Habari

Mashahidi kesi ya ubakaji Kiungoni Pemba hawaridhishwi na maamuzi ya Mahkama

October 1, 2018 – by Manager

Imeandikwa na Zuhra Juma na Salmin Juma , Pemba

MASHAHIDI waliyotarajiwa kutoa ushahidi wa kesi ya mtoto (16) alietuhumiwa kubakwa na baba yake wa kambo Kiungoni, wamesema hawakuridhika na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kwa kumuachia huru mshitakiwa wa kesi hiyo.

Walisema kuwa, kila siku wanapoitwa mahakamani wanakwenda, ingawa wanapofika kesi hiyo huakhirishwa kutokana na baadhi ya siku hakimu kutokuwepo mahakamani na siku nyengine mtuhumiwa kutokufika mahakamani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgonjwa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mashahidi hao walisema kuwa, siku iliyotolewa hukumu hiyo, wao hawakuwepo mahakamani kutokana na kuwa walipata dharura, jambo ambalo halikuwaridhisha.

“Sisi kila tunapoitwa mahakamani tunakwenda lakini siku nyengine hakimu hayupo na siku nyengine tunaambiwa kuwa mtuhumiwa hawezi kuja mahakamani kwa sababu anaumwa, lakini kinachotushangaza ni kuwa sisi hatukwenda siku moja tu na hakimu aliamua kuiachia huru kesi hiyo”, walisema mashahidi hao.

Babu wa watoto hao alisema kuwa, hukumu iliyotolewa na mahakama ni uonevu mkubwa kwao, kwani wao wailikuwa wanakwenda mahakamani kila wanapoitwa, hivyo aliiomba mahakama kuangalia upya shauri hilo na lirudi tena kusikilizwa, ili haki iweze kupatikana.

“Sisi hatukwenda siku moja tu kwa sababu tulipata matatizo, kwanini mahakama haikupanga tarehe nyengine kama sisi tulivyokuwa tukienda wao hawapo? asionewe huruma mtuhumiwa kwani alioufanya kwa watoto hawa ni uhalifu”, alisema Babu huyo.

Kwa upande wake mtoto aliyetuhumiwa kubakwa, alisema kuwa mara nyingi wamekwenda mahakamani bila ya kumkuta hakimu na baadhi ya siku kutofika kwa mtuhumiwa, jambo ambalo lilikuwa linawapotezea muda na nauli zao.

“Mimi sijaridhika na hukumu hiyo, kwani mahakamani ilikuwa tunaenda kila tunapoitwa, sasa siku hiyo tuliopata dharura sisi imeatolewa hukumu ya kumuachia huru kwa sababu kesi haijasikilizwa mashahidi, sijui nisema kuwa rushwa imetendeka hapa ama la”, alisema mtoto huyo.

Mama wa mtoto alisema kuwa, haikuwa kosa lao kusababisha kufutwa kesi kwa kutosikilizwa mashahidi bali ni kosa la Mahakama, kwani wao kila inapofika tarehe ilikuwa wanafika mahakamani tena kwa wakati.

“Kesi irudi maana tumepoteza pesa za kwenda mahakamani, ingawa hakimu siku nyingi hatumkuta, hivyo tunaiomba Serikali irudishe kesi hiyo, ili kama mtuhumiwa atapatikana na hatia aweze kuhukumiwa”, alisema mama huyo.

Nae Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed alisema kuwa, alisikia kuwa mahakama iliiachia huru kesi hiyo, kutokana na kutosikilizwa shahidi hata mmoja tokea ilipofikishwa mahakamani na kusema kuwa mahakama hutoa maamuzi kwa kufuata sheria, hivyo inawezekana hakimu husika ameona sababu ya kuiachia kesi hiyo.

Septemba 3 mwaka huu, hakimu wa mahakama ya Mkoa Wete Makame Mshamba Simgeni aliiachi huru kesi hiyo chini ya kifungu cha 209 (2) cha sheria namba 7 ya mwaka 2004 Sheria ya Serikali ya Zanzibar.

Kwa maelezo aliyoyatoa mahakamani hapo wakati akitoa hukimu, hakimu Mshamba alisema amemuachia huru mshtakiwa huyo kutokana na kesi hiyo kukaa mahakamani zaidi ya miezi minne bila ya kusikilizwa mashahidi.

“Kesi hii ilifunguliwa mahakamani Januari 17 mwaka 2018 na alisomewa shitaka lake Januari 31 mwaka huu na hajasikilizwa shahidi hata mmoja, hivyo namuachia huru mshitakiwa chini ya kifungu cha 209 (2) cha Sheria namba 7 ya mwaka 2004 Sheria ya Zanzibar, alisema hakimu huyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii, kesi hiyo ilifunguliwa Januari 17 mwaka huu katika mahakama ya Wilaya, kwani hakimu husika alikuwa hayupo, ambapo January 31 mstakiwa alisomewa shitaka lake na kesi kuakhirishwa hadi Febuari 21 ambapo mashahidi walifika mahakamani, ingawa mtuhumiwa alidai kuwa hawezi kusikiliza kutokana na kuwa ni mgonjwa.

Kesi ilipangwa tena Machi 20 kisha Aprili 16 ambapo mtuhumiwa hakuletwa mahakamani kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mgonjwa, Mei 14 hakimu hakuwepo mahakamani, Mei 28 na Juni 28 hakimu alikwenda likizo, ambapo ilipangiwa Julai 25 kwa ajili ya kutajawa tena.

Baada ya kutajwa tena kesi hiyo ilipangiwa kurudi tena Septemba 3 mwaka, ambapo iliondoshwa na mahakama chini ya kifungu 209 (2) kutokana na kesi hiyo kukaa mahakamani muda wa miezi tisa bila ya kusikilizwa ushahidi.

Hata hivyo baba huyo anatumikia kifungo cha miaka 12 jela kwa kesi mbili za motto wake wa miaka nane (8), ambazo ni kubaka na shambulio la aibu.

PembaToday

Share: