Habari

Mbarawa ajiandaa kumrithi Dk Shein kwa uovu, chuki na ubaguzi dhidi ya Wazanzibari

Ijumaa, Novemba 17, 2017

WAZIRI wa Serikali ya Muungano anayehudumu katika Wizara ya Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewadhalilisha Wazanzibari baada ya waziri wa zamani wa fedha, Saada Mkuya kutoa mapendekezo ya kutaka ajira kwa shirika la mawasiliano la simu kwa upande wa Zanzibar, ziwe kwa Wazanzibari tu.

Profesa Mbarawa katika kujibu mapendekezo yaliyotolewa na Saada Mkuya (Mbunge wa Welezo, Unguja) alisema alitegemea hoja ya aina hiyo ingezungumzwa na watu wa vijijini, Pemba au vijiweni Darajani, Unguja na siyo Saada.

Profesa Mbarawa alionekana kituko katika Kikao cha Bunge cha Jioni Siku ya Jumatatu, Novemba 13, 2017 wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia Muswada wa Shirika la Mawasiliano wa 2017, uliowasilishwa bungeni na yeye mwenyewe (Profesa Mbarawa).

Alisema: “Utaratibu wa ajira TTCL ni Mtanzania yeyote anafanya kazi TTCL. Tunachoangalia sisi muhimu ni uwezo wa mtu na sifa za mtu.”

“Ni jambo ambalo limenishtua sana na sikutegemea Mhe Saada angalisema vile kwamba anataka TTCL Zanzibar, ifanywe na Wazanzibari wenyewe tu.”

“Hicho kitu sikutegemea hasa kutoka kwa kiongozi kama Mhe Saada ambaye amekuweko serikalini. Hasa kutoka kwa kiongozi kama Mhe Saada ambaye anauzoefu mkubwa,” alisema Profesa Mbarawa na kuongeza:

“Nilitegemea mawazo au maoni kama yale yazungumzwe na watu wa kijijini kule Pemba. Nilitegemea mawazo kama yale yazungumzwe na watu wa kijiweni pale Darajani. Sikutegemea kabisa,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema: “Nilitegemea yeye (Saada) kama kiongozi na sisi kama Tanzania katika kujenga umoja wetu tuseme kila Mtanzania aweze kufanyakazi mahali popote Tanzania.”

“Mheshimiwa Naibu Spika hivi tunavyoongea leo Meneja wa TTCL Zanzibar ni Mzanzibari anaitwa Mohamed Mohamed. Meneja wa TTCL Pemba ni Mzanzibari anaitwa Ngwali Khamis,” alisema Profesa Mbarawa.

“Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Saada, hazijui kiutendaji.  Mtendaji Mkuu wa TTCL mwaka 2010 mpaka 2012 alikuwa Injinia Said Ameir ambaye miye ni mwalimu wangu ni Mzanzibari.”

Alisema: “Sasa sikutegemea nasema tena ni kitu kimeniuma sana. Nilitegemea kama Mtanzania unatoka Lindi kama kuna fursa TTCL Zanzibar unaenda. Kama Mzanzibari ameona fursa Kibondo aende.”

“Hii ndio Tanzania tunayoitaka. Hii ndio Tanzania Watanzania kule nje wanayoitaka. Nikienda zaidi TTCL tuna TTCL Pesa ina watendaji watano waandamizi. Watanzania watatu ni Wanzanzibari,” alisema Profesa Mbarawa na kuongeza:

“Mkuu wa mahusiano (head of compliance), anaitwa Ndugu LULU ni kutoka Zanzibari, Bw Rashid Khamis au Khamis Rashid anatoka Zanzibari ni mkuu pale, Ndugu Nasra Mugheiry (pengine ni ndugu yetu) anatoka Zanzibaa.”

“Sasa leo tunapeleka ‘message’ kwamba hawa wote tuwatoe tuwapeleke Zanzibar ama Pemba, sio sahihi hatuwatendei haki Watanzania.”

Alisema: “Sisi viongozi tuoneshe mfano, hasa sisi tulioko serikalini na wengine waliyokaa serikali wanajuwa utaratibu Watanzania wote ni wamoja lazima tujenge umoja.”

“Nataka nimuhakikishie Mhe Saada, serikali ya SMZ, itam-‘support’ kiongozi yeyote ambaye anafanyakazi TTCL Zanzibar au Tanzania nzima. Haitambagua Mtanzania yeyote. Naomba alifahamu hilo na Waheshimiwa wabunge wote naomba mlijue hilo,” alisema profesa Mbarawa.

Jitihada za Saada Mkuya, kutaka kumpa Profesa Mbarawa taarifa inayohusu ajira kwa upande wa Zanzibar, ziligonga mwamba baada ya Naibu Spika, kumweleza kuwa kikanuni waziri akiwa amesimama kwa hatua kama ile ya Jumatatu, 13/11/17, hakuna taarifa.

SHEIN NA MBARAWA NI MBWA MWITU WALIOVAA NGOZI ZA KONDOO.
Baada ya majibu ya Profesa Makame Mbarawa dhidi ya Saada Mkuya na Wazanzibari wengine, ni wakati wa kufanya uchambuzi kwa Wazanzibari aina ya Profesa Makame Mbarawa waliyomo ndani ya madaraka na wanaotaka madaraka makubwa zaidi ya uongozi kwa siku zijazo.

Profesa Mbarawa na Dk Ali Mohamed Shein wanajidai kuwa wanaasili ya Pemba, jambo ambalo kuliamini moja kwa moja ni shida, si-rahisi. U-Pemba wao hauko wazi, unamashaka na utata.

Kuna msemo: ‘mdharau kwao ni mtumwa’ Profesa Mbarawa, tayari ameshakudharau kwao kwa maelezo yake ya kuwadharau Wapemba wa vijijini. Profesa Mbarawa anavyojidai anatoka kijiji cha Mkanyageni, Kusini Pemba.

Profesa Mbarawa katika maelezo yake hapo juu, kuhusu wazo la Saada Mkuya, kwamba ajira zote za TTCL kwa Zanzibar, waajiriwe Wazanbari tu. Hili ndilo lililomshtua na kumsikitisha Profesa Mbarawa, anayejinasibu kwamba kwao ni Mkanyageni, Pemba.

Profesa Mbarawa, hilo limemuhuzunisha sana hadi kufika kuona kwamba mawazo ya Saada Mkuya, yanafanana au yanastahili kuwa mawazo ya Wapemba wa vijijini ambao kwa mujibu wa Profesa Mbarawa Wapemba wa vijijini ni wajinga na mawazo yao hayawezi yakasaidia katika masuala ya kujenga nchi. Mawazo ya Wapemba wa vijini, hayahitajiki na viongozi kama Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa, aliwahi kuwania ubunge, Jimbo la Mkanyageni, Pemba katika uchaguzi ulifanyika mwezi wa Oktoba 2015. Wananchi wa Mkanyageni, hawakuhafilika walisema ‘hawafugi mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo.’

Kadhalika, wananchi hao hao wa Mkanyageni, waliwahi kumpiga na chini mara mbili, Dk Ali Mohamed Shein alipojaribu kugombea Ujumbe wa Baraza la Uwakilishi. Hapa, tunapata picha kuwa Dk Shein na Profesa Mbarawa, Pemba si kwao. Hilo si jambo la kuogopa kulizungumza.

Kuna taarifa za chini kwa chini kwamba Profesa Makame Mbarawa ameahidiwa atapokea kijiti cha Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutoka kwa Dk Ali Mohamed Shein, hapo 2020.

Ni kwa sababu hiyo Profesa Mbarawa, anakuwa mkali, kiburi na kuwadhalilisha Wazanzibari kwa sababu ndiyo hulka na tabia wanayofundishwa na mabwana zao wa CCM ya Tanganyika.

Kila mbunge au kila kiongozi kutoka Zanzibar, anapojaribu kusemea maslahi ya Wazanzibari kwenye jambo lolote, huwajia juu kwa maneno ya kejeli na dharau. Mfano wa karibu ni huu wa Profesa Mbarawa.

Kwa kanuni za CCM Tanganyika, wanampa urais wa Zanzibar mtu, ili kwende kufanyakazi kwa maslahi ya Tanganyika wala si kwa maslahi ya Wazanzibari wenye nchi yao. Hilo ndilo wanalolitekeleza Dk Shein na viongozi wenzake wa Zanzibar, waliyopo madaraka.

Profesa Mbarawa kwa kauli ya kufoka aliyoitoa bungeni Jumatatu, Novemba 13, katika kikao cha bunge cha jioni akijibu hoja za Saada Mkuya (Mbunge wa CCM – Zanzibar), anaonekana tayari anatekeleza matakwa ya mabwana zake wa Tanganyika. Kauli yake imeegemea katika kujipendekeza, akitarajia kuwa Rais wa Zanzibar.

Kwa falsafa iliyozoeleka ya Viongozi wa Watanganyika ili kwao mtu aaminiwe kuwa Rais wa Zanzibar, lazima mtu huyo awe ni adui wa Wazanzibari na kuwa mtiifu kwao kwa kupeleka maslahi ya Zanzibar,  Tanganyika.

Uamuzi wa wananchi wa Mkanyageni, Pemba kutokuwachagua Dk Shein na Profesa Mbarawa, ndiyo sababu zinazofanya kuonekana wanafaa kuwa ma-Rais wa Zanzibar. Watanganyika wanaamini adui wa Zanzibar, ndiye rafiki yao na ndiye mwenye maslahi na Tanganyika.

Mifano ipo: Kiongozi wa Zanzibar kwa maana Rais wa Zanzibar, awe tayari kujenga siasa za kuwagawa, siasa za kibaguzi, siasa za uonevu  na chuki miongoni mwa wananchi wa Zanzibar wenyewe kwa wenyewe.

Na hicho ndicho wanachokifanya viongozi wa Zanzibar, waliyopo madaraka. Kitaendelezwa na Profesa Mbarawa, muda ukifika. Maneno yake ya uchafu ya Bungeni Dodoma, Jumatau jioni 13/11/17 ya kuwadhalilisha Wazanzibari, hususan Wapemba, hayatasahaulika hadi siku ya kiama.

Kiongozi wa Zanzibar, anayetakiwa na CCM Tanganyika ni yule anawatesa wananchi wa Zanzibar kwa kuwaweka magerezani kwa uonevu kwa udhalilishaj. Kama inavyoshuhudiwa sasa kwa Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho. Wanafikisha miaka minne ndani ya gereza.

Hata hizo enzi za tawala za kifalme, haikuwa kutokea Mzanzibari kupelekwa Tanganyika kwenda kudhalilishwa pasina sababu bali ni ushenzi na kukosa utu.

Si rahisi kuamini kuwa viongozi wa Zanzibar ni waislamu. Hakuna muislamu mwenye madaraka au mtawala, anayeridhika kusimamia mateso ya mwiislamu mwenzake, bila kosa au sababu.

Masheikh wale hawakumkufuru Mwenyezi Mungu, mtukufu wa mbingu na ulimwengu. Kama walifanyamakosa ni makosa ya kidunia yanayosameheka na kusahaulika. Hasa ni kitu gani walichokosea kinachofanya serikali za CCM, kushindwa kuwasamehe na kuwaachia huru kuishi na familia zao.

Wafalme wote waliyotawala Zanzibar, hawakuwahi kuwatesa raia zao kama ambavyo inatokea sasa kwa Wafalme wa CCM.

Kwa kumalizia, nikirudi kwa Profesa Mbarawa, maelezo yake dhidi ya Saada Mkuya na Wazanzibari, tayari ameanza kutekeleza matwaka ya CCM Tanganyika.

Profesa Mbarawa, anamatarajio ya kuwa Rais wa Zanzibar, ili kuendeleza maonevu, mateso, chuki na ubaguzi atakaorithi kutoka kwa Dk Shein na wasaidizi wake. Wazanzibari akiwemo Saada Mkuya, wemeshikamana na kamba ya Allah.

 

 

Tagsslider
Share: