Habari

Mbunge anapohamia CCM anabadilika sana

Picha na maktba ya mzalendo.net: Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akiwa na Mbunge wa Temeke wa CCM, Abdallah Mtolea

Jumapili, Aprili 28, 2019

Binadamu kubadilika ni mara moja, chambilicho Wapemba katika msemo wao: ‘Binadamu kubadilika si kazi’ Baadhi ya binadamu kubadilika ni mara moja. Lakini kuna mambo mengi yanayomfanya mtu kubadilika.

Baadhi ya watu hubadilika kutokana na sababu za lazima, kama hofu, woga na vitisho lakini, baadhi ya watu ama hubadilika tabia na kauli zao kutokana na mambo mengi kama kukata tamaa, shida na njaa, utapeli wa kupenda madaraka na fedha, kukosa malengo na tabia ya unafiki.

Watu wengi wanajiuliza kwa mtu kama Humphrey Polepole (Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi), kauli alizokuwa akizitoa alipokuwa Mjumbe/Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba, na kauli zake za sasa baada ya kushika wadhifa huo aliyonao. Inashangaza sana, huamini kuwa ni mtu mmoja yuleyule.

Nimeona niweke kitangulizi cha maneno haya, ili kuunga mkono makala iliyopo chini iliyotoka katika Gazeti la Mwananchi la siku ya Jumatano, Aprili 24, 2019 Mwandishi ni Luqman Maloto.

MAKALA YA MALOTO: Mbunge anapohamia CCM anabadilika

Wasomi wa sayansi ya mfumo wa fahamu watakuwa wanajua nadharia inayoitwa “Dual Consciousness”, kwamba baadhi ya watu hutokea kuwa na ufahamu wa aina mbili kutokana na ubongo kuwa na sehemu mbili zenye kutofautiana.

Sehemu ya kushoto ya ubongo inaweza kuwa na ufahamu wake na ile ya kulia ikawa na mapokeo tofauti. Matokeo yake inakuwa sawa na watu wawili ndani ya mwili mmoja.

Upande huu unaweza kuchakata mawazo na kuyatoa, upande wa pili ukaibuka na kuyapinga. Mtu mmoja anakuwa anajipinga mwenyewe utadhani ni watu wawili wanapingana. Hata hivyo, sayansi hii bado inaelea.

Maana wanasayansi hawajakubali kuithibitisha nadharia hii wala kuikataa. Inaendelea kuaminika kuwepo bila uthibitisho wa kisayansi.

Inaweza kuwa si matokeo ya Dual Consciousness, lakini inashangaza jinsi ambavyo mbunge ambaye amehama kutoka chama upinzani na kuhamia CCM anavyobadilika. Hoja aliyotoa alipokuwa upinzani, anaipinga mwenyewe baada ya kuwa CCM.

Hutaacha kujiuliza, amebadilika kisiasa mpaka namna ya kufikiri? Je, anakuwa na aina mpya ya ubongo, kwa hiyo ufahamu wake ni tofauti na mwanzo hata jinsi anavyotafsiri mambo?.

Aprili mwaka jana, katika Bunge la Bajeti 2018-2019 Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea wakati huo akiwa CUF, alipokuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, alikosoa vikali muundo wa muungano.

Mtolea alisema katika sherehe za Mapinduzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano hupokwa mamlaka yake na kuingia uwanjani mapema, kisha itifaki ya mamlaka hupewa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kuingia wa mwisho uwanjani na kupigiwa mizinga 21, kipindi hicho Rais wa Tanzania yupo jukwaani.

Alifafanua kuwa kitendo hicho cha Rais wa Zanzibar kupewa heshima ya kiitifaki kwa kubakizwa wa mwisho kuingia uwanjani na kupigiwa mizinga ya kijeshi ni cha uvunjaji wa katiba, kwa sababu Rais wa Tanzania ndiye Mkuu wa Nchi, kwa hivyo ndiye mwenye kustahili heshima hiyo.

Kwenye mchango wake hakutumia Tanzania Bara, badala yake alitumia jina Tanganyika. Na hata alipoongozwa na kiti kutumia neno Tanzania Bara, hakubadili.

Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, kipindi akiwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliwahi kuzungumza kwenye kongamano la utoaji wa maoni ya katiba kuwa haihofii Zanzibar kwa sababu kero zao karibu zote zipo mezani na zinajadiliwa.

Lakini, alisema anaihofia Tanganyika siku wakianza kudai haki zao inaweza kutokea hatari kubwa.

Mtolea pia alirejea nukuu hiyo ya Profesa Kabudi na kuzidi kujenga hoja kwamba Muungano una changamoto nyingi ambazo hazipatiwi majibu.

Zaidi, aliwapongeza wabunge wa Zanzibar kwa kile alichoeleza kwamba husimama pamoja kuipigania Zanzibar yao na ndiyo maana serikali hujibu kero za Zanzibar kama suluhu ya Muungano.

Mtolea mwaka huu

Novemba mwaka jana, Mtolea alihamia CCM. Alipewa tiketi ya chama hicho, akagombea ubunge na kurejea bungeni kuendelea kuiwakilisha Temeke.

Bunge la Bajeti 2019-2020 linaloendelea, Mtolea akichangia bajeti ya wizara ileile, alisema Muungano wa Tanzania ni wa kipekee na unapaswa kuenziwa.

Bila kutaja kero yoyote, alisema mazingira na historia ya Muungano wa Tanzania huwezi kufananishwa na mwingine wowote kwa sababu ni wa kipekee.

Alisema, CUF ndiyo hawataki muungano kwa sababu ina sera ya kutaka mamlaka kamili kwa kila upande wa muungano.
Mtolea aliwakosoa wabunge wa Zanzibar kuwa wanabebwa kwenye muungano.

Hivi sasa Mtolea amebadilika, anasema Muungano wa Tanzania ni wa kipekee dunia nzima na amewaponda Wazanzibari wanaolalamika, kwamba wanabebwa na Tanzania Bara.

Mwaka jana aligoma kutamka Tanzania Bara, mwaka huu hajatamka Tanganyika. Ameita Tanzania Bara na Zanzibar, aliita Tanzania Visiwani. Je, Mtolea ni watu wawili kwenye mwili mmoja?

Share: