Habari

Maradhi yasiyopewa kipaumbele yapewa msaada wa gari Zanzibar

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo akipokea funguo za gari kutoka kwa mwakilishi wa SCI la Uingereza, Dk Khalfan Abdallah Mohamed.

Na Makame Mshenga – Maelezo Zanzibar

Posted Alhamisi, Julai 2, 2015

Shirika la Shistosomiasis Control Initiative (SCI) la Uingereza, limetoa msaada wa gari mbili aina ya Toyota Double Cabin kwa Wizara ya Afya Zanzibar kupitia kitengo chake cha maradhi yasiyopewa umuhimu (NTD).

Mwakilishi wa Shirika hilo, Dk Khalfan Abdallah Mohamed akikabidhi gari hizo jana, alisema lengo la msaada huo ni kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua katika mapambano yake na maradhi yanawaandama watu wengi.

Maradhi yanayohusika kwa matumizi ya msaada huo ni pamoja na matende, minyoo na kichocho ambayo ni vigumu kupata misaada ya matibabu kutoka kwa wafadhili wa jumuiya za kimataifa.

“Ni rahisi sana kuomba msaada wa maradhi kama UKIMWI kwa vile yanapewa kipaumbela na wafadhili lakini maradhi mengine kama minyoo au matende ni vigumu sana kuwashawishi wafadhili na kuweza kusaidia” alisema Dk Khalfan wa SCI.

Alisema gari hizo ni kwa ajili ya kazi za kitengo cha maradhi yasiyopewa umuhimu na kwamba zitatumika zaidi katika zoezi la ulishaji wa dawa kwa wagonjwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo alilishukuru SCI kwa mashirikiano ya muda mrefu na Wizara ya Afya, kupitia kitengo cha NTD kinachoendesha zoezi la ulishaji dawa maskulini na katika jamii kwa ujumla.

Aidha, alitowa wito kwa mashirika mengine ya maendeleo kuunga mkono jitihada za Wizara ya Afya Zanzibar katika kupambana na maradhi mbalimbali ambayo yanadhoofisha afya za wananchi wa Wazanzibari.

Waziri Mahmoud amezipokea gari kwa niaba ya wizara yake na kuliahidi Shirika la SCI kuzitunza ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Gari hizo mbili, moja itatumika Unguja, na moja itatumika Pemba kwa lengo hilohilo la kusaidia mapambano ya kuondoa maradhi yasiyopewa umuhimu..

Imetolewa na Maelezo Zanzibar

Share: