Habari

Mazombi kuvamia viongozi 70 wa CUF usiku wa leo

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Baada ya kufanikiwa aliyekuwa mkurugenzi wa habari wa CUF – Chama cha Wananchi wilaya ya Magharibi A Unguja wiki iliyopita, sasa askari wa vikosi vya serikali ya Ali Mohamed Shein maarufu kama mazombi wanaripotiwa kwamba wamepanga operesheni kubwa ya kuwavamia viongozi 70 wa chama hicho usiku wa leo Alhamisi tarehe 5 Oktoba 2017.

Chanzo chetu kinaeleza kuwa tayari baadhi ya viongozi hao wa CUF wameshajulishwa na wasamaria wema ndani ya serikali ya Shein juu ya mpango huo, na wengine wameshaanza kuchukuwa hatua za tahadhari.

“Wameamua kuwa lazima wawaumize viongozi wengi wa CUF kwa wakati mmoja. Wameona kuwa kumshambulia kiongozi mmoja mmoja kama walivyofanya kwa Marehemu Ali Juma hakutoshi kujenga mazingira ya hofu au hata kuwaingiza vijana wa CUF kwenye mapambano. Sasa operesheni hii itafanikisha azma yao haraka”, kinasema chanzo hicho.

Mmoja wa viongozi wa CUF waliotajwa kuwa kwenye orodha hiyo ya watakaoshambuliwa amekiri kuambiwa jambo hilo, lakini akasema kwamba haamini kuwa serikali ya CCM itafanya “upuuzi huo, hasa sasa ikiwa ni wiki moja tu tangu tumzike mwenzetu”, akikusudia Ali Juma Suleiman, ambaye alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja siku ya Alhamis iliyopita, baada ya kuchukuliwa nyumbani kwake Mtopepo usiku wa Jumanne na mazombi.

Alipoulizwa mpashaji habari wetu ikiwa polisi inajuwa kuhusu njama hizo, alisema kuwa “vyombo vya dola vinaonekana aidha kujuwa na vinayaacha yaendelee au vimezidiwa na shinikizo la kisiasa kutoka kwa kundi la viongozi wa serikali ya Dk. Shein walioasisi makundi haya.”

Habari hizi zinakuja katika wakati ambapo wafuasi wa CUF kote Zanzibar hivi sasa wamekaa katika hali ya kungojea jambo kubwa kutokea, kwa mujibu wa katibu mkuu wao, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye amewajengea matumaini kuwa kutakuwa na mabadiliko ya uongozi wa nchi ndani ya siku chache zijazo.

“Hali hii imewatia wasiwasi sana viongozi wa serikali ya Shein. Wanajiuliza huu ujasiri wa viongozi wa CUF kupita wakiwaambia watu wao kuwa kunakuja mabadiliko wameutoa wapi? Watu wao wamehamasika Zanzibar nzima. Sasa wanataka kuwatia adabu na kuwaonesha kuwa wao ndio wenye serikali”, kinasema chanzo hicho.

Tagsslide
Share: