Habari

Matawi ya CUF yavamiwa usiku, bendera zachanwa

Picha kutoka mitandao ya jamii Baraza za CUF, Shehia ya Muwambe, Kusini Pemba wakati wa ziara ya Maalim Seif Mkoa wa Kusini Pemba, Mwaka 2017. Picha haihusiani na hujuma za kuchanwa kwa bendera za CUF, Uzi Kusuni Unguja.

Kutoka Uzi, Unguja
Jumatano, Februari 20, 2019

Siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kufutilia mbali bodi ya wadhamini ya CUF iliyoteuliwa na Profesa Ibrahim Lipumba, watu wasiojulikana katika shehia ya Uzi, Kusini Unguja wamevamia matawi mawili na baraza tatu (maskani) za wanachama wa chama hicho na kuchana bendera usiku wa kuamkia Jumanne, Februari 19, 2019.

Hujuma dhidi ya matawi ya CUF ya shehia hiyo, imefanyika wakati Dk Shein alipofanya ziara katika wilaya hiyo leo Jumatano, Februari 20 na kutembelea kisiwa cha Uzi, ambako aliweka jiwe la msingi la skuli ya maandalizi na msingi Ng’ambwa na baadae kuwahutubia wanaCCM wa Uzi na viongozi aliyofutana nao.

Kisiwa cha Uzi ni moja ya ngome kubwa ya Chama cha Wananchi (CUF) tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992. Inawezekana kufuatia ziara ya Dk Shein ndiyo chanzo kilichopelekea kuhujumu kwa matawi ya CUF.

Akizungumza Mjini Zanzibar, Jana Februari 19 Mkurugenzi wa Habari wa CUF Jimbo la Tunguu, Juma Ali amesema hawajatambua ni nani waliyohusika kufanya hujuma hizo kwa kuwa tukio hilo limefanyika usiku wa manane.

Amesema matawi mawili na baraza tatu za wanachama wa chama hicho milingoti ya bendera imekatwa na baadhi ya bendera kuchukuliwa na watu wasiyojuilikana.

“Kwa vile chama chetu kinaheshimu na kutii sheria hatutafanya lolote lile lililo kinyume cha sheria badala yake tutalifikisha suala hili sehemu husika,” amesema Juma.

Ameongeza: “Kwa sasa tunajikusanya kwa ajili ya kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi Tunguu ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria huku tukiamini kuwa waliofanya haya watadhibitiwa na kufikishwa kunakohusika.”

Baadhi ya wanachama wa CUF katika shehia hiyo walieleza kushangazwa na tukio hilo kwa vile wamekua wakifanya siasa kwa muda mrefu bila ya kugombana.

“Shehia ya Uzi ina wanachama kutoka vyama tofauti na kwa muda mrefu matukio ya kuchaniana bendera hayajatokea hivyo tunashangazwa na kitendo hiki, huenda waliofanya wamedhamiria makubwa zaidi,” alisema Ali Shaibu.

Mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho, Salim Bimani alipoulizwa alisema amepokea taarifa hizo na kwamba anashangazwa na tukio hilo ambalo anaamini lisingeweza kutokea wakati wa sasa.

Alisema kwamba tukio hilo si la kiungwana na kuwataka wanachama wa chama hicho kutokubali kuingizwa kwenye mitego ambayo alidai kuna watu wamedhamiria kufanya uchokozi ili utokee ugomvi ambao utakuwa na madhara makubwa kwao.

Share: