Habari

Massauni: Zanzibar haijavunja Muungano

Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni Hamad Yussuf Masauni

Na Mussa Juma, Mwananchi

Aprili 5 2014

Kwa kuwa Tawala za Mikoa siyo suala la Muungano, sioni tatizo Rais wa Zanzibar kugawa wilaya

Dodoma. Bunge la Katiba limeanza kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba katika sura ya kwanza na sura ya sita ambayo kwa kiasi kikubwa inahusu Muundo wa Muungano.

Sura hizi mbili, ndizo ambazo zinaelezwa kuwa ni roho ya mjadala wa Katiba katika Bunge hilo Maalumu kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imependekeza Muundo wa Muungano wa serikali tatu katika sura hizo na ibara nyingi katika rasimu inayojadiliwa, zinajengwa kwa muundo huo wa Muungano.

Wakati akiwasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba bungeni Jaji, Joseph Warioba alitoa sababu nyingi za tume kufikia kukubali mapendekezo ya wananchi kuhusu serikali tatu.

Miongoni mwa sababu kubwa ni pamoja na sasa Muungano kubadilika kuwa ni wa serikali mbili na nchi mbili, Muungano ambao siyo ule ulioachwa na waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid Karume wa serikali mbili nchi moja.

Nchi mbili ndani ya Muungano, zimetokana na Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, ambayo yalifanyika mwaka 2010.

Katika mabadiliko hayo yaliyopo katika sehemu ya kwanza tu ya Katiba ya Zanzibar yanasema Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambavyo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.

Zanzibar ni sehemu ya Muungano

Namba mbili katika katiba hiyo sehemu ya kwanza, inaeleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya pili(a) inaeleza kuwa , kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyototungwa na Baraza la Wawakilishi.

Katiba ya Zanzibar pia imebadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema Sheria za Muungano zinazotungwa na Bunge la Jamhuri, zitume sehemu zote, lakini kwa sasa Zanzibar ili Sheria ya Muungano itumike ni lazima ipelekwe Baraza la Wawakilishi.

“Maana yake ni kuwa, Katiba ya Zanzibar ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” anasema Jaji Warioba.

Kutokana na utata huu, Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad Yusuph Masauni alifanya mahojiano na gazeti hili na kueleza ifuatavyo;

Swali: mababadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, yanatajwa kuwa moja ya mambo ambayo yamechangia sana mapendekezo ya Serikali tatu, je nini maoni yako?

Jibu: Ni kweli kuwa yamefanyika mabadiliko hayo, lakini kwa ufahamu wangu mimi nadhani Zanzibar hawajavunja Katiba, kwani kusema tu Zanzibar pia Katiba ya Zanzibar kumpa Mamlaka Rais kuigawa katika mikoa na wilaya siyo kosa.

Swali: lakini jambo hili linatajwa kuwa nyeti kwani kwa kiasi kikubwa licha ya matatizo mengine, inaonekana ndilo limebariki uwepo wa serikali tatu.

Jibu: Hapana. Kwanza naomba ieleweke Suala la Tawala za mikoa siyo la Muungano hivyo, haimzuii Rais wa Zanzibar kugawa mikoa na wilaya kwani jambo hili si la Muungano.

Swali: Unadhani ni kwa nini Zanzibar imefikia kufanya mabadiliko haya makubwa ya Katiba yake?

Jibu: Mimi sioni kama kuna tatizo, lakini kwa kuwa sasa tunatengeneza Katiba ya Muungano ni vyema tukafanya marekebisho kama tunataka kulifanya suala la tawala wa mikoa liwe la Muungano.

Swali: Masauni wewe ni mbunge wa Jamhuri wa Jimbo la Kikwajuni Zanzibar. Hivi sasa kuna mjadala mzito juu ya Muundo wa Serikali nini maoni yako?

Jibu: Mimi naunga mkono msimamo wa chama changu na wananchi wa jimbo langu kuendelea na muundo wa serikali mbili.

Swali: Lakini muundo huu unaonekana kulalamikiwa na Wazanzibari wengi kutokana na hoja kuwa Tanganyika imevaa koti ya Muungano na fedha nyingi zinaendesha Maendeleo ya Tanganyika badala ya Zanzibar.

Jibu: Ni kweli kuna madai hayo, lakini naamini changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi kama ambavyo aliahidi Rais Jakaya Kikwete alipokuja kuzindua bunge.

Swali: Lakini hata baada ya bunge kuzinduliwa na kutolewa ahadi hizo na Rais Wazanzibari na hata wanaounga mkono mfumo wa Serikali tatu, wanasema hata katika bunge hilo bado kunaonyesha Zanzibar kumezwa. Nini Maoni yako?

Jibu: Hayo ni madai ya wanasiasa wachache ambao wana malengo ya kushika dola kama mfumo wa Serikali tatu, ukipita lakini mimi binafsi naamini Zanzibar haijamezwa bungeni kwanza katika kamati zote kama Mzanzibari siyo mwenyekiti basi ni makamu.

Swali: Je, wewe binafsi kwa mtazamo wako unaona ni Muundo wa Serikali ngapi unafaa na je, wananchi wa jimbo lako watakuelewa kwa kutetea msimamo wa chama chako?

Jibu: Mimi naunga mkono serikali mbili na hakika nikirudi na serikali tatu wananchi wangu hawatakubali sio kwa sababu jimbo langu wana ccm ni wengi lakini wana hoja.

Swali: Baraza la Wawakilishi limetajwa pia kupendekeza muundo wa serikali tatu, hasa kutokana na hoja yao, kutaka Zanzibar yenye Mamlaka, Tanganyika yenye Mamlaka na kujulikana Mamlaka ya Muungano.

Jibu:Binafsi siwezi kuzungumzia maoni ya wawakilishi lakini nadhani tatizo ni tafsiri tu zinachanganya watu.

Swali: Unadhani sasa Bunge hili la Katiba linaweza kusaidia kuondoa matatizo ya Zanzibar na hata Tanganyika katika mfumo wa Muungano uliopo?

Jibu: Ndio kwani Bunge hili lina jukumu kubwa la kutunga sheria ambazo ndizo zitakuwa kuu kwa pande zote na kuondoa kero za muda mrefu kwa kila upande.

Swali: Nini hofu yako katika Muundo wa serikali tatu?

Jibu: Hakuhitaji mtu kuwa ya PhD kujua kuwa serikali tatu zitaua muungano wetu, hofu yangu mimi bila Serikali mbili muungano unakwenda kufa.

Swali: Nini maoni yako ya jumla kuhusu Bunge Maalumu la Katiba?

Jibu: Mimi wito wangu kwa wajumbe,tutengeneze Katiba hii kwa maslahi ya wananchi na sio masilahi yetu. Hakuna wananchi ambao wanataka vurugu zitokee katika Bunge hili hata baada ya kupitishwa mapendekezo ya Katiba.

Chanzo Mwananchi

Mussa Juma ni mwandishi wa mwananchi.0754296503.

Share: