hali inaweza kupatikana kwa kuzingatia misingi ya Katiba iliyoainishwa hapo juu ambayo yanaweka mkazo juu ya haki na maslahi ya pande mbili za Muungano ya kujiamulia hatma za mambo yao yote, ya kiuchumi, ya kijamii na ya kisiasa,” alisisitiza Kificho.

Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
Katika suala la muundo unahitajika katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati hiyo ya Uongozi ilisema “Baraza la Wawakilishi halikufikia maamuzi maalum katika mtazamo wa Baraza kama taasisi, Muungano wa Tanzania unaweza kuchugua muundo wowote kwa kuzingatia misingi ya Katiba iliyoelezewa hapo juu”.

Kila jambo lenye lenye mwanzo basi huwa lazima liwe na ukomo wake kwa maana ya hitimisho na hivyo Kamati ya Uongozi wa Baraza hilo chini ya wajumbe wake, walihitimisha maoni yao kwa kusema “ni imani ya Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, kuwa misingi ya Katiba ambayo imeelezewa hapa kwa ufupi sana ni muhimu sana katika kujenga Jamhuri ya Muungano iliyo imara na yenye kuonyesha dhamira halisi ya kuwepo na Muungano endelevu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Tagsslider
Share: