Habari

Mapapasi wasio na vitambulisho kukamatwa

October 1, 2018

NA TATU MAKAME

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, limesema, linaendelea na operesheni ya kuwaondosha watembeza watalii (mapapasi) wasio na vibali kutoka Kamisheni ya Utalii ili kulinda usalama wa watalii na mali zao.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Haji Abdalla Haji, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.

Alisema opereshen ya kuwaondosha watembeza watalii ambao hawana vibali itafanyika fukwe zote za kitalii zilizomo katika mkoa huo.

Aliyataja maeneo ambayo yanaendelea kufanywa zoezi hilo kuwa ni Nungwi na Matemwe na baadae Kiwengwa.

Alisema zoezi hilo linafanyika kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wamiliki wa hoteli ya kuwepo vijana wanaofanya kazi ya kutembeza watalii bila ya kuwa na vitambulisho.

“Tunaendelea na zoezi hili kwani wapo wageni ambao wamejeruhiwa na kuibiwa, hivyo kila anaefanya kazi ya kutembeza watalii lazima awe na kitambulisho,” aliongeza.

Alisema vijana hao pia ni kero kwa wageni kwani huwalazimisha kuwatembeza ingawa hawana vibali kutoka mamlaka husika.

Akizungumzia uingiaji wa wageni kiholela, alisema wanatakiwa kutumia njia zinazotambulika ili kuweza kuishi ndani ya shehia wanazotaka kwa amani.

Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa wageni katika shehia zao ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Zanzibarleo

Share: