Habari

Masuala yasio na majibu katika Muungano

Othman Masoud Othman ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwasilisha mada katika Mkutano Maalum ulioandaliwa na Zanzibar Law Society siku ya kuadhimisha miaka 41 ya Muungano katika Hoteli ya Bwawani Zanzibar tarehe 23.4.2005 wakati huo Othman alikuwa ni Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).

Kumbukumbu za Mh Othman Masoud Othman

MASUALA YASIYO NA MAJIBU KATIKA MUUNGANO

[Mada imetayarishwa na Kuwasilishwa Katika Mkutano Maalum ulioandaliwa na Zanzibar Law Society Kuadhimisha Miaka 41 ya Muungano. Hoteli ya Bwawani Zanzibar tarehe 23.4.2005]
UTANGULIZI

Tokea kuasisiwa hapo tarehe 26 Aprili, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndio uliozaa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania umekuwa na sifa mbili kuu. Sifa moja ni ile ya kuwa nyenzo au kitambulisho cha umoja wa kitaifa Tanzania, na hivyo wale wanaojinadi kwa uzalendo na hisia za umoja wa kitaifa wamekuwa wakijinasibisha na kuupenda mno Muungano na kuahidi kuulinda kwa gharama zozote. Mapenzi haya ya Muungano yamepelekea hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa na kifungu mahsusi cha kuwataka Viongozi wa Kitaifa (Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanziba) kula kiapo cha kuulinda Muungano kabla ya kuanza kazi zao (Kifungu cha Katiba ya Muungano). Aidha Sheria ya Vyama vya Siasa inakiondolea sifa ya kutosajiliwa chama chochote cha Siasa ambacho Katiba yake au sera zake ni za kutaka kuvunja Muungano. Hii ni kusema kwamba Katiba na Sheria zetu zinakataza wananchi kuwa na mawazo ya kuvunja Muungano. Huu ni ulinzi na mapenzi makubwa kwa Muungano.
Sifa ya pili ni kuwa Muungano umekuwa ni kitu kinachotambuliwa na kukubaliwa na wale ‘WANAOUPENDA’ na “WASIOUPENDA” kwamba una kasoro nyingi – lugha ya siku hizi huitwa KERO za MUUNGANO. Fedha, wataalamu na muda mwingi umetumika katika kutafuta suluhisho la Kasoro au Kero hizo, lakini mafanikio yamekuwa madogo mno (kama yapo). Kuna wanaosema kuwa Kasoro au Kero za Muungano zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua. Wanaosema hivyo mimi nawaunga mkono. Naamini yeyote atayetafakari

kwa makini atawaunga mkono. Hivyo, suala la msingi ni kwa nini kipenzi hiki cha Taifa la Jamhuri ya Muungano kinachoitwa MUUNGANO ambacho sote tunakubali kuwa kinaumwa tokea uchanga wake hadi leo, miaka 41 tokea kizaliwe, kimeshindwa kupatiwa dawa pamoja na Tanzania kuwa na mabingwa wa dawa za kisiasa na pamoja na juhudi kubwa za mabingwa hao bado MUUNGANO unaumwa zaidi. Wapo wanaodai kuwa dawa ipo na inajulikana lakini pengine inaonekana ni chungu sana kupewa kipenzi hicho cha Watanzania!!.

1.2 Ni maoni yangu kwamba MUUNGANO una kasoro za msingi za kimaumbile. Kasoro hizo ni miongoni mwa sababu za MUUNGANO kuwa na KERO sugu. Kasoro hizo za maumbile ni kuwepo kwa masuala ya msingi ya kikatiba ambayo hayana majibu ama kutoka ndani ya Katiba, Sheria, Sera na hata kutoka kwa watendaji.

1.3 Katika Waraka huu nitajaribu kueleza juhudi mbali mbali za kuondoa Kero za Muungano ambazo zimeshindwa kuondoa Kero hizo. Juhudi hizo na kushindwa kwake ni kielelezo cha kuwepo kwa kasoro za maumbile katika Muungano. Aidha nitaeleza baadhi ya Masuala yasiyo na Majibu katika Muungano. Maswali hayo ni kielelezo cha kasoro za maumbile na ni miongoni mwa sababu za kushindwa kupatiwa dawa KERO za Muungano. Kwa kuelewa mambo hayo mawili pengine itatusaidia sote kwa pamoja kutoa mapendekezo ya kusawazisha KERO za Muungano.

2.0 JUHUDI ZA KUONDOA KERO ZA MUUNGANO

2.1 Katika kutekeleza shughuli za Muungano matatizo kadhaa yamejitokeza ambayo yamepelekea kuwepo zinazoitwa Kero za Muungano.

Tatizo la siku za mwanzo kabisa la Muungano lilijitokeza mwaka 1965 wakati jambo jipya la Muungano lilipoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano; inaonyesha bila ya makubaliano baina ya Serikali hizi mbili. Mawasiliano yaliopo katika kumbukumbu baina ya Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano yanaonyesha kuwa mawazo ya Serikali ya Zanzibar katika uundaji wa Benki Kuu hayakusikilizwa. Baada ya muelekeo wa kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki kufifia, nchi za Afrika Mashariki zikitanguliwa na Uganda zilichukua hatua za kuanzisha Benki Kuu zao hata kabla ya kuivunja rasmi Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Katika hali hiyo ndipo Serikali ya Muungano ilipochukua hatua za haraka za kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania bila ya maafikiano rasmi na Zanzibar na hivyo kupelekea Zanzibar kukosa haki zake katika Bodi ya Sarafu na ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.

Kutokana na hatua hiyo Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karumed aliunda Kamati ya watu 12 ikiongozwa na mtaalamu wa Masuala ya Benki Bw. E. Ebert ili kuishauri Serikali juu ya kuanzisha Benki ya Serikali ya Zanzibar. Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake mwishoni wa mwaka 1965. Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine ilipendekeza kuwa Benki hiyo iwe ndio Benki ya Serikali na itumike kusimamia hesabu za (Accounts) Serikali. Kamati ilipendekeza hadi ifikapo July, 1966 ‘accounts’ zote za Serikali ziwe zimehamishiwa Benki hiyo. Hapo ndipo ilipoanzishwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo iliendelea kuwa ndio Benki ya SMZ hadi mwaka 2001 wakati Benki Kuu ya Tanzania ilipoanza rasmi kuwa Benki inayotumiwa na Serikali ya Zanzibar. Hivyo pamoja na kuwepo Benki Kuu kama chombo cha Muungano lakini kuanzia awamu ya kwanza hadi ya Tano za Serikali ya Zanzibar, haikutumia Benki hiyo. Serikali ya Muungano ilikuwa siku zote ikililalamikia jambo hilo.

2.2 Wakati wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Zanzibar, matatizo ya Muungano yalijitokeza zaidi. Rais Aboud Jumbe alionekana dhahiri kutoridhishwa hata kidogo na mwenendo wa Muungano. Mbali ya kutafuta mtaalamu wa Sheria kutoka Ghana, Bw. Bashir Swanzi ili kujenga Hoja ya kukiukwa kwa Katiba ya Muungano na kupendekeza hatua za kisheria za kuondoa kasoro hizo, hatua iliyopelekea kuanguka kwake katika Uongozi, lakini yeye binafsi alichukizwa sana na mambo ya Muungano yanavyoendeshwa bila ya kufuata Katiba na ‘sprit’ ya Muungano. Katika moja ya mawasiliano yake ya kiserikali ya tarehe 23 Oktoba, 1983 aliwahi kuandika yafuatayo:

“Kosa moja ambalo linaendelea kufanywa ni lile la kudhani kwamba kuimarisha Muungano kuna maana moja na kuhaulisha shughuli zisizokuwa za Muungano ziwe za Muungano na kwamba Chama na Serikali ya Muungano wanaweza kufanya hivyo – bila ya kuzingatia Katiba wala hisia au matakwa ya Zanzibar.

Dhana hizo ni ama ni za kupotosha kusudi kwa sababu wanazozielewa wenyewe wafanyao hivyo, au ni kukataa kuelewa Katiba. Vyovyote vile ilivyo ni mashaka.

Kisheria shughuli yoyote isiyo ya Muungano haiwezi kufanywa iwe ya Muungano bila ya ridhaa ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika au na Serikali ya Muungano kwa niaba ya Tanzania Bara. Mpango wa Serikali ya Muungano kuwakilisha pia Tanzania Bara umeleta fadhaa na wasiwasi wa kutosha katika miaka kadhaa, hasa ya hivi karibuni.

Hata kingekuwa Chama au Serikali ya Muungano vingeweza Kikatiba kufanya hivyo, na haviwezi , basi lingelikuwa ni kosa la uadilifu na pia la kisiasa kufanya hivyo, bila ya ridhaa na makubaliano ya pande zote mbili za Muungano, wala hicho kisingekuwa kitendo cha kuimarisha, bali cha kudhoofisha na hata kupotosha dhamiri na maana ya Muungano.

Najua baadhi wana mashaka na kimya changu na wangependa kujua msimamo wangu juu ya suala hili la masahihisho ya Katiba. Msimamo haunihusu kwa sasa, jambo la msingi ni kwamba lazima Katiba ziheshimiwe, maadili yafatwe na dhamiri ya Muungano ihifadhiwe. Dhamiri lazima siku zote ibaki kuwa ni zao la nidhamu ya hali ya juu kabisa.

Muungano au Umoja hauwezi kuimarishwa kwa upande mmoja kutwaa madaraka ambayo ni ya pande mbili za umoja huo. Ikiwa wote tutatekeleza wajibu wetu kwa dhati, haki haitakuwa mbali kuonekana na kila upande utakuwa na utaridhika na haki yake. Huko ndiko kuimarisha Muungano”.

Hii ni ushahidi wa wazi kuwa pamoja na viongozi wakuu wa Muungano kuupenda Muungano lakini waliona kasoro za wazi za utekelezaji wa Muungano zaidi ya miaka 20 iliyopita.

2.3 Katika Awamu ya Tatu na Nne mbali ya mambo ya Muungano kuongezeka, juhudi za kusawazisha kasoro za Muungano ziliendelea. Njia kubwa iliyotumika ilikuwa ile ya vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Muungano na Zanzibar. Vikao hivyo vikiongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi.

2.4 Katika Awamu ya Tano, kama tutavyoona hapo baadae, Serikali ilichukua hatua nyingi zaidi kuliko awamu yoyote kushughulikia kasoro za Muungano. Dr. Salmin Amour hakuwa akificha hisia zake za kutoridhishwa na utekelezaji wa Muungano. Miongoni mwa mambo aliyoyawekea msimamo wazi wa kutaka kuwe na uwazi na masawazisho ni masuala ya uchumi, kupunguzwa mambo ya Muungano yasiyo ya lazima na suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kuna taaarifa za kuaminika kuwa wiki chache kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Rais Salmin Amour alimuandikia Waraka maalum Rais Benjamin Mkapa, kueleza msimamo na mtazamo wa Zanzibar juu ya uwakilishi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo ambalo nina hakika ni kuwa Waraka huo wa kurasa 10 wenye maoni na mtazamo wa Zanzibar haukushughulikiwa hadi leo!!

2.5 Awamu ya Sita ya Serikali ya Zanzibar inajulikana wazi kwa msimamo wake juu ya suala la uchimbaji wa mafuta – msimamo ambao iliurithi kutoka Awamu ya Tano. Mbali ya suala hilo, iliunda Kamati ya Wataalamu katika siku za mwanzo za kuingia madarakani. Kamati ilichambua kasoro za Muungano na kupendekeza mambo ya kubaki katika Muungano, mambo ya kupunguzwa, mambo ya kuongezwa na utaratibu wa kuendesha masuala ya Muungano kisera, kiutawala na katika kutunga Sheria za Muungano. Miongoni mwa mapendekezo mahsusi ya Kamati ilikuwa ni pamoja na kuwa Bunge la Tanzanzia liwe na sehemu mbili – ‘Lower house’ itayoshughulikia mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na ambapo Wabunge wa Zanzibar hawatoshiriki na “Upper House” ambayo itashughulikia mambo ya Muungano tu na itakuwa na uwakilishi sawa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha Kamati ilirudia mapendekezo ya Bomani ya kuwa na Baraza la Taifa (Council of State) ingawa kwa muundo tofauti. Baraza hilo kazi yake ni kushughulikia mambo ya Muungano kisera na kiutawala. Kamati iliwasilisha Ripoti yake Serikalini mwezi March, 2001. Kwa kadri ya ninavyoelewa hakuna hata moja katika mapendekezo ya Kamati, na ambayo yalikubaliwa na Serikali lililofanyiwa kazi. Eneo jengine lilofanyiwa kazi na Awamu ya Sita ni masuala ya fedha – Benki Kuu na Tume ya Pamoja ya Fedha.

2.6 Maelezo hayo yanathibitisha mambo mawili:-
(a) Muungano una kasoro za msingi
(b) Juhudi za kuondoa kasoro hizo zinazofanywa na viongozi wa SMZ hazijawa na mafanikio ya maana

JUHUDI MAHSUSI ZA SMT NA ZA SMZ

2.7 SMZ peke yake ama kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano, zimechukua hatua kadhaa za kutafuta ufumbuzi wa Kero za Muungano. Kwa upande wa SMZ, miongoni mwa hatua ilizochukua na ambazo zinajulikana ni pamoja na kuunda Kamati mbali mbali. Miongoni mwa Kamati zilizoundwa na SMZ kushughulikia Kero za Muungano kati ya mwaka 1990 na 2003 ni pamoja na ziufatazo:
(a) Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992.

(b) Kamati ya Rais ya Kupambanua na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamhuna, 1997).

(c) Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Kisanga (Kamati ya Salim Juma).

(d) Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya SMZ juu ya Kero za Muungano. (Kamati ya Ramia, 2000).

(e) Kamati ya BLM juu ya Sera ya Mambo ya Nje.

(f) Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano (2001).

(g) Kamati ya BLM ya Jamuiya ya Afrika Mashariki.

(h) Kamati ya Mafuta

(i) Kamati ya Madeni baina ya SMZ na SMT.

(j) Kamati ya Suala la Exchusive Economic Zone (EEZ)
(k) Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu.

(l) Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu – (1996 – 1999)

SMZ pia imewahi kuajiri mtaalamu wa mambo ya fedha
Dr. Courtrey Blackman na Mtaalam wa masuala ya mafuta.

2.8 Mbali ya baadhi ya Kamati hizo za SMZ peke yake, SMT na SMZ zimeunda Tume, Kamati na Kuajiri Wataalamu mbali mbali ili kutafuta suluhisho la Kero mbali mbali za Muungano. Miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni kama zifuatazo:
(a) Kamati ya Mtei
(b) Tume ya Nyalali
(c) Kamati ya Shellukindo
(d) Kamati ya Bomani
(e) Kamati ya Shellukindo 2, ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
(f) Kamati ya Harmonisation.
(g) Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)

Aidha SMZ na SMT zimefanya vikao vya pamoja visivyopungua 80 katika ngazi mbali mbali ili kuzungumzia Kero za Muungano. Aidha Serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba msaada wa IMF ili kuzishauri kuhusiana na Benki Kuu, mgawano wa Misaada na uhusiano wa kifedha (intergovernmental fiscal relationship).

2.9 Mbali ya juhudi zote hizo, tarehe 14 Novemba, 2000 wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa akizundua Bunge aliahidi kuzipatia ufumbuzi Kero za Muungano ndani ya siku 60!! Tokea ahadi ilipotolewa hadi leo ni siku 1620 – yaani siku 60 zimepita mara 27.

2.10 Pamoja na hatua zote hizo zilizoambatana na masikitiko ya Viongozi wa juu, manung’uniko ya wananchi wa pande zote mbili juu ya uendeshaji wa Muungano na ahadi nzito za viongozi wa juu wa Serikali za kuondoa kasoro za Muungano – lakini bado Kero au Kasoro hizo zipo pale pale au zimezidi zaidi. Cha kusikitisha zaidi kuwa baadhi ya Kero zilizozungumzwa mwaka 1984 katika vikao vya pamoja ndizo Kero hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Shellukindo ya 1992 na katika Muafaka baina ya SMZ na SMT wa mwaka 1994 na ndizo hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Kamati ya Wataalamu ya SMZ ya 2001.

Suala muhimu ni kuwa ni kwa nini juhudi zote hizo zimeshindwa? Jibu langu ni kuwa Muungano una Kasoro za maumbile, za kuzaliwa nazo!!

2.11 Suala muhimu ni kuwa ni vipi tutaweza kuzibaini Kasoro hizo za Maumbile katika Muungano? Jibu ni kuwa baadhi ya kasoro hizo hazitaki utaalamu kuziona. Hata hivyo kwa sababu kasoro nyingi za Muungano ziko wazi na zimeshazungumzwa mara nyingi, wengi wamezizoea na kuona kwamba kasoro ni sehemu ya Muungano. Lakini tunaposogea mbele zaidi na kujiuliza ni kwa nini Kero za Msingi Muungano zimeshindwa kupatiwa ufumbuzi pamoja na juhudi na ahadi nzito za viongozi, nadhani jibu si kuwa Kero hizo zimezoeleka au kuwa ni sehemu ya Muungano. Tunapaswa tujiulize zaidi nini kiini cha tatizo. Wengi wana maoni kuwa kiini cha tatizo ni mfumo wa Serikali mbili. Ingawa mfumo huo kweli umechangia, lakini hilo bado ni jibu rahisi kwa suala zito (gumu) – “it is an oversimplified answer to a very complicated question”.

2.12 Kwa maoni yangu, tatizo la msingi ni kuwa kila uhusiano baina ya watu una Kanuni za msingi zinazoongoza uhusiano huo (“basic principles” au “grundnorm” za uhusiano). Aidha kuna mipaka ya uhusiano (parameters). Nyenzo za uhusiano kama vile nyaraka na sera lazima ziwe na uwezo wa kujibu maswali ya msingi kuhusiana na uhusiano huo.

2.13 Katika Muungano wa Tanzania, Zanzibar na Tanganyika ziliungana kwa baadhi ya mambo tu na sio mambo yote na ndio maana kuna orodha ya mambo ya Muungano. Aidha ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano inaeleza wazi kuwa Bunge halina mamlaka ya Kutunga Sheria kwa mambo ya Zanzibar yasiyokuwa ya Muungano. Hivyo ilitarajiwa kwamba, kwa vile pande hizi zimeungana kwa baadhi ya mambo tu Kanuni ya msingi ni kuwa pande hizo lazima ziwe na kauli sawa kuhusiana na Mambo ya Muungano katika Sera, Utawala na katika kuyatungia Sheria. Aidha ziwe na kauli sawa katika kuongeza na kupunguza mambo ya Muungano na Katiba iweke bayana jambo hilo.

Katika Muungano wa Kikatiba au wa kisiasa, Katiba au Mkataba wa Muungano, Sheria na Sera za Muungano ndio nyenzo kuu. Iwapo nyenzo hizo zinashindwa kutoa majibu kwa masuala ya msingi kuhusiana na Muungano ni kielelezo tosha kuwa Muungano huo una kasoro za maumbile. Kasoro hizo ni pamoja na kutokuwa na Kanuni za Msingi na kutokuwepo Mipaka katika Waraka huu tutaeleza Masuali ya Msingi ambayo hayana Majibu katika Katiba, Sheria na Sera za Muungano.

3.0 MASUALA YASIYO NA MAJIBU

3.1 SUALI LA KWANZA: JE WASHIRIKI WA MUUNGANO BADO WAPO AU HAWAPO?

3.1.1 Suala hili ni la msingi kwa vile nchi ambazo zimeungana kwa baadhi ya mambo tu, inategemewa kwamba waliounganisha mambo hayo wapo, wana vikao rasmi vinavyotambuliwa na Katiba na Sheria za Nchi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wanaamua kuongeza kupunguza mambo ya Muungano wakiwa na nguvu sawa ya uamuzi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wana kauli sawa za maamuzi juu sera, uendeshaji na Sheria za Muungano. Suala ni kuwa hivi ndivyo hali ilivyo?

3.1.2 Suala hili kila mtu anaweza kuwa na maoni na fikra zake, lakini sio jibu na wala huwezi kupata jibu ndani ya Katiba, Sheria na Sera za Muungano. Sababu zinazoonyesha kuwa hakuna jibu la suali hili ni zifuatazo:

(a) Wengi wanadhani kuwa Zanzibar ipo na ni Tanganyika tu ndio haipo – lakini ukweli Zanzibar haipo katika Muungano. Wengine wanahisi Tanganyika ipo ndani ya Muungano ikivaa koti la Muungano lakini hata hilo haliko wazi kama iliomo ndani ya Muungano ni Tanganyika au nalo ni koti tu la Tanganyika.

(b) Hakuna Kikao kinachotambulika kisheria kinachozikutanisha pande mbili za Muungano.

(c) Mambo ya Muungano kiutawala na kisera yanaamuliwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Zanzibar haiwakilishwi ndani ya Baraza hilo. Rais wa Zanzibar anaingia kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri na sio kama upande mmoja wa chombo hicho ambao unaruhusiwa kutetea msimamo wa Zanzibar. Hivyo ndani ya Baraza Rais wa Zanzibar haiwakilishi Zanzibar kwa vile akiwa ndani ya Baraza hilo anawajibika kwa Rais wa Muungano na sio kwa mamlaka yoyote ya Zanzibar. Mawaziri ambao ni Wazanzibari nao hawawakilishi Zanzibar bali ni Mawaziri sawa na wengine ambao wanafungwa na Kanuni ya kuwajibika kwa pamoja (Collective responsibility). Hivyo lazima wakubaliane na maamuzi ya wengi na kwa vyovyote vile hawamo ndani ya Baraza kuiwakilisha Zanzibar.

(d) Inapotokea Rais wa Muungano au Makamo wa Rais anatoka Zanzibar – jee anaiwakilisha Zanzibar. Ameteuliwa na Zanzibar kama mshirika wa Muungano kuiwakilisha? Anayo haki na uwezo wa kisheria wa kutetea maslahi ya mmoja wa Washiriki ndani ya Muungano ambayo ni Zanzibar. Jibu ni kuwa Makamo wa Rais wala Rais anapotokea kutoka Zanzibar haiwakilishi Zanzibar ndani ya Muungano bali anatumia fursa yake kama Mtanzania kushika nafasi hiyo. Hapaswi na hana uwezo wala wajibu wa kutetea Zanzibar ndani ya Muungano.

(e) Katika kutunga Sheria za Muungano Zanzibar kama mshirika inawakilishwa? Takribani Sheria zote za mambo ya Muungano zinapitishwa kwa wingi wa Kura. Kwa vile idadi ya wabunge kutoka Zanzibar takriban ni robo tu ya Wabunge wa Bunge la Muungano ni wazi kuwa Zanzibar kupitia Wabunge hao haina kauli katika kutunga Sheria za Muungano. Ni mambo yale tu yaliyoainishwa katika Orodha ya Pili ya Jadweli ya Pili ya Katiba ya Muungano ndio yanayoamuliwa kwa kauli sawa. Kichekesho ni kuwa kati ya mambo hayo 8 yaliyoorodheshwa baadhi sio mambo ya Muungano.

(f) Inapotokea Zanzibar kushirikishwa kama Zanzibar katika masuala ya Muungano ni kwa njia ya SMZ kutakiwa kutoa maoni. Hata hivyo, maoni hayo ya SMZ ambayo baadhi ya wakati huandaliwa na Baraza la Mapinduzi, mara nyingi hukataliwa na hata Mkurugenzi tu wa Serikali ya Muungano au Katibu Mkuu au Waziri. Baadhi ya mifano mashuhuri ambapo maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa katika masuala muhimu ya Muungano ni:

(i) Katika uanzishaji wa Benki Kuu, mwaka 1965 na marekebisho ya Benki Kuu, 1995.
(ii) Uanzinshwaji wa Mamlaka ya Mapato TRA.
(iii) Katika suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(iv) Sera ya Mambo ya Nje
(v) Uraia na Uhamiaji na
(vi) Sheria ya Deep Sea Fishing Authority.

(g) Kwa upande wa pili, ingawa tunasema kuwa Tanganyika imevaa koti la Muungano lakini suala bado linabaki, kuwa Tanganyika (T/Bara) kama mshirika wa Muungano ipo. Jee Serikali ya Muungano kweli inawakilishwa na kutetea maslahi ya Tanganyika ndani ya Muungano na kwa utaratibu gani?

3.2 NINI MAANA YA JAMBO LA MUUNGANO
3.2.1 Suala hili lina sehemu mbili zifuatazo:
(a) Mambo ya Muungano ni mangapi; na
(b) Jambo linapoitwa ni la Muungano maana yake ni nini.

Mambo ya Muungano ni Mangapi:
3.2.2 Jibu rahisi kwa watu wengi kuhusiana na suala hili ni kuwa mambo ya Muungano ni 22 kama yalivyoainishwa na Katiba ya Muungano katika Jadweli la Kwanza. Lakini hata Jadweli hilo limeorodhesha zaidi ya mambo 22 kama ifuatavyo:
(i) Katiba ya Muungano
(ii) Mambo ya nje
(iii) Ulinzi
(iv) Usalama
(v) Polisi
(vi) Hali ya Hatari
(vii) Uraia
(viii) Uhamiaji
(ix) Mikopo ya Nje
(x) Biashara
(xi) Utumishi katika Serikali ya Muungano
(xii) Kodi ya Mapato
(xiii) Forodha (Ushuru)
(xiv) Kodi ya Bidhaa (exercise)
(xv) Bandari
(xvi) Usafirishaji wa Anga
(xvii) Posta
(xviii) Simu
(xix) Sarafu
(xx) Mabenki
(xxi) Fedha za Kigeni
(xxii) Leseni za Viwanda
(xxiii) Takwimu
(xxiv) Elimu ya Juu
(xxv) Mafuta yasiyosafishwa
(xxvi) Gesi asilia
(xxvii) Baraza la Mitihani
(xxviii) Usafiri wa Anga
(xxix) Utafiti
(xxx) Mahkama ya Rufaa
(xxxi) Usajili na Shughuli za Vyama vya Siasa

3.2.3 Pamoja na Orodha hiyo jadweli ya Pili, Orodha ya Pili inaeleza kwamba, Bunge lilipotaka kubadili masuala yanayohusiana na Mamlaka ya Serikali ya Zanzibar na suala la Mahkama Kuu ya Zanzibar – lazima yakubaliwe na theluthi mbili ya Wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wa Zanzibar. Suala hapa ni kuwa kwani hayo ni mambo ya Muungano?

3.2.4 Dalili ya pili inaonyesha kwamba Mambo ya Muungano hayajulikani ni mangapi ni kuwa yapo mambo yanayofanywa kimuungano pamoja na kwamba si ya Muungano (kama vile Bima – inayosimamiwa na Kamishna ya Bima). Aidha yapo mambo ya Muungano ambayo hayasimamiwi kimuungano kama vile Takwimu (isipokuwa sensa ya Idadi Watu), Bandari na Leseni za Viwanda.

3.2.5 Dalili ya tatu ni kuwa Bunge limekuwa likitunga Sheria na kuzifanya za Muungano hata kwa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano. Mfano ni Sheria ya Proceeds of Crimes Act ya 1991.

3.2.6 Dalili ya nne ni kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo Serikali zenyewe (pamoja na Wanasheria Wakuu) hazikubaliani kama ni ya Muungano au si ya Muungano. Maeneo hayo ni kama vile “Deep Sea Fishing Authority”, na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora. Aidha suala la Ushirikiano wa Kimataifa.

3.2.7 Dalili ya Tano ni kuwa hata kwa yale mambo ambayo yamo katika Orodha ya Mambo ya Muungano, mengi hayana tafsiri na hivyo hayajulikani mipaka yake. Mifano ni kama vile Elimu ya Juu (inaanzia wapi inaishia wapi?), Usalama (Jee ni ule wa hata kuweka “watchman”) jee Serikali ya Zanzibar haina siri zake peke yake ambazo hazipaswi kujulikana na Serikali ya Muungano na hivyo kuwa na taratibu zake za usalama? Mikopo ya Nje, Biashara za Nje. Posta na Simu jee ni miundo mbinu au udhibiti (regulatory aspect).

3.2.8 Dalili au hoja ya Sita ni kuwa jee mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara pekee nayo ni ya Muungano au si ya Muungano. Hili linaonekana kama suali la kijinga mno, lakini ndio suali gumu hata kwa wanaojiona werevu mno. Hakuna ubishi kuwa jambo lisipokuwa la Muungano Zanzibar inaweza kulisimamia wenyewe, lakini kuna matatizo kwa upande wa Tanzania Bara.

3.2.9 Baadhi ni kama yafuatayo:
(i) Bajeti: Zipo baadhi ya Taasisi za Muungano ambazo zinafanya kazi za Muungano na sizizo za Muungano – kwa mfano Bunge linatunga Sheria na kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Vivyo hivyo kwa ‘Executive’ na Judiciary ya Muungano. Hivi gharama zake zitoke wapi. Kwa sasa Bunge na Executive inajulikana kuwa ni za Muungano, hivyo igharamiwe na Mfuko wa Muungano?

(ii) Taasisi zisizo za Muungano ndizo zinazoiwakilisha Zanzibar nje kwa jina la Tanzania mfano Kilimo, Kazi, Utalii na hata Tanzania Football Federation. Hivyo suala linakuja ni wakati gani taasisi ya Tanzania Bara isiyokuwa ya Muungano inakuwa sio ya Muungano?

3.2.10 Majibu ya maswali yote hayo hayamo katika Katiba wala Sheria zetu wakati ni mambo ya msingi na ndio uti wa mgongo wa Muungano.

Jambo linapoitwa la Muungano Maana yake Nini.

3.2.11 Jibu la rahisi ni kuwa jambo linapoitwa la Muungano ni kuwa Zanzibar haina uwezo wa kulisimamia kisera, kiutawala na kisheria. Hata hivyo suala hili ni gumu kuliko linavyoonekana. Kabla ya kuja sera za biashara Huria mashirika kama vile Air Tanzania, Shirika la Posta na Simu na Benki ya Taifa ya Biashara n.k yakijulikana kama mashirika ya Muungano. Katika vikao kadhaa ilikubaliwa kuwa Zanzibar ishirikishwe katika uendeshaji wa mashirika hayo ya Muungano. Mashirika hayo mengi yamebinafsishwa.

3.2.12 Hisa za mashirika ama zinamilikiwa na HAZINA ya Serikali ya Muungano ama zimeuzwa kwa ‘Strategic Investors” au hata kwa wananchi. Zanzibar haikupewa hisa. Kuna hoja kwamba zile hisa za Serikali ya Muungano ndio pia za Zanzibar. Hoja hii haina uzito kwani katika Muafaka baina SMT na SMZ ilikubaliwa kuwa suala hilo lizungumzwe upya baina ya Serikali mbili (Uk. 46, dondoo la 18.4.3 la Muafaka). Kwa kadri ya ninavyofahamu suala hilo halijazungumzwa tena na Zanzibar imekosa haki zote katika mashirika hayo yaliyokuwa ya Muungano. Tatizo kama hilo lilijitokeza katika Benki Kuu. SMZ ilipodai kuwa na hisa ambazo ilizilipia kupitia Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, Zanzibar ilielezwa na SMT kuwa haiwezi kuwa na hisa katika Benki Kuu lakini inaweza kupewa mafao kwa kima cha asilimia 4.5.

3.2.13 Kwa upande wa pili, taasisi ambazo ni za Muungano kama vile TRA, TPDC, TCRA, TCAA, n.k zinaonekena ni za Muungano katika ngazi ya Bodi ya Wakurugenzi. Hata hivyo katika ajira vigezo vinavyotumika ni vya Tanzania Bara. Kwa mfano anayeomba kuajiriwa katika Taasisi hizo kama Mwanasheria, lazima awe ni Wakili wa Mahkama Kuu ya Tanzania (Bara) ingawa Mahkama Kuu ya Zanzibar na Tanzania (Bara) zina mamlaka sawa, lakini kuwa wakili wa Mahkama Kuu, Zanzibar hakutambuliwi. Aidha Makao Makuu ya taasisi zote hizo yapo upande mmoja wa Muungano. Mashirika haya sio tu kuwa yanatoa fursa za ajira lakini yanatumia fedha nyingi sana kufundisha wafanyakazi wake kuliko fedha zinazotumiwa na bajeti ya SMZ kufundisha watumishi wake. Hivyo kama taasisi hizo ni za Muungano kwa nini Mshirika mmoja asifaidike na fursa hizo?

Maelezo haya yanaweka bayana suala ambalo
halijapatiwa jibu la nini maana ya jambo la
Muungano?

3.3 NINI MAANA YA MTU ANAYETOKA ZANZIBAR/TANZANIA BARA.

3.3.1 Moja kati ya zilizokuwa nguzo kuu za Muungano ni ile ya uwakilishi wa Zanzibar ndani ya Muungano kupitia Rais wa Zanzibar ambaye alikuwa Makamo wa Rais wa Muungano kwa kupitia wadhifa wake wa Urais wa Zanzibar. Baada ya Marekebisho ya 11 ya Katiba Rais wa Zanzibar aliondolewa katika nafasi ya Makamo wa Rais kwa kupitia wadhifa wake. Badala yake Makamo wa Rais anapatikana na utaratibu wa Mgombea Mwenza. Chini ya ibara ya 47(3) ya Katiba ya Muungano, Mgombea Mwenza anateuliwa kwa Kanuni kuwa iwapo Rais ni mtu anayetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais awe ni mtu anayetoka upande wa pili wa Muungano.

3.3.2 Suala ni kuwa mtu anayetoka upande mmoja wa Muungano ni sifa ya uzawa, ukaazi au ya mahusiano? Mtu anaweza, kwa mfano kutoka Zanzibar kwa sababu ya kuzaliwa ama kwa sababu ameishi Zanzibar au kwa sababu wazazi au mmoja wa wazazi wake ametoka Zanzibar lakini yeye mwenyewe hajazaliwa wala hajawahi kuishi Zanzibar.

3.3.3 Nafasi ya Urais (iwe Rais au Makamo) ni muhimu katika Muungano, Ni moja ya nguzo zake kuu. Aidha Katiba ndio muongozo wa uteuzi wake. Hivi sasa kuna madai kuwa hakuna utaratibu wa kubadilishana zamu za Urais baina ya Bara na Zanzibar kwa vile haijaelezwa ndani ya Katiba wala Sheria yoyote. Kutokana na utaratibu uliopo (angalau ndani ya CCM) ya uteuzi wa mgombea Urais, tunaanza kuandika Kanuni kuwa Zanzibar itaendelea kutoa Makamo wa Rais. Lakini kwa vile maana ya mtu anyetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano hajafafanuliwa ndani ya Katiba, kesho itakuja Hoja kuwa neno hilo halikutafsiriwa ndani ya Katiba wala Sheria, hivyo sifa moja yoyote ya uzawa, ukaazi au uhusiano inafaa. Sijui kama kuanzia hapo patakuwa tena na Muungano huu tunaoujua leo. Njia rahisi ilikuwa ni kusema kwamba mtu anayetoka Zanzibar ni yule ambaye ana sifa ya kuwa Mzanzibari chini ya Sheria za Zanzibar.

3.3.4 Serikali ya Muungano ilikataa wazo hilo kata kata wakati wa kujadili Muafaka baina ya SMZ na SMT hapo mwaka 1994. Kamati ya Shellukindo iliwahi hata kupendekeza Sheria ya Mzanzibar ifutwe kwa vile inatoa dhana ya uraia wa aina mbili (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.6 la Ripoti ya Shellukindo). Serikali ya Muungano hata hivyo katika muafaka wa 1994 ilikubali kuwa kuifuta Sheria hiyo ni makosa, na hivyo iendelee kuwepo kwa vile ndiyo inayofafanua nani ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa Zanzibar. (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.2.2.1 ya Taarifa ya Muafaka).

Hivyo suala hili muhimu halina majibu ndani ya Katiba na Sheria zetu na ni wazi kuwa ni mbegu ya mzozo wa baadae.

3.4 JEE TANZANIA INA UCHUMI MMOJA AU CHUMI MBILI

3.4.1 Ingawa katika Kitabu cha Muafaka baina ya SMT na SMZ inaeleza kuwa “Tanzania ni nchi moja yenye uchumi mmoja wenye mazingira tofauti” lakini katika utekelezaji Serikali zote mbili zinaonyesha kuwa na jibu tofauti – kwamba uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni tofauti. Hata katika hali halisi ndivyo ilivyo. Mtafaruku uliopo unatokana na ukweli kwamba ingawa chumi ni mbili lakini nyenzo zote kuu za uchumi zinadhibitiwa na Serikali ya Muungano. Nyenzo kama vile udhibiti wa sera za fedha, kodi na mahusiano na nchi za nje hazimo mikononi mwa Zanzibar ingawa Zanzibar inategemea ijiendeshe kiuchumi.

Dalili au sababu zinazoonyesha wazi kuwa Tanzania ina chumi mbili ni pamoja na zifuatazo:

(i) Masuala ya Maendeleo ya Uchumi sio ya Muungano; hivyo kila upande una Wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake.

(ii) Kila upande una Mfuko wake Mkuu wa Serikali na hivyo mapato yake.

(iii) Kila upande una jukumu la kushughulikia huduma za jamii, miundo mbinu n.k.

(iv) Kila upande una Sera na Sheria zake za biashara na uwekezaji na hata Sheria za ajira.

Pamoja na ukweli huo Katiba ya Muungano haiweki bayana na ndio inayofanya kusiwe na majibu ya wazi ya suala hili kwa sababu zifuatazo:

(i) Kodi ya Mapato, Mikopo ya nje na Biashara za Nje bado yamefanywa ni mambo ya Muungano. Kodi ya Mapato ambayo ni nyenzo kuu ya uchumi wa visiwa ambao ni “Service oriented” badala ya kuwa “resource based” kama ilivyo kwa Bara, bado ni jambo la Muungano kisera, ingawa mapato halisi yanatumika Zanzibar.

(ii) Sera za fedha na mahusiano ya kikanda yapo chini ya Serikali ya Muungano bila ya kuwa na uwazi wala Sheria inayoilazimisha kushughulikia maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar.

3.4.2 Kutokana na kutokuwepo majibu ya wazi na pia kuwepo mtafaruku ya lipi hasa ndio sahihi, ndio maana Kero za Muungano zinaonekana kuzidi badala ya kupungua kwani maisha ya watu hasa wa Zanzibar yamedidimia kutokana na uchumi wa Zanzibar kuanguka kutokana na zao la karafuu kushuka bei. Mategemeo pekee ya kiuchumi au uwekezaji katika nyanja zote hasa za huduma. Hata hivyo Zanzibar haiwezi kuweka sera huru na za kuvutia za kiuchumi kuliko Tanzania Bara kwa vile haina mamlaka katika eneo hilo. Mfano mzuri ni kushindwa kwa miradi ya EP2, Bandari Huru na Off-Share Companies.

4.0 HITIMISHO
4.1 Muungano wetu hautalindwa kwa siasa na kuusifu pekee na kuwaita wale wanaoukosoa kuwa ni maadui wa Muungano ingawa wapenzi wa Muungano wenyewe wanazikubali kasoro hizo hizo na hata wameziandika na kuzifanyia vikao. Muungano utalindwa kwa kuwekewa misingi madhubuti iliyo wazi na ambayo italindwa kwa misingi ya Katiba na Sheria inayokubalika na ambayo itatokana na ridhaa za washirika wa Muungano.

4.2 Mifano ipo mingi. Muungano wa Uingereza (England) na Scotland ingawa ulianzia mwaka 1603 lakini ulijadiliwa rasmi mwaka 1705 na kuanzishwa rasmi kisheria mwaka 1707. Hata hivyo miaka ya 1990 imeshuhudia ukizungumzwa tena na kuafikiwa kurejeshwa kwa Bunge la ndani la Scotland. Aidha, kwa upande mwengine, ingawa Uingereza iliungana rasmi na Ireland mwaka 1800 kwa Sheria ya “Union of Great Britan and Ireland” lakini kwa kukosekana misingi madhubuti mwaka 1922 majimbo 26 yalijitoa katika Muungano na kuanzisha Irish Free State ambayo sasa ni Ireland. Mfano mwengine, ambao pengine si mzuri ni ule wa Canada na Uingereza. Ingawa Canada ilipewa hadhi ya kuwa Dominion kupitia Sheria ya British North America Act ya 1867 lakini bado kulikuwa na matatizo mengi ambayo yalifanyiwa kazi ambako kulipelekea kutungwa Sheria ya kuweka bayana masuala yenye mzozo kwa Sheria ya Statute ya Westminster ya 1931.

4.3 Hali ni tofauti katika Muungano wa Tanzania ambapo marekebisho mengi ya kikatiba, kishera na kisera yanafanya Muungano kuwa na matatizo zaidi kwa vile kiini cha Kero za Muungano hakijashughulikiwa. Masuala ambayo hayana majibu ni mengi ndani ya Muungano.

4.4 Niliyoyaeleza ni mifano tu ya masuala hayo mengi. Kinachojidhihirisha ni kuwa tatizo sio la idadi ya Serikali tu lakini ni zaidi ya hapo. Tatizo la msingi ni lile la Kanuni za msingi za Muungano kutozingatiwa na kutopatiwa majibu. Kutokana na Kasoro hizo ndio maana Muungano wetu kama ulivyo hivi sasa hauwezi kuhimili mabadiliko ya kisiasa.

4.5 Hakuna Muungano madhubuti ambao unategemea kulindwa na sera za chama. Muungano madhubuti ni ule unaolindwa na misingi madhubuti, uwazi na wenye majibu kwa masuali yanayohusu nguzo kuu za Muungano huo.

Othman Masoud Othman ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Share: